• HABARI MPYA

    Saturday, February 14, 2009

    CHEKA AMDUNDA TENA RASHID MATUMLA

    Cheka hapa akiwa na Koba Kimanga


    WAHENGA wamesema mengi, yapo yenye kusadikika, lakini mengine, ni vigumu kukubaliana nayo kwa mfano lile neno; Ujuzi hauzeeki.
    Kwa kilichotokea juzi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro katika pambano la ndondi za kulipwa, kati ya Rashid ‘Snake Boy’ Matumla dhidi ya Francis Cheka ‘SMG’, kuwania taji la International Circuit Boxing (ICB) uzito wa Middle, hakika ni vigumu kukubaliana na neno la wahenga, eti ujuzi hauzeeki.
    Kwani bondia bora zamani nchini, aliyeweza kuwabwaga wakali wa aina mbalimbali hadi kuwa bingwa wa dunia aliyeshimika ulimwenguni, alishindwa kufanya vitu vyake vilivyomjengea hadhi kubwa kwenye medani ya mchezo huo.
    Rashid, yule bingwa wa kukwepa na kupiga ngumi kali za kudonoa, mtaalamu wa kucheza kwenye kamba aliyekuwa akiwapiga wapinzani kwa Knockout (KO) mbaya, alishindwa kabisa kurudia makeke yake ya enzi zile.
    Pamoja na mazoezi makali aliyofanya kiasi cha kupungua mno uzito wake kutoka kilogramu 80 hadi 72.2, lakini bado hakuwa Snake Boy yule aliyemshawishi hadi rais wa awamu wa tatu ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, Benjamin Mkapa kumkaribisha Ikulu mwaka 1997.
    Mkapa alimualika Matumla Ikulu, baada ya kutwaa ubingwa wa Afrika wenye hadhi ya kweli ya Afrika, kwa kumtwanga Patrice Mbeh Benle wa Cameroon Machi 30, mwaka kwa Ko raundi ya tano mjini Dar es Salaam.
    Rashid yule aliyekuwa akimvutia hadi rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwenye mapambano yake, Jakaya Kikwete enzi hizo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, si huyu wa sasa anayepigana akiwa na umri wa miaka 40.
    Rashid ambaye alikuwa akimvutia hadi Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tatu, Frederick Sumaye kwenye mapambano yake miaka ya 1990, juzi alijitutumua mbele ya Cheka atakayetimiza miaka 27, Aprili 15, mwaka huu na kumaliza raundi 12 za pambano, akishindwa kwa pointi.
    Kweli kama alivyotamba, safari hii amejiandaa kikamilifu, hilo lilidhihirika ulingoni kwamba alifanya mazeozi ya kutosha, ambayo yalimsaidia tu kuvumilia kipigo cha mpinzani wake ulingoni na si kumuwezesha kushinda.
    Utaalamu wa kukwepa ngumi sasa haupo tena, ujuzi wa kupinga ngumi makini zenye kumlevya hadi kumkalisha chini mpinzani wake, sasa hana Rashid na juzi pamoja na kupigana kwa jitihada zake zote, hakufikia hata nusu ya makali ya enzi zile akiwabwaga wababe mfululizo ndani na nje ya ardhi ya Tanzania.
    Kwa mwenye kumjua Rashid yule, bingwa wa zamani wa dunia, hakika alikuwa ana kila sababu ya kumsikitikia jinsi alivyokuwa akitaabika ulingoni kutafuta namna ya kushinda angalau kwa pointi lake dhidi ya Cheka.
    Ikumbukwe Cheka pia alimpiga mdogo wa Rashid, Hassan kwa KO raundi ya Machi mwaka jana mjini Dar es Salaam.

    PAMBANO LILIVYOKUWA:
    RAUNDI YA KWANZA:
    Cheka aliianza kwa kasi raundi hii, akimtandika ngumi kali za kudonoa mpinzani wake ambazo zilimlewesha ile mbaya na kupepesuka kama anayetaka kuanguka, kabla ya kujitutumua na kusimama imara.
    Kwa ujumla raundi yote hii, Matumla alikuwa kwenye wakati mgumu na alizidiwa mno.

    RAUNDI YA PILI:
    Tofauti na alivyoanza raundi ya kwanza, mikono yake haikuonekana kuchomoka kabisa kuielekeza kwa mpinzani wake, katika raundi hii Matumla angalau alikuwa akijibu ngumi na kupunguza kasi ya Cheka na hapo ndipo matarajio ya watu kwamba angemalizwa kwa KO ya mapema yalipoanza kutoweka.

    RAUNDI YA TATU:
    Mabondia wote walionekana kupigana sawa katika raundi hii, ingawa ngumi za Cheka zilionekana kuwa na madhara zaidi kwa mpinzani wake aliyekuwa ‘sugu’, kwani licha ya kukutana na makombora makali alijitutumua asiende chini na kuishia kupepeuka tu kidogo.

    RAUNDI YA NNE:
    Raundi hii, hakika ilipooza, kasi ya mabondia wote ilikuwa ya chini na Cheka alionekana na kurudi nyuma mara nyingi, ingawa Rashid naye hakuwa na ngumi kali za kuweza kumtetemesha mpinzani wake. Walipigana sawa.

    RAUNDI YA TANO:
    Hii ni raundi ambayo Matumla alionekana kumzidi kidogo Cheka ambaye alikuwa anarudishwa nyuma na ngumi za kudonoa za Snake Boy. Hadi kengele ya kuashiria kumalizika kwa raundi inapigwa, Rashid alikuwa anamsukumia ngumi Cheka.

    RAUNDI YA SITA:
    Naam, kwa mara nyingine ilionekana dhahiri Matumla amemzidi Cheka, kwani pamoja na SMG kuanza kwa kasi, alitulizwa kwa ngumi za kudonoa na kujikuta akihangaika angalau kupenyeza ngumi kwenye paji la uso la mpinzani wake. Lakini kitu kimoja tu, ngumi za Rashid pamoja na kufika kwenye kichwa cha Cheka hazikuonekana kuwa na madhara.

    RAUNDI YA SABA:
    Kwa mara nyingine, Cheka aliibuka na kuanza kumsukumia makonde makali mpinzani wake, ambaye ingawa alijitahidi kujibu, lakini mwisho wa raundi hiyo, ilionekana Matumla alizidiwa.

    RAUNDI YA NANE:
    Raundi hii Cheka alionekana kuanza kuyumba kutokana na ngumi za kudonoa za mpinzani wake, lakini ngumi zake moja moja alizokuwa akichomoa zilionekana kuwa na maana zaidi kwenye raundi hiyo, kwani zilimuingia sawia na kumfikishia maumivu Matumla.

    RAUNDI YA TISA:
    Kwa mara nyingine Snake Boy aliiteka raundi hii akimsukumia makonde mfululizo mpinzani wake, ambaye alionekana kuizungusha mikono yake nyuma ya kiuno cha mwenzake ili kumbana na kupunguza kasi ya kushambuliwa. Ni katika raundi hii, mashabiki wa Cheka waliposikika wakimsihi bondia wao: Cheka nyumbaani hapa, kupigwa aibu. Kweli hiyo ilimpa ujasiri Cheka na kusimama imara.

    RAUNDI YA 10:
    Japokuwa walionekana kujibizana ngumi, lakini konde moja la kudonoa la Cheka alilokutana nalo Matumla, lilionekana kumlevya, ingawa baadaye alijitutumua na kumaliza randi hiyo vizuri.

    RAUNDI YA 11: Rashid alionekana kutawala raundi hii na angalau kwa mara ya kwanza alionekana kumyumbisha hadi kwenye kamba mpinzani wake kutokana na kumlevya kwa ngumi. Hata hivyo, Cheka alisimama imara na kumalizia raundi hiyo vizuri.

    RAUNDI YA 12: Matumla alionekana kutaka kummaliza mpinzani wake katika raundi hii, lakini Cheka alipigana kwa tahadhari zaidi. Rashid alifanikiwa kumrudisha mpinzani wake nyuma muda wote wa raundi hii hadi wakati fulani aliteleza na kuanguka chini. Lakini Cheka alisimama na kuendelea kupigana, japokuwa ukweli ni kwamba katika raundi hii yote SMG alikuwa kwenye wakati mgumu.

    MWISHO WA MPAMBANO:
    Kengele inalia mabondia wote wakiwa hoi bin taaban, wanapeana mikono na kukumbatiana, wote wakihema kama wagonjwa mahututi,
    Rashid akiomba kiti apumzike na Cheka akihaha kuomba maji ya kunywa. Kila upande wa mashabiki ulikuwa kimya, kusubiri mshindi atangazwe.
    Hata hivyo, kutokana na watu kuwa wengi ulingoni, ilikuwa vurugu tupu jambo ambalo liliwafanya wahusika, wazime taa zote ili watu washuke kwanza ulingoni. Lakini watu hawakuondoka na ndipo wahusika wakaamua kutangaza matokeo katika hali hiyo hiyo ya giza.
    Jaji wa kwanza, Omary Yazidu alitoa pointi 118 kwa 117, jaji wa pili Anthony Rutta alitoa pointi 119 kwa 118 na jaji wa tatu, Ally Bakari ‘Champion’, alitoa pointi 119 kwa 115.
    Ni matokeo ambayo kulingana na kile kilichotokea ulingoni, ilikuwa sahihi, Cheka alishinda pambano, igawa safari hii haikuwa kama alivyoshinda kwa kumpiga vibaya mpinzani wake kwenye mapambano mawili yaliyopita, aliyoshinda pia kwa pointi.
    Ikumbukwe juzi mabondia hao walipigana kwa mara ya nne na mbali na Cheka kushinda mara tatu kwa pointi, pambano la kwanza Matumla alishinda kwa KO raundi ya tatu.
    Juanuari 23, mwaka 2003 katika pambano la kwanza baina ya mabondia hao, Rashid ndipo alishinda kwa KO raundi ya tatu, ingawa kwenye pambano la pili, Aprili 25 mwaka 2004 alipigwa kwa pointi (93-100, 95-100 na 93-100) kwenye pambano la raundi 12, ukumbi wa Luxury Pub, Temeke.
    Katika pambano la tatu, Novemba 3, mwaka juzi, Cheka alimpiga vibaya Matumla, kwani Snake Boy alikwenda chini raundi ya tisa ingawa alijitutumua na kupigana kumaliza raundi 12. mwisho wa pambano, jaji wa kwanza Simon Mlundwa alitoa pointi 95-99, wa pili Ally Champion alitoa 96-99 na wa tatu Abdallah Mpemba alitoa 94-99.
    Kwa Cheka hilo lilikuwa pambano lake la 23 tangu alipoanza kucheza ngumi za kulipwa, mwaka 2000 akiwa ameshinda 15, 10 kati ya hayo kwa ameshinda kwa KO, amepigwa mara sita, mara tatu kwa KO na ametoka sare mara moja, wakati Matumla hilo lilikuwa pambano lake la 49, tangu alipoanza kucheza ngumi za kupigana kifua wazi, mwaka 1993.
    Katika mapambano hayo 49, Matumla sasa amepoteza 10, matatu kwa KO, ameshinda 38, kati ya hayo 29 alishinda kwa KO ikiwemo moja dhidi ya Cheka.

    ALIYOSEMA CHEKA BAADA YA PAMBANO:
    “Nimefurahi sana kushinda pamano hilo, nimedhihirisha kama Rashid ni mteja wangu tu, ila kwa kweli leo amenipa wakati mgumu ulingoni, inaonyesha kweli alijiandaa. Rashid ni bondia mzuri, ila kwa sasa naelekeza fikra zangu kwenye pamano langu la Poland, sitaki tena kupigana na bonaia wa Tanzania,”alisema.
    Cheka alisema kwamba pambano lilikuwa gumu na limempa changamoto nzuri, kwani mwezi ujao ana pambano nchini Poland, hivyo mchezo wake wa juzi ulikuwa kama sehemu ya maandalizi yake ya pambano hilo.

    ALIYOSEMA MATUMLA BAADA YA PAMBANO:
    “Naheshimu uamuzi wa majaji, nashukuru kila mtu ananiambia nimepigana vizuri, wengi wamenisihi nisiache ngumi, bali niachane na Cheka. Narudi nyumbani Dar es Salaam, nafikiri baada ya wiki moja nitakuwa na jibu kamili.
    Kwa sababu watu wameniambia kwa mifano mingi sana, nami ninapaswa kutulia kuyafanyia kazi niliyoambiwa, mimi ni bondia mzuri, naondoka Morogoro sina kinyongo na mtu yeyote, na hata kama nitaendelea na mchezo huu, basi sifikirii kama nitapigana tena na huyu mtoto,”alisema juzi usiku baada ya pambano.
    Lakini kwa upande wake, aliyekuwa msaidizi wake ulingoni, Samuel Mhagama ‘King Kiboya’, alilalamikia kitendo cha Cheka kwenda uwanjani mchana siku ya pambano na kupanda ulingoni.
    “Hili lilikuwa pambano kubwa, mabondia wote walitakiwa kupanda ulingoni wakati mmoja tu wa kupigana, sasa wewe sisi tupo kambini, huyu jamaa kaja mchana kafanya mambo yake ulingoni, ndio maana Rashid hata mikono ilikuwa haitoki,”alilalamika Kiboya, yule jamaa anayeonekana kutetemeshwa na kukohoa kwa Ferooz kwenye video ya wimbo Starehe, wakati akizungumza na daktari Profesa Jay.
    Kwa upande wao, Best Man Art Promotions walioandaa pambano hilo, walisema kwamba kutokana na mafanikio yao kwenye mchezo huo uliodhaminiwa na Vodacom na Pepsi, sasa wanajipanga kwa ajili ya kumuandalia pambano lingine kubwa Cheka mjini Morogoro.
    Meneja Mipango wa Best Man, Aristos Nikitas ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Morogoro (MRFA), alisema kwamba watakaa viongozi wa Shirikisho la Masumbwi Tanzania (PST) kujadili nao juu ya mustakabali wa Cheka.



    Kinyogoli atwaa ubingwa
    wa taifa ndondi za kulipwa


    na mahmoud zubeiry, morogoro
    MTOTO wa bondia maarufu wa zamani nchini, Habib Kinyogoli aitwaye Maliki wa Dar es Salaam, juzi jioni alitwaa ubingwa wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (PST) uzito wa Light Welter baada ya kumpiga Deo Njiku wa hapa kwa knockout (KO) raundi ya nne, kwenye pambalola raundi 10, Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
    Kwa ushindi huo, Rais wa PST, Emanuel Mlundwa alisema kwamba atakwenda Philippines kupigana Aprili mwaka huu kupigana katika pambano la ubingwa ambao utatajwa baadaye.
    Katika mapambano mengine, Mbenna Albert alimpiga kwa pointi Maneno Chipolopolo, wote was mjini hapa katika uzito wa Bantam raundi nne.
    Juma Afande wa Morogoro alimpiga kwa KO raundi ya tatu, Jaffar Majia wa Dar es Salaam katika pambano la uzito wa Light, wakati katika uzito wa Light-Fly, Msimbe Mchinya wa Morogoro alimpiga Sadik Abdulaziz wa Dar es Salaam kwa pointi na Fadhil Majia wa Dares Salaam alimpiga alimpiga Epson John wa Morogoro kwa KO raundi ya tatu katikauzito wa Fly.
    Augustino ‘Tino’ Michael wa Morogoro naye aliambulia kipigocha KO raundi ya pili kutoka kwa Hamisi Ajali wa Dar es Salaam.
    Mapambano hayo yaliandaliwa na kampuni ya Best man Art Promotions chini ya Mkurugenzi wake, Zumo Makame na siku hiyo pambano kuu lilikuwa kati ya Francis Cheka dhidi ya Rashid Matumla. Matumla alipigwa kwa mara ya tatu mfululizo na Cheka kwa pointi, katikamara nee walizokutana na ulingoni.
    Pambano la kwanza ndilo alishinda Rashid kwa KO raundi ya tatu mjini Dar es salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHEKA AMDUNDA TENA RASHID MATUMLA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top