• HABARI MPYA

    Saturday, February 21, 2009

    MANJI ATOA FUNGU YANGA KUIUA AHLY

    Manji akiwa na rais wa zamani wa Yanga, Francis Kifukwe


    MFADHILI wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji, ameahidi kuwapa viongozi wa klabu hiyo, fungu la fedha kwa ajili ya maandalizi ya mechi za raundi ya kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Al Ahly ya Misri.
    Manji alimwambia mwandishi mwandamizi wa magazeti haya jana kwamba; “Nilikuwa na viongozi wa Yanga, wamekuja kuniomba fedha kwa ajili ya maandalizi ya Al Ahly, na nitawapa, mimi bado mfadhili wa Yanga,” alisema.
    Wakati Manji akiahidi kuipiga jeki kwenye maandalizi dhidi ya vigogo hao wa Afrika, kocha wa klabu hiyo, Dusan Kondic, amesema kwamba amezidiwa na mawazo juu ya maandalizi ya timu yake kwa ajili ya mchezo huo.
    “Nashindwa kuelewa, sijui itakuwaje, wachezaji kumi sina hapa, wako na timu ya taifa, siyo vibaya, lakini elewa kwenye mashindano yale, Taifa Stars ina nafasi kubwa ya kufika mbali.
    “Mashindano yanakwisha Machi 8, sisi tunatakiwa kucheza mechi ya kwanza Machi 13, hebu fikiri lini watarudi hao wachezaji, ni kuanzia tarehe kumi labda, saa ngapi watashughulikiwa pasipoti zao kutiwa visa.
    “Vyema wote warudi wakiwa fiti, ikiwa wapo watakaokwaa majeruhi, itakuwaje?”alihoji Kondic katika mahojiano na DIMBA, siku moja kabla ya kupanda ndege kwenda Afrika Kusini, anakoishi kwa ajili ya kubadilisha hati yake ya kusafiria.
    Kondic aliyeondoka nchini Alhamisi, alisema kwamba alipanga kuanza mazoezi mapema Jumatatu, lakini ilishindikana kutokana na wachezaji kutofika mazoezini na pia kutowapata kwenye simu.
    “Napiga simu, wengine hawapokei, wengine wamezima kabisa, yaani sijui nitafanya nini, mambo ni magumu,” alisema.
    Kwa sababu hiyo, Kondic alisema mazoezi ya wachezaji pungufu wa kikosi chake, yataanza keshokutwa Jumanne baada ya yeye kurejea kutoka Afrika Kusini.


    Simba SC, Yanga hatarini kutupiwa virago Ligi Kuu

    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeziambia klabu za Simba na Yanga, kwamba zisipoajiri watendaji kwa mujibu wa katiba mpya, zitashushwa daraja msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
    Akizungumza na DIMBA kabla ya kwenda Ivory Coast, Jumatano wiki hii, Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela, alisema kwamba Simba na Yanga zilipewa onyo hilo, katika vikao vya pamoja kati ya TFF na klabu za Ligi Kuu.
    “Katika vikao vyetu na wao, tumewaambia kabisa, kama hadi msimu ujao watakuwa hawajaajiri viongozi hawa, tutawafuta kwenye Ligi Kuu, na wao wanalijua hilo,” alisema Mwakalebela.
    Aidha, Mwakalebela alisema kwamba kwenye vikao hivyo pia wamekuwa wakiwaambia viongozi wa klabu za Ligi Kuu, kwamba kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa ligi hiyo, kila klabu itatakiwa kuwa na Uwanja wake maalumu wa kufanyia mazoezi.
    “Vinginevyo haitashiriki Ligi, hatulazimishi klabu lazima inunue uwanja wake, hapana, tunataka kila klabu iwe na uwanja wake maalumu wa mazoezi, kama ni Shule ya Msingi Uhuru, basi sisi tujue Simba wanafanya mazoezi hapo,” alisema.
    Kiongozi huyo wa kuajiriwa TFF, alisema kwamba heshima kubwa ya shirikisho hilo kwa sasa imetokana na kufanya kazi kwa ufanisi hasa kwa kufuata Katiba na kanuni, hivyo hawatakuwa tayari kuyumbishwa na klabu yoyote.
    “Hatupo kwa ajili ya klabu fulani, eti Simba au Yanga, tupo kwa ajili ya kuongoza mpira wa miguu Tanzania kwa misingi ya Katiba na Kanuni, atakayeshindwa out (nje),”alisisitiza Mwakalebela.
    Baada ya semina ya siku tano Novemba 18, mwaka 2007 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, kuhusu utawala bora na uongozi iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), TFF iliziagiza klabu za Ligi Kuu kutengeneza katiba mpya zitakazokidhi matakwa ya uendeshaji klabu kitaaluma, ikiwemo kuajiri watendaji.
    Hata hivyo, agizo hilo na kuajiri watendaji limeonekana kupuuzwa na klabu nchini, hasa Simba na Yanga, jambo ambalo limeifanya TFF kutilia mkazo kwa staili hiyo.

    Tanzania kuandaa fainali za vijana Mataifa ya Afrika

    na mwandishi wetu
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), lina mpango wa kuomba uenyeji wa fainali za vijana Afrika, chini ya umri wa miaka 20, mwaka 2013, imeelezwa.
    Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela, alisema kwamba Tanzania ilishindwa kushiriki michuano yoyote ya vijana kwa miaka miwili iliyopita kutokana na ukosefu wa fedha, lakini kwa sasa imejipanga vizuri kwa ajili ya kuandaa fainali hizo.
    Alisema sambamba na hilo, kuanzia mwaka huu timu za vijana Tanzania zitashiriki michuano ya Afrika, ikiwemo ile ya chini ya miaka 20 kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika mwaka 2011, zitakazofanyika Libya.
    Mwakalebela alisema kwamba hivi sasa kocha wa vijana, Marcus Tinocco anaendelea vizuri na programu zake za kuandaa vijana kwa ajili ya kushiriki michuano ya Afrika.
    “Ni matarajio yetu safari hii tutashiriki kwa lengo la kufika mbali, kwa sababu kama tumedhamiria kuwa wenyeji wa fainali za 2013, lazima vijana wetu wacheze fainali za 2011 Libya,” alisema.
    Tanzania haijawahi kushiriki fainali zozote za vijana Afrika, ingawa mwaka 2005 ilifuzu kucheza fainali za vijana chini ya miaka 17 nchini Gambia, lakini ikafutwa kutokana na kubainika ilitumia mchezaji mmoja aliyezidi umri, Nurdin Bakari.
    Kwa sababu hiyo, nafasi ya Tanzania ilichukuliwa na Zimbabwe, ambayo pamoja na Zambia na Rwanda zilitolewa na Serengeti Boys katika hatua za kuwania kufuzu.


    Zia Musica yajichimbia Kinyerezi


    BENDI mpya ya muziki wa dansi, Zia Musica International, inatarajia kuingia kambini leo, Kinyerezi mjini Dar es Salaam kujiandaa na uzinduzi wake, utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii.
    Mkurugenzi wa bendi hiyo, Heriswida Lyaunga, alisema kwamba Zia itakuwa kambini kwa siku tano kujinoa kwa ajili ya uzinduzi wake na wa albamu yake ya kwanza, iliyopewa jina, Binadamu yenye nyimbo sita.
    Mkurugenzi huyo alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Mtalaka Wangu, Swida, Hasira Hasara, Jishughulishe, Panda Mti na huo uliobeba jina la albamu.
    Alisema kuwa bendi hiyo ambayo iko chini ya Rais Alfabeti Kabeza, inatarajia kusindikizwa na bendi ya Kalunde katika uzinduzi huo ambao utafanyika Februari 28.
    Herisidwa aliwataja wanamuziki wengine wanaounda bendi iliyoanzishwa mwaka jana na kuweka kambi Sinza kabla ya kuhamia Kinyerezi kuwa ni Mrisho Rajabu, Dokta Kumpeneka na Salum Hamis, ambao wote ni waimbaji wakiwa chini ya Kabeza, Adam Hassan (solo), Linus Mkomela (rythm),Jimmy (besi), Aziz Mohamed (kinanda) na Patrick Klavery (drums).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANJI ATOA FUNGU YANGA KUIUA AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top