• HABARI MPYA

    Tuesday, February 03, 2009

    TENGA: GTV WALIKUWA NA MSAADA MKUBWA KWETU

    RAIS wa Shirikisho la Soka nchini, TFF, ambaye pia anashika cheo kama hicho katika Baraza la Vyama vya Michezo Afrika Mashariki na Kati, CECAFA, Leodegar Tenga, amesema kuondoka ghafla kwa kampuni ya GTV kwenye udhamini ni pigo kubwa.
    GTV (Gateway Broadcast Services) hutoa huduma ya vipindi vya televisheni katika nchi nyingi za Afrika Mashariki kuanzia Kenya hadi Botswana na imekuwa ikidhamini ligi kadhaa za ndani, zikiwamo za Ghana, Tanzania na Uganda.
    GTV pia ni mdhamini wa kombe la CECAFA, maarufu kama Kagame Cup.
    "GTV imewekeza kiasi cha kama paundi 500,000 Uingereza kwa CECAFA kila mwaka na paundi laki sita katika ligi kuu ya Tanzania Bara, kwa hiyo ni hasara kubwa,” Tenga alinukuliwa akiiambia BBC Sport.
    "CECAFA ilikuwa inaangalia wadhamini wengine zaidi, hatukuwa tumewapata hadi sasa, lakini tuna matumaini ya kuwapata,” alisema.
    "Tulidhani tungepata wadhamini wa ziada baada ya GTV, lakini sasa tutalazimika kuanza upya,”
    Mashabiki waliokuwa wakitazama ligi kuu ya England kupitia GTV, wakiwa nyumbani au kwenye kumbi za burudani, walikosa uhondo huo mwishoni mwa wiki.
    "Tunajua usumbufu ambao umetokana na hali hii kwa wateja wetu, wadeni wetu na wafanyakazi,” GTV walisema na kuendelea:
    "Tumejaribu kila njia kuhakikisha kampuni yetu inaendelea kufanya kazi, lakini mwishowe tumejikuta hatuna ujanja, nasi tumekuwa waathirika wa kuporomoka kwa uchumi wa dunia.”
    Msemaji wa ligi kuu ya England, Dan Johnson, aliiambia BBC World Service kwamba wanatumai kumpata mtangazaji wake kwa ajili ya Afrika haraka iwezekanavyo.
    "Tunafanya kila jitihada kuondoa tatizo hili na tuna matumaini kuwa jambo hili litafanikiwa mapema kwa kadiri iwezekanavyo,” alisema Johnson.
    "Ni wazi kwamba wapo watu sokoni ambao wana uwezo huo.”
    Mamia ya mashabiki wa ligi kuu ya England barani Afrika wanakosa matangazo hayo, mashirikisho kadhaa ya soka na mamilioni ya wapenzi wa ligi hiyo wameachwa solemba kutokana na kufilisika huko kwa GTV.
    Kampuni hiyo ilitangaza kufilisika Ijimaa iliyopita, ikidai ni matokeo ya kuyumba kwa uchumi wa dunia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TENGA: GTV WALIKUWA NA MSAADA MKUBWA KWETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top