• HABARI MPYA

    Thursday, February 26, 2009

    PHIRI AIPIGIA UPATU ZAMBIA

    KOCHA Mkuu wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Patrick Phiri ameipa timu ya soka ya Chipolopolo ya Zambia nafasi ya kushinda mechi ya leo baina yao na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
    Akizungumza na Mtanzania jijini Dar es Salaam jana, Phiri alisema kuwa kiukweli timu hiyo ya Zambia inawazidi kiwango Stars.
    Alisema mchezo wa leo ni mgumu sana kwa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ hasa ukizingatia timu hiyo kuongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne sawa na Senegal ambao waliwafunga Stars bao 1-0 katika mechi ya kwanza.
    “Sijasema kuwa timu yetu ya taifa haichezi vizuri hapana ila kimchezo Zambia iko juu hivyo Stars wanatakiwa kufanya juu chini ili kushinda mechi hiyo muhimu,” alisema Phiri.
    Aidha Phiri aliwataka Watanzania na wadau wote wa michezo nchini kuiomba timu hiyo kucheza vizuri katika mechi hiyo muhimu leo.
    Stars ikishinda mechi ya leo itakuwa imeingia nusu fainali ya michuano hiyo.
    Jumatano usiku Stars ilifanikiwa kuwafunga wenyeji wa mashindano hayo Ivory Coast kwa bao 1-0 hivyo ushindi wa leo utawapa nafasi ya moja kwa moja kuingia fainali.





    MEZA WAJIJIFUA KWA MASHINDANO YA DUNIA

    KAMBI ya timu ya taifa ya mpira wa meza kujiandaa na mashindano ya vijana ya Dunia, inaendelea katika Shule ya Msingi Kisutu, jijini Dares Salaam ambapo wachezaji wamekuwa wakijifua vilivyo.
    Akizungumza na Mtanzania jijini jana, Katibu wa Chama cha Mpira wa Meza Tanzania (TTAA), Isa Mtalaso, alisema kuwa wachezaji wanane wapo kambini tangu wiki iliyopita kujiandaa na mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika Machi 16 hadi 28 jijini Cairo, Misri.
    Aliwataja baadhi ya wachezaji hao kuwa ni Calistus Swelehe, Masoud Isa, Aman Amon, Mwanvita Abdul na Faudhia.
    Aidha Mtalaso alisema kuwa wachezaji wote waliopo kambini wameonyesha shauku ya kufanya mazoezi kwa bidii ili waweze kufanya vyema katika mashindano hayo ya Cairo.
    “Kwa sasa tupo katika mchakato wa kutafuta mfadhili kwa ajili ya maandalizi ya safari yetu hii ya kitaifa ingawa kuna wafadhili mbalimbali wameahidi kutusaidia,” alisema Mtalaso.



    UENYEKITI TGU NJE NJE KWA MALINZI

    MWENYEKITI wa Umoja wa mchezo wa Gofu Tanzania (TGU), Dioniz Malinzi, ni mgombea pekee wa nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa viongozi wa chama hicho unaofanyika leo jijini Dar es Salaam.
    Akizungumza na Mtanzania kutoka Bukoba jana, Kocha Msaidizi wa gofu, Stanley Sanga, alisema kuwa Malinzi ameombwa na wanachama kuendelea kushikilia kiti hicho.
    Alisema kuwa uchaguzi huo utafanyika katika Klabu ya Gofu ya Gymkhana ya Dar es Salaam na kwamba Malinzi hana mpinzani katika kinyang’anyiro hicho.
    “Ni kiongozi aliyeleta mabadiliko makubwa katika mchezo huu tangu kuingia kwake madarakani, hivyo nafikiri hiyo ndiyo sababu kubwa ya kumfanya apendekezwe tena,” alisema Sanga.
    Wakati huo huo, Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Mohammed Kiganja, amesema kuwa usaili wa wagombea hao utafanyika leo asubuhi.
    Alisema wanachama kutoka klabu saba za gofu zilizosajiliwa, watakuwa na mkutano mkuu leo asubuhi na kuwa viongozi wa kuendesha chama hicho, hutoka katika klabu hizo.
    “Wagombea watajulikana leo hii asubuhi na gofu wako tofauti na vyama vingine ambao wagombea hata wasio katika klabu, hugombea nafasi mbalimbali,” alisema Kiganja.
    Alizitaja klabu hizo kuwa ni Gymkhana ya Dar es Salaam, Lugalo, Mufindi, Morogoro, TPC, Arusha na Moshi.


    BOMBESO WANG'ARA BILLZ

    KIKUNDI cha wacheza muziki cha Bombeso, jana kilipagawisha wapenzi wa burudani wakati wa uzinduzi wa kinywaji kipya cha kuongeza nguvu kiitwacho Burn katika Ukumbi wa Club Bilicanas, jijini Dar es Salaam.
    Wasanii wa kikundi hicho kinachoundwa na wachezaji sita, walicheza nyimbo mbalimbali za wasanii wa hapa nchini na hata nje ya Tanzania.
    Kati ya nyimbo walizocheza kwa umahiri mkubwa na kukonga nyoyo za waliohudhuria uzinduzi huo, ni nyimbo za kundi la P Square la Nigeria kama Do Me na nyinginezo.
    Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja Masoko wa Cocacola, Rita Tsehai, alisema kuwa kampuni hiyo imeamua kuongeza bidhaa hiyo ili kukidhi mahitaji ya wateja wao.
    Aidha alisema kuwa kinyaji hicho hakina kilevi na kinaongeza nguvu na kuwafanya wanywaji wake kuchangamka.
    “Idadi kubwa ya vijana wanafurahia vinywaji visivyo na vilevi siku hizi na hii inakwenda sambamba na mabadiliko ya maisha ya kisasa,” alisema Rita.
    Aidha alisema kuwa kinywaji hicho kipya kiko katika ujazo wa milimita 250 kina radha nzuri na hupatikana kwa bei ya Sh 1,500 tu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PHIRI AIPIGIA UPATU ZAMBIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top