• HABARI MPYA

    Wednesday, February 11, 2009

    MICHO ALIKUWA KIU YA JIBU YANGA













    WAMEKUJA makocha wengi katika klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, lakini miongoni mwa makocha wa miaka ya karibuni ambao Yanga walimpoteza na alikuwa bora, ni Milutin Sredojevic ‘Micho’.
    Huyu jamaa nilikutana naye mwaka 2003 mjini Kampala, Uganda, tukiwa kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, mwaka huo akiwa anaifundisha SC Villa ya huko.
    Mwaka huo Waandishi wa Habari tuliokwenda huko kutoka Tanzania ni Frank Sanga akiwa Spoti Starehe, kabla ya kuhamia Mwanaspoti, Maulid Kitenge wa Radio One na ITV, Angetile Osiah akiwa Nipashe kabla ya kuhamia Mwananchi, Peter Mwendapole akiwa Uhuru kabla ya kuhamia Bingwa, Philip Cyprian akiwa Clouds FM kabla ya kuhamia TBC, Charles Mateso aliyekuwa Mwanaspoti wakati huo kabla ya kuhamia Champion na mimi ambaye nilikuwa na bado nipo DIMBA.
    Nilitokea kuwa rafiki kipenzi wa Micho na alikuwa akinipa habari nyingi kuhusu yeye na klabu yake, SC Villa.
    Nilikuwa nahudhuria mazoezi ya Villa, namuona Micho anavyofundisha, anavyoishi na wachezaji wake kwa maelewano, namna anavyosimamia nidhamu, maslahi ya wachezaji na kuwa mstari wa mbele katika mipango ya ushindi. Hakika nilibaini mapema, kwamba jamaa ni kocha wa ushindi na mafanikio kwa timu.
    Siku moja kabla ya fainali ya michuano hiyo, iliyozikutanisha Villa na Simba, Micho aligundua kikosi chake hakikuwa sawasawa, wachezaji wake tegemeo akiwemo Mkongo, Ekuchu Kasongo walikuwa wagonjwa.
    Jamaa alipigana kuishawishi CECAFA hadi ikasogeza mbele mechi hiyo kwa siku moja, ili awape nafasi wachezaji wake wapone. Katika mipango yake nilikuwa naye bega kwa bega na baada ya kufanikiwa nilikwenda kwenye internet kutuma stori Dar es Salaam juu ya mechi kuahirishwa.
    Niliporudi hotelini (Motel Lomwe) jioni, niliwakuta waandishi wenzangu wamepumzika wakisubiri fainali kesho yake, nikawaambia tu kwa mzaha; Wazee naona mmepumzika mnajiandaa kwa kuripoti fainali kesho”. Kwa sababu mimi ni mtu ninayependa sana utani, nao walichukulia kama ni utani wa kawaida, ila nilipowaambia kwamba fainali haipo kesho yake kama wanavyodhani, imesogezwa mbele, walitaharuki.
    Jinsi jamaa walivyoinuka na kuanza kwenda mbio kwanza kuthibitisha kwa viongozi wa FUFA na CECAFA na pili kutuma stori Dar es Salaam, kwangu ilikuwa burudani kubwa. Sitasahau.
    Kweli, Micho alifanikiwa kuiwezesha Villa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, kwa ushindi wa 1-0 kwenye Uwanja wa Namboole, bao pekee likitiwa kimiani na mshambuliaji aliyekuwa Yanga kabla ya hapo, Vincent Tendwa (Mkenya), akiunganisha nyavuni krosi ya Shaaban Kisiga ‘Malone’, ambaye baadaye alihamia Simba.
    Kwa hakika Micho alikuwa rafiki yangu mkubwa wakati ule na baada ya michuano tuliendelea kuwasiliana akiwa Uganda mimi nikiwa Tanzania. Aliniambia juu ya nia yake ya kutaka kufundisha soka Tanzania, nami nilianza kuwasiliana na Francis Kifukwe wa Yanga kumuambia kuhusu kocha huyo.
    Mawasiliano kati ya Kifukwe na Micho yalianza siku nyingi, lakini hakuweza kuja kwa wakati aliohitaji mwenyewe, alikuja katika wakati ambao Yanga walimuhitaji, mwaka 2006 akitokea Orlando Pirates ya Afrika Kusini, aliyojiunga nayo akitokea St. George ya Ethiopia. Alikwenda St. George akitokea klabu yake ya kwanza kufundisha Afrika, Villa ya Uganda.
    Nilifurahi rafiki yangu kuja kufanya kazi katika nchi yangu, Tanzania, tena katika klabu niipendayo, Yanga.
    Micho pamoja na kuwa na wachezaji wa ‘hivyo hivyo’, lakini aliweza kupigana na kufikisha Yanga katika hatua ya kuheshimika, aliifikisha Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa na Esperance ya Tunisia kwa mabao 3-0.
    Micho alisema Yanga ilikuwa safi idara zote, kasoro safu ya ushambuliaji tu, hakuwa wafungaji, enzi hizo safu hiyo ilikuwa inaongozwa na watu kama Abuu Ramadhani na Gaudence Mwaikimba.
    Kwa kutolewa kwenye Raundi ya Pili, Yanga iliangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa klabu ya Tanzania kupata nafasi hiyo. Huko nako ilitolewa na El Merreikh ya Sudan kwa kufungwa mabao 2-0.
    Wakati nikiamini kwamba Micho ataisuka Yanga vizuri zaidi na kuanzia msimu wa 2007/08 itakuwa tishio zaidi Afrika, alinipigia simu akiniambia niende kwenye mail yangu nikaangalie ujumbe alionitumia.
    Nilidhani amenitumia habari njema kuhusu usajili wake wa msimu mpya, nilikwenda kwa shauku, lakini nilipoanza kuisoma tu, nilihisi mwili wangu unakufa ganzi. Hii hapa, hebu isome.

    From: SREDOJEVICH MICHO (micoach@hotmail.com)
    Sent: Tue 9/11/07 12:48 PM
    To: princezub@hotmail.com

    Dear Zubeiry
    Being pleased to have an amazing cooperation with you during my spell as a Yanga coach I want to express appreciation to you personally to allow me privilege and honor to count you as a friend, I wish you all the best.
    This bellow is my personal PRESS RELEASE regarding me and Yanga:
    Being privileged and honored to be coach of Yanga, really institution of not only Tanzanian, but even African football and glorious club.
    I made deep analyze of actual situation and I recognized that temporary because of personal problems I can not continue to be coach of Yanga. In respect to everything what I went trough with Yanga, i wish to express sincere and honest appreciation to Yanga players, technical and supporting staff, management of Mr. Kifukwe before and Mr. Madega after, to express special appreciation to sponsor Mr. Yusuf Manji and Yanga supporters for the cooperation assistance and support given to me as a coach.
    Furthermore sincere appreciation to all printing and electronic media journalists for correct and objective cooperation during my spell in Tanzania. Also thank you very much to all sport opponents teams, their players and supporters and my colleagues coaches, to house of football TFF (all officials, national coaches, referees) to all other stakeholders in beautiful game of football and out of football, neutral football lovers and all Tanzanians whose culture, style of life, history and tradition I learned and I was honored and privileged to be part of and I will forever keep inside my heart and remain friend of beautiful country like Tanzania. Is good and passionate people like Tanzanians are and rising star of African football like Tanzanian football.
    sincerely yours coach Micho.

    TAFSIRI:
    (Mpendwa Zubeiry
    Kwa kuheshimu ushirikiano wetu hasa katika kipindi ambacho nilikuwa kocha wa timu ya Yanga.
    Ningependa kuonyesha shukrani zangu kwako binafsi na heshima kubwa kwako kama rafiki yangu kipenzi. Nakutakia kila la heri.
    Ifuatayo ni taarifa yangu kuhusiana na klabu ya Yanga:
    Kupewa nafasi na heshima kubwa ya kuinoa Yanga, ni fursa kubwa si tu kwa Watanzania pekee, bali kwa soka la Afrika pia.
    Nimefanya uchambuzi wa kutosha kuhusiana na suala hili na kutokana na matatizo binafsi siwezi kuendelea kuwa kocha wa Yanga. Kwa heshima na taadhima, nakubaliana na kila kitu na muda wote niliokuwa na Yanga, napenda kutanguliza shukrani zangu kwa wachezaji wa Yanga, benchi la ufundi uongozi chini yake Bw. Kifukwe na baadaye Bw. Madega, namshukuru pia mfadhili Bw. Yusuf Manji na mashabiki wote wa Yanga kwa sapoti kubwa na ushirikiano walioonyesha kwangu kama kocha.
    Shukrani zaidi ziviendee vyombo vya habari, waandishi kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa kwa kipindi chote nilichokuwa nikifanya kazi Tanzania.
    Pia nazishukuru timu zote pinzani, wachezaji wao na mashabiki na makocha wenzangu, maofisa wa TFF na wadau wote kutokana na usimamizi imara wa mchezo huo. Pia shukrani kwa mashabiki wote wa soka na namna zote ambavyo niliweza kuendana na utamaduni, mila na desturi za Watanzania kitu ambacho daima kitabaki moyoni mwangu. Ni busara na hekima kwa Watanzania ambao nyota yao sasa inaanza kung’ara katika medani ya mchezo huo.
    Wako ni mimi kocha Micho).
    Baada ya kuisoma, kwa kweli ilinikera mno, kwa nini ameamua kuondoka wakati alikwishaanza kutengeneza Yanga inayocheza soka ya kueleweka? Tuliiona Yanga ikipiga pasi kibao, ikitengeneza mipango ya maana uwanjani, lakini jinsi ya kuupachika mpira nyavuni ilikuwa tatizo kutokana na ubutu wa washambuliaji wa wakati huo.
    Nilikumbuka mengi niliyowahi kuzungumza na Micho akiwa Yanga, kubwa ni kwamba ikiwa Kifukwe ataondoka madarakani, basi naye hataendelea kufanya kazi kwenye klabu hiyo. Lakini pia, Micho ni kocha mwenye kukubali matokeo, anaposhindwa kuipa timu taji, huwa hapendi kuendelea kuifundisha.
    Nikadhani labda kitendo cha kufungwa na Simba kwenye fainali ya Ligi Ndogo mjini Morogoro bao 1-0 na kukosa ubingwa huo au kutolewa kwa Yanga bila kufika hatua ya makundi ya michuano yoyote ya Afrika vilimkera. Labda.
    Au matatizo yake na TFF na kocha wa timu wa taifa, Marcio Maximo kuhusu wachezaji wa Yanga kukaa muda mrefu na timu hiyo, hali iliyokuwa inamnyima fursa ya kuwa nao muda mrefu kuwaandaa kwa ajili ya mchezo/mashindano. Hakika kuondoka kwake kuliniumiza kichwa, kwani barua yake ilisema ameamua kuacha kazi kwa matatizo yake binafsi.
    Hakika Yanga ilipoteza kocha wa ukweli, ambaye itawachukua muda kumpata.
    Hii Yanga ya sasa chini ya hawa Waserbia watatu, Dusan Kondic, Spaso SokoloVoski na Civojov Serdan pamoja na kuwa na wachezaji wazuri zaidi kulinganisha na wale wakati ule, lakini haifikii hata robo Yanga ya Micho kwa ubora wa kucheza soka. Hii inamaanisha kwamba Micho alikuwa bora zaidi.
    Nimeendelea kuwasiliana na Micho aliyezaliwa miaka 39 iliyopita hata baada ya kuondoka kwake nchini, akinipa habari mbalimbali za mafanikio yake katika klabu yake ya sasa St. George ya Ethiopia, ambako amemchukua kipa wa Yanga, Ivo Mapunda.
    Jumanne ya Mei 27, mwaka jana alinitumia email akinijulisha juu ya mafanikio yake katika msimu uliopita wa Ligi ya Ethiopia.
    Alisema ameiwezesha St. George kutwaa ubingwa wa Ethiopia ikiwa imebakiza mechi nne, haijafungwa hata mchezo mmoja, katika mechi 24 ilizocheza imeshinda 19, imetoka sare tano, ikiwa imefunga mabao 58 wakati wao imefungwa saba tu.
    Klabu yake pia imetoa mfungaji bora, ambaye ni Saladin Said aliyefunga mabao 21 katika mechi 17 alizocheza, wakati yeye ametwaa tuzo ya kocha bora wa Ligi ya nchi hiyo, hiyo ikiwa ni mara ya tatu kwake, kuanzia msimu wa 2004/2005, 2005/2006 na uliopita wa 2007/2008.
    “Ni jambo la kujivunia kwamba hili ni taji langu la tatu naipa timu hii hapa Ethiopia, na mengine matatu niliipa timu Uganda, SC Villa ambayo pia niliipa na ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame 2003), jumlisha na kuifikisha Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Kitu ambacho ni rekodi ya kujivunia kwa kocha mwenye umri wa miaka 38,” alisema Micho.
    Inasikitsha kuona kwamba katika klabu zote alizofundisha, ni Yanga tu hana cha kujivunia na kama alivyosema wakati anaondoka; Nimefanya uchambuzi wa kutosha kuhusiana na suala hili na kutokana na matatizo binafsi siwezi kuendelea kuwa kocha wa Yanga”.
    Hakika ipo haja kwa klabu zetu kujitazama mara mbili. Micho aliingia mkataba ambao unamuwezesha kulipwa vizuri na mfadhili Manji, alipewa kila alichokitaka, lakini mwisho wa siku, aliamua kuondoka.
    Labda alijiuliza; “Hii Yanga siku Manji akiondoka, mimi mustakabali wangu utakuwaje?” Hiyo pia inaweza kuwa changamoto kwa klabu zetu kubwa nchini kujiuliza, ni lini zitakuwa zina uwezo wa kujitegemea kiasi cha kumshawishi yeyote kufanya nao kazi? Yote kwa yote, kwa Micho, Yanga ilipoteza kocha wa maana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MICHO ALIKUWA KIU YA JIBU YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top