• HABARI MPYA

    Wednesday, February 25, 2009

    CHUJI SAFI, KUIVAA IVORY COAST LEO

    na abdul mohammed, abidjan
    KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo pamoja na kumkosa kiungo Geoffrey Boniface aliyeumia kwenye mechi dhidi ya Senegal Jumapili wakati timu hiyo ikilala 1-0, kitakuwa na nguvu mpya ya nyota wake wawili, viungo Athumani Iddi ‘Chuji’ na Kiggi Makasy wakati kikimenyana na wenyeji, Ivory Coast, Uwanja wa Felix Houphouet Boigny mjini hapa.
    Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela alisema jana kwamba Chuji yuko fiti na atakuwamo kwenye kikosi cha kwanza cha Stars leo sawa na Kiggi Makasy.
    Mchezo huo wa Kundi A leo ni muhimu kwa timu zote ili kujitengenezea mazingira ya kuingia Nusu Fainali ya michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), hasa ikizingatiwa zilipoteza mechi zao za kwanza.
    Wakati Tembo wa Ivory Coast walilala kwa Chipolopolo wa Zambia 3-0 kwenye mchezo wa ufunguzi, muda mfupi baadaye Tanzania ilipigwa 1-0 na Simba wa Teranga.
    Kocha wa wenyeji, Georges Kouadio anaamini leo timu yake itaibuka na ushindi mbele ya Tanzania katika michuano hii inayokutanisha wachezaji wanaocheza Ligi za nchini mwao pekee.
    “Tuntakiwa kushinda dhidi ya Tanzania ili kurejesha matumaini ya kusonga mbele, na tutajaribu kufanya kila kinachowezekana kuhakikisha tunafanya hivyo,” alisema.
    Kocha wa Tanzania, Marcio Maximo, ambaye amekuwa akisema kwamba anawaheshimu wenyeji wa michuano hiyo kama miongoni mwa wapinzani wa kweli, amesema watapigana kufa na kupona kuhakikisha nao wanashinda ili kujiweka sawa.
    Maximo alisema kwamba timu yake itatumia mambo mawili ili kuweza kuibuka na ushindi katika mechi ya leo dhidi ya wenyeji Ivory Coast. Stars leo itaumana na wenyeji hao wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN).
    Maximo aliyataja mambo mawili ambayo atayatumia leo kuwa ni presha ya wenyeji kutokana na kuwa nyumbani na pili ni presha ya timu hiyo kufungwa mabao 3-0 na Zambia katika mechi yao ya kwanza.
    “Watacheza wakiwa katika presha, tunachotakiwa kufanya sisi ni kuutumia huo udhaifu wao ili tuweze kuwafunga," alisema Maximo. Alisema kwamba watahakikishaa wanacheza pasi za haraka haraka na kutumia zaidi mipira ya chini huku wakiwa makini katika kujihami na kushambulia kwa haraka.
    "Kinachotakiwa kwetu ni kutulia, kumumiliki mipira na kucheza pasi za chinichini kwa haraka," alisema. Maximo alisema kwamba morali ya wachezaji iko juu na anaamini kwamba hali hiyo itawasaidia kuibuka na ushindi lakini zaidi ni kutumia udhaifu wa wenzetu ambao kwa sasa wamejaa presha yya kutaka kushinda; Akizungumzia majeruhi katika timu yake Maximo alisema kwamba mbali na Godfrey Bonny wachezaji wengine ni wazima na leo (jana) jioni alitarajia kuwa na mazoezi ya pamoja.
    Jana (juzi) jioni wachezaji hao walifanya mazoezi mepesi ya kukimbia na kuogelea. Kuhusu Chuji, Maximo alisema mchezaji huyo si kwamba anaumwa sana; maumivu aliyonayo ni madogo lakini anahitaji kuwa katika kiwango sawa na wenzake. "Unajua hakucheza mechi na Zimbabwe, hata katika timu yake ya Yanga nako hakushiriki kikamulifu mechi za timu hiyo, hivyo mbali na kuwa majeruhi lakini hayuko katika kiwango sawa na wenzake," alisema. Hata hivyo Maximo alikataa kutaja kikosi cha wachezaji watakaocheza mechi ya leo akidai kwamba hiyo itakuwa siri yake hadi leo jioni.
    Kuhusu mchezaji Haruna Moshi Boban ambaye aliibua hofu baada ya kucheza chini ya kiwango katika mechi na Senegal kiasi chq kudhaniwa kwamba alikuwa mgonjwa, naye ni mzima wa afya na kwa mujibu wa Kocha Msaidizi, Ali Bushiri, Boban ameshiriki kikamilifu mazoezi ya jana na wenzake.
    Mechi na Ivory Coast ambayo itachezwa saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki itakuwa ya pili kwa Stars ambayo tayari imepoteza mechi yake ya kwanza na Senegal kwa kuchapwa bao 1-0. Zambia ndiyo inayoongoza katika kundi A ikiwa na pointi tatu na mabao matatu wakati Senegal ni ya pili ikiwa na pointi tatu na bao moja, Stars ya tatu ikiwa haina pointi na imefungwa bao moja na Ivory Coast inashika mkia ikiwa haina pointi na imefungwa mabao matatu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHUJI SAFI, KUIVAA IVORY COAST LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top