• HABARI MPYA

    Tuesday, February 03, 2009

    YANGA: TUTAJIENDESHA KWA MAPATO YA MILANGONI

    KLABU ya soka ya Yanga, imedai makusanyo yanayopatikana katika mechi zake za ligi kuu na mashindano ya kimataifa yanatosha kuifanya ijiendeshe, endapo itathibitika kwamba mfadhili wake mkuu, Yussuf Manji, amejitoa.
    Pamoja na kukiri kwamba hana taarifa rasmi za kujitoa kwa mdhamini huyo, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Imani Madega, alisema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba mkataba wa Manji kwa Yanga, ulihusu mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi na si zaidi ya hapo.
    “Kuna watu hawaelewi kilichopo. Kwa muda wote Manji alisaini mkataba na Yanga wa kuwalipa mishahara wachezaji na benchi la ufundi, kitu ambacho amekuwa akikifanya vizuri kabisa.
    “Linapokuja suala la ukarabati wa jengo, usafiri wa timu kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani, kuiweka timu kambini pale Lamada Hotel na misaada mingine, yeye alikuwa akitoa kama ambavyo mpenzi ye yote wa Yanga anaweza kufanya, halazimishwi na mkataba.
    “Lakini pia ni vyema watu, hasa wanachama wa Yanga wakafahamu kwamba, mtoto huzaliwa na kukua, huwezi kutegemea kusaidiwa kila siku. Manji amefanya vitu vingi sana kwa klabu hii. Ametulea katika kipindi kigumu, wakati Uwanja wa Taifa ulipokuwa umefungwa, tulichezea Morogoro ambako fedha za kiingilio zilikuwa ni chache.
    “Sasa tumehamia Dar es Salaam, timu inafanya vizuri mashindano ya ndani na nje, wanachama wanahamasika kuja kuishangilia na fedha zinapatikana. Tunaweza kusimama wenyewe,” alisema.
    Kumekuwa na taarifa za kujiondoa kwa mfadhili huyo katika klabu hiyo, hali inayoweza kuwatisha wanachama na wapenzi wa mabingwa hao wa soka Tanzania Bara.
    Madega alisema uongozi wao upo imara na bado wanamhesabu Manji kama mdhamini wao mkuu, licha ya hivi karibuni kuingia mkataba na kampuni ya bia nchini, TBL. Alisema: “TBL wanatupa Sh milioni 16 kwa mwezi, wakati mishahara ya wachezaji wa Yanga na benchi lake la ufundi ni karibu Sh milioni 40 kwa mwezi. Unataka atupe nini tena zaidi ya hii? Wajibu wetu ni kuangalia jinsi gani tunaweza kusonga mbele kuanzia hapa.”
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA: TUTAJIENDESHA KWA MAPATO YA MILANGONI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top