• HABARI MPYA

    Tuesday, April 28, 2020

    MACHO YA WAPENDA KANDANDA HUPENDA KUTAZAMA SOKA SAFI

    Na Ibrah Mkemia, DAR ES SALAAM
    MOJA ya vitu ambavyo watanzania wengi wameshindwa, ni kufanya utalii hasa ule wa ndani ya nchi. Tanzania ni nchi ambayo imejaaliwa vivutio vingi kama wanyama, milima, misitu, na n.k. lakini imekuwa ngumu kwa watanzania kufanya hivyo.
    Ila kupitia wizara ya maliasiri na utalii wamejaribu kuongeza chachu ya watanzania kupenda kufanya utalii wa ndani kwa kuanzisha kampeni nyingi kuhusu utalii kama kupanda milima, n.k
    Nikapata muamko wa mimi kuanzisha safari kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi, Kilimanjaro kwa kupitia usafiri wa reli kwa maana ya garimoshi (treni). Kiukweli nilifarijika kuona uzuri wa nchi yetu, ukubwa wa maeneo ya wazi yenye miti mirefu na mifupi iliyopambwa na rangi nzuri ya kijani moyoni nikasema "Nakupenda Tanzania".

    Nikiwa kwenye viti ambacho ni maalumu kwa watu wawili,  vyenye kutazamana kwa jumla ya idadi ya watu wanne. Nilipata bahati ya kukaa na watu wa makomo hivi,  japo walikuwa sio wazee sana ila walikuwa na umri mkubwa.
    Wakati safari ikiendelea uku nikiwa nimeelekeza macho yangu nje ya dirisha,  wale wazee ambao nimekaa nao walikuwa wanaendelea na mazungumzo yao, kwa sauti ya chini sana. Nilijaribu kuwekeza masikio yangu kwa karibu lakini nilipata shida kusikia wanazungumza kitu gani. Kimoyo moyo nikasema " ya ngoswe muachie ngoswe".
    Kutokana na ugeni wa safari na ni mara yangu ya kwanza kupanda usafiri huo. Nikajikuta nimepitiwa na usingizi, Mara nikasikia sauti kubwa ya honi ya garimoshi nikafungua macho nikagundua sasa tumeingia korogwe.
    Hapa sasa ndipo nilipokuja kujua kuwa wale wazee mazungumzo yao yalikuwa yanahusu nini. Mmoja wa wazee wale alipaza sauti uku akinyoosha kidole nje ya dirisha. Akimwambia mwenzie "Tazama kile kibao" upesi na mimi nikatupia jicho nikaona kibao ambacho kimeandikwa TTC KOROGWE.
    Yule mzee akamwambia mwenzake umeona? Kabla hajajibu mzee akaendelea kusema "pale ndipo utamu wa soka wa Tanzania na maendeleo ya mpira wa miguu yalipo funuliwa. Na mtaalamu mzawa, Nuru ya Taifa amabaye ni JOEL BENDERA (marhemu)"  jibu likaja kama swali "Alifanya nini?  Mzee akasema nenda kamuulize Leodiger Tenga, Pita Tino, na Mwalimu wa prisons Adolf rishad.
    Wakati safari ikiendelea na mazungumzo ya kumuhusu Joel Bendera tukafanikiw kufika stesheni ya Mombo. Wale wazee wakinitakia safari njema kisha wao wakashuka. Nikakaa kimya kama dakika kadhaa hivi nikatafakari maongezi yao. Kwanini wazee wale watumie muda kumkumbuka marehemu Bendera maswali yakawa mengi sana kichwani. Kubwa likawa TAIFA LINAHITAJI NINI KUKUZA SOKA LETU.
    Nichukue nafasi hii kumuelezea JOEL BENDERA kifupi kwa wasiomfahamu. Nitamuelezea kidogo kwa upande wa soka sababu anastahili heshima kubwa kwa taifa letu tukufu la Tanzania kwa mafanikio yake. Joel Bendera alizaliwa mkoani Tanga wilayani korogwe,  Alianza safari yake ya soka akiwa mwalimu wa pale TTC KOROGWE. Alifundisha timu ndogo ndogo,  Lakani nuru ilikuja kuwaka pale alipokabidhiwa timu ya Taifa na kufundisha kwa mafanikio.
    Tumemaliza kumfahamu kwa ufupi marehemu Bendera, swali linabaki kuwa Taifa litaendelea kuwasubiri akina Joel Bendera kupatikana pasipo julikana  au tutangojea wachipuke kama uyoga pori unapoota mwituni. Soka letu linahitaji utalaamu na kila nafasi ishikwe na muhusika. Nikiwa na maana kuwe na vyuo vya walimu wa mpira na waamuzi,  Na kutengeneza viwanja vingi ili kuwapa nafasi watoto wacheze.
    Tumekuwa tunataka mafanikio mpaka tunavurugana wakati hayo tunayoyataka hatujayandaa. "Tusitake Nusu ya nyama itupe wingi wa finyango chunguni kwa kuweka binzali" ilo haliwezekani tutabadili rangi ya mchuzi tu.
    Sisi ni ndugu wa soka miaka inasonga mbele tuna ufumbuzi gani?,  yanayotakiwa kufanyika tushayajua. Jicho la mpenzi wa soka linatakiwa kuona soka safi lenye vitu vilivyotimia. 
    Viwanja bora, wanasoka mahili (wachezaji), waamuzi wanaotenda haki na walimu wenye ujuzi pamoja na uongozi thabiti wenye kufata miongozo na katiba ya nchi. Pia kupiga vita rushwa.
    Naimani tukijenga misingi imara ya soka letu kuanzia chini kuelekea juu, tutakuwa na nchi yenye idadi kubwa ya wasukuma kabumbu ambao sio wa kubaatisha kama mbegu za mpapai unnuapo barabarani. Nimalize kwa kuwaomba viongozi kusikia nisemacho. Wino wa kalamu ni mweusi na mgumu ni kufutika. 
    Masaa machache kupita nikasikia tena mlio wa honi kubwa ya treni. Kuchungulia dirishani nikaona kilele cha mlima wa Kilimanjaro kwa mbali kikiwa kimerembwa na theluji kwa kwa juu. Nilitoa tabasamu la nguvu kisha nikasema Hodi Hodi Kilimanjaro.

    (Ibrah Mkemia anapatikana kwa barua pepe kalomoibrahim@gmail.com au nambari +255 715 147 449 na +255 692 945 323)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MACHO YA WAPENDA KANDANDA HUPENDA KUTAZAMA SOKA SAFI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top