• HABARI MPYA

    Thursday, February 26, 2009

    STARS YAIFUNGISHA VIRAGO IVORY COAST

    Ngassa aliyeruka juu akifunga bao katika mechi dhidi ya Sudan, ambayo iliipa Tanzania tiketi ya CHAN

    BAO la kichwa cha mbizi la winga machachari Mrisho Ngassa la dakika 35 lilitosha kuitoa kimasomaso Taifa Stars na kuwalaza wenyeji wa michuano ya CHAN Ivory Coast bao 1-0 katika mchezo wao uliofanyika jana.
    Baada ya kuingia ka bao hilo, Ngassa alianza kushangilia kwa mtindo wa mcheza mieleka maarufu nchini Marekani, John Cena ya 'You can't see me', kabla ya kuungana na wenzake kubembeleza mtoto na kumalizia na staili ya kijoti-joti.
    Bao hilo pia limehitimisha zama za mwisho za wenyeji hao kuendelea na michuano hiyo, huku wakisubiria kukamilisha ratiba kwa kumenyana na Senegal 'Simba wa Teranga.'
    Stars ilionekana kuwa makini katika mchezo huo uliokuwa na kasi muda wote na kuwamiliki wenyeji hao katika idara zote.
    Ngassa alifungwa kwa kichwa baada ya kupokea pasi maridadi kutoka upande wa kulia iliyochongwa na nahodha wa zamani wa Stars, Henry Joseph.
    Kabla ya kutoa krosi hiyo, Henry alipata pande kali kutoka kwa kiungo na nahodha wa mchezo huo, Nizar Khalfan.
    Kwa matokeo hayo, Stars itakuwa imekusanyia pointi tatu na kushika nafasi ya tatu kwenye kundi lake la A huku ikisubiri mchezo wake dhidi ya Zambia keshokutwa.
    Senegal na Zambia 'Chipolopolo', ndizo zinazoongoza kwenye kundi hilo kutokana na kila timu kuwa na pointi nne.
    Katika mchezo wa jana, kocha Marcio Maximo alifanya mabadiliko ya kikosi chake kilichofungwa katika mchezo wa kwanza dhidi ya Senegal Jumapili iliyopita kwa kuwapumzisha Haruna Moshi, Jerry Tegete, Godfrey Bonny.
    Katika hilo, Maximo aliwaanzisha Kigi Makassy, Mussa Hassan 'Mgosi' na Nurdin Bakari.
    Stars ilifanya mabadiliko katika mchezo huo kwa kuwatoa Henry, Ngassa na Mgosi na nafasi zao kujazwa na Shaban Nditi, Tegete na Mwinyi Kazimoto.
    Kikosi kilichoanza Stars; Shaban Dihile, Nsadrack Nsajigwa, Juma Jabu, Nadir Haroub, Salum Swed, Nizar Khalfan, Henry Joseph, Mrisho Ngassa, Kigi Makassy, Nurdin Bakari na Mussa Mgosi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS YAIFUNGISHA VIRAGO IVORY COAST Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top