• HABARI MPYA

    Friday, April 10, 2020

    AMBAVYO SIMBA HAWAKUMUELEWA MO DEWJI KUHUSU UWEKEZAJI WAKE

    Na Abbas Mwalimu, DAR ES SALAAM
    KUMEKUWA na fukuto la sintofahamu juu ya uwekezaji wa mfanyabiashara maarufu na mwekezaji katika klabu ya Simba ndugu Mohammed Dewji maarufu kwa jina la MO.
    Uwekezaji wa MO katika klabu ya Simba unapitia kampuni yake ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited kwa kifupi MeTL.
    Baadhi ya wanachama wa klabu ya Simba wamekuwa wakihoji juu ya kiasi cha Shilingi Bilioni 20 za Kitanzania ambazo MO aliahidi wakati anaingia kuwekeza Simba.
    Niliwahi kuandika makala tarehe yenye kichwa cha kifuatacho tarehe 18 Juni, 2019:

    SIMBA MLIMUELEWA MO KUHUSU PRICE TO EARNINGS RATIO?
    Kwa bahati mbaya inaonekana wanachama, wapenzi na washabiki wa  klabu hiyo hawakumuelewa MO pindi alipogusia ni nini Price to Earning Ratio.
    Ni ukweli ulio wazi kuwa wanachama na mashabiki wa klabu hii kongwe wameingia katika hali ya sintofahamu juu ya bilioni 20 walizoahidiwa kuwekezwa hasa ukizingatia kuwa Simba imejidhatiti kufikia mafanikio kama ya TP Mazembe au Al Ahly.
    Wakati huu ambao ligi inaelekea kuisha na kila dalili zikionesha kuwa Simba itawaiwakilisha Tanzania katika michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao wanachama na washabiki wa klabu hii wameanza kuingiwa na hofu kama klabu yao itaweza kushindana na timu kama Al Ahly, Etoile du Sahel, Esperance n.k kama alivyoeleza MO wakati ule.
    Hoja kubwa ninayotaka wanamichezo tuifahamu hapa ni hii ya Price to Earnings Ratio aliyosema mfanyabiashara maarufu  na mwekezaji kwenye klabu ya Simba Mohammed Dewji almaarufu kama MO wakati akizungumza na waandishi wa habari.
    Kwenye ile clip iliyozagaa mitandaoni wakati ule  ilimuonesha Mo akizungumza na waandishi wa habari kwenye kipande kilichorekodiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya America (VOA Swahili) Mo alisikika akisema maneno yafuatayo, ninayanukuu:
    "Ishu yangu ni 20 Billion brother tusifanye masihara eeh! Unajua 20 billion naweza kununua bank! Acha ngoja nikwambie value of the club. Nenda kafanye valuation hata kwenye balance sheet yao wanaonyesha value ya majengo ni billion 3.8 billion 4. Brother ngoja nikwambie-trademark, unajua kwenye biashara ukitaka kununua biashara kuna kitu ambacho kinaitwa Price to Earnings Ratio ndiyo nini? Ngoja niwape somo kidogo."
    Clip ile iliishia hapo.
    Kutokana na hapo alipoishia Mo kwenye somo Price to Earnings Ratio nami nimeona si vibaya nikapaendeleza ili walau watu tuweze kuelimika.

    PRICE TO EARNINGS RATIO NI NINI?
    Gibson (2008:339) katika kitabu chake "Financial Reporting and Analysis. Using Financial Accounting Information" amefafanua Price to Earnings Ratio kwa kueleza yafuatayo:
    "Price to Earnings Ratio is a ratio that expresses the relationship between the market price of a share of common stock and that stock's current earnings per share."
    Kwa maana nyingine ni kwamba "The price to earnings ratio (P/E) is the ratio  for valuing a company that measures its current share price relative to its per share earnings (EPS).
    Kwa tafsiri ya jumla ni kwamba:
    Price to Earnings Ratio (P/E) ni uhusiano kati ya thamani ya soko ya bidhaa kwa ujumla kwa kulinganisha na mapato ya wakati uliopo ya bidhaa husika kwa hisa.
    Kwa maana nyingine ni kwamba P/E inalenga kutazama ni kiasi gani cha pesa ambacho mwekezaji anaweza kuwekeza katika kampuni ili kupata shilingi moja ya mapato ya ile kampuni kutokana na uwekezaji huo.
    Kanuni hii ya uwiano ilipata umaarufu kutokana na kuelezwa vema na Benjamin Graham ambaye alikuja kuitwa " Baba wa Uwekezaji wenye Tija" yaani 'Father of Value Investing.'
    Benjamin Graham ndiye aliyemjengea ushawishi mkubwa Warren Buffet kuingia katika biashara.
    Price to Earnings Ratio hupimwa kwa kuchukua mapato yote ya jumla ya kampuni kabla ya kutoa gharama nyingine dhidi ya thamani ya bidhaa katika soko kwa wakati huo.
    Mfano wa Price to Earnings Ratio katika hili la Mo kwa Simba lipo hivi:
    Mfano tuseme kwamba club ya Simba imeripoti mapato yake yote ya jumla kwa mwaka 2018/2019 kuwa ni bilioni 2.
    Mapato yote ya jumla kwa lugha ya kingereza huitwa 'basic or diluted earnings per share.'
    Thamani ya bidhaa iliyo katika nyaraka yaani  documented (siyo ya ile mdomoni) ambayo kwa mujibu wa Mo ni bilioni 4.
    Kwa haraka hapo Price to Earnings Ratio itakuwa 2.
    Yaani P/E=Market Value of the Club per share/Basic ama Diluted Earnings per share
    Hivyo utachukua bilioni 4 utagawa kwa mapato ya bilioni 2 iliyopata club.
    Sasa katika hili la MO Simba wajiuulize wameingiza kiasi gani? Thamani ya klabu kwa mujibu wa balance sheet aliyosema Mo ni kiasi gani? 
    Wakati wa mahojiano yale walisikika baadhi ya waandishi wakimuuliza kuhusu 'Thamani ya Brand ya klabu ya Simba' je hiyo thamani ya klabu ilifanyiwa valuation na taasisi kama Price Water Coopers au Delloite kuona kuwa brand ya Simba ina thamani gani na ikawa documented?
    Tufahamu kuwa biashara  ya uwekezaji inatazamwa kwa kitu kilichoelezwa kwenye nyaraka (Documents au Balance sheet) je brand imeelezwa humo?
    Kwa mantiki ya Mo ni kuwa kitu ambacho kimo kwenye balance sheet ni thamani ya majengo na si brand ya klabu.
    Kwa muktadha huo na kwa mujibu wa kanuni ya Price to Earnings Ratio inawezekanaje Mo kuwekeza bilioni 20 katika kampuni yenye thamani ya bilioni 4 na mapato ya bilioni 2?
    Kama wanamichezo, do we see his logic behind his reasoning? Tukumbuke Mo ni mfanyabiashara msomi na hili somo la investment analijua vema sana. Ndiyo maana katika clip anasikika akisema 'Ngoja niwape darasa kidogo.' Huyu ni mtaalamu wa biashara.
    Damodaran. A (2002) katika kitabu chake "Investment Valuation: Tools and Techniques for Determining the Value of Any Asset" anaeleza kuwa, sababu ya wawekezaji kuwekeza ni kwamba wawekezaji hutarajia ukuaji mkubwa wa kampuni huko baadae na kama hawaoni dalili za ukuaji hupata tabu kufikiri kuhusu kuwekeza katika kampuni husika.
    Huenda hili ndilo linalomsumbua Mo kichwani mwake akitafakari kuwekeza bilioni 20.
    Kwa mujibu wa Damodaran (2002) ni kwamba ili Simba imvutie Mo zaidi ni lazima iwe na uwezo wa kushiriki ligi ya mabingwa kila mara na kuchukua kombe hapo mapato yataongezeka na growth (ukuaji) itaonekana.
    Jambo moja ambalo nadhani wanamsimbazi wanapaswa kufahamu ni kuwa katika hili la uwekezaji wa Mo wanazungumzia watu wawili, wa kwanza ni Mohammed Dewji mwenyewe na pili Mohammed Dewji Enterprises Limited (METL). Kibiashara hivi ni vitu viwili tofauti.
    Wale waliosoma Accounts na Business Law nadhani watakuwa  wanakumbuka zile General Accepted Accounting Principles kwa kifupi  GAAP yaani kanuni za kiuhasibu zilizokubalika kwa pamoja. Hizi ni kanuni za kiuhasibu zilizokubalika na taasisi takribani zote za kiuhasibu duniani.
    Kuna kanuni mojawapo katika GAAP inasomeka kama "The Business Entity Concept" ambayo inaeleza kuwa "Mfanyabiashara na biashara ni vitu viwili tofauti"
    Mfanyabiashara ni mwanadamu yeye kisheria huitwa 'natural person' halafu kuna biashara nayo ambayo kisheria hutambulika kama mtu wa kisheria yaani 'legal person' hivyo basi kibiashara kuna mtu anaitwa 'MO' na kuna mtu anaitwa 'METL'
    MO ana mikono, miguu, masikio, mdomo, pua, macho ,ulimi n.k huyu METL ana pesa nyingi sana na rasilimali nyingine kibao lakini hana macho, masikio, mdomo wala pua. Yeye anamtegemea Mo kuona,kunusa,kusikia,kusema n.k.
    Hivyo basi Mo anapotaka pesa ni lazima amuombe METL. Kama kwa METLratio za kuwekeza bilioni 20 zinakataa hawezi kumpa Mo hizo bilioni. Hapa ndipo wengi tunaposhindwa kuelewa.
    Kwa bahati mbaya sana hata mitaani kwetu watu wengi hatuijui kanuni hii.
    Utakua mtu ana duka lake halafu hapo hapo familia ikitaka unga anawapimia bila ya kupatiwa pesa, anashindwa kuelewakuwa kibiashara yeye na hiyo biashara ni vitu viwili tofauti. Anapaswa kununua kama wanavyonunua wengine.
    Sawa Mo ni mfanyabiashara nguli na msomi, anaifahaku kwa kina hii 'Business Entity Concept'. Kwa kuthibitisha  hili tazama ile video clip ambayo alizungumza na waandishi wa habari kwa makini utaona vitu viwili.
    Kwanza utamuona Mo anayesema "Ishu yangu ni 20 billion brother..." halafu tazama kwa mbele kwenye upande wake wa kushoto utaona kitu kimesimamishwa mezani kimeandikwa METL huyu ni mtu wa pili ambaye wengi hatumuoni.
    Kwa ufupi "Price to Earnings Ratio" inagoma. Kanuni ya biashara inagoma kukubaliana na matakwa ya Mo kwa kuzingatia mazingira yaliyopo sasa labda kwa baadae sana jambo ambalo kwa mujibu wa price to earning ratio wanasimba hawalielewi.
    Kwake MO ishu kubwa kwake ni 'thamani ya klabu' "value of the club" ambayo ipo kwenye nyaraka za Simba zilizothaminiwa, kimahesabu (ya darasani) haiwezi kuendana na uwekezaji wa Bilioni 20 kwa sababu haitopanda kufikia bilioni 20 ambayo inatarajiwa kuwekezwa katika kipindi hiki kwa mujibu wa rejea hizo nilizoeleza hapo juu.
    Mdomoni Mo anaweza kuweka mzigo wa bilioni 20 lakini technically amekwaa kigingi kwa sababu kanuni ya value investing ya Benjamin Graham inagoma.
    Si rahisi kuwekeza Bilioni 20 kwa mkupuo kwenye klabu yenye thamani ya Bilioni 4, kikanuni hesabu hazikubali. MO anaongozwa na hesabu si utashi wake hilo watu wanapaswa wafahamu.
    Kwa Yanga lipo la kujifunza hapa.
    (Abbas Mwalimu ni mchambuzi wa masuala ya siasa, Diplomasia na biashara anayepatikana kwa na namba +255 719 258 484. Unaweza pia kumfollow Instagram @AbbasMwalimu | Twitter @AbbasMwalimu | Facebook Abbas Mwalimu)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMBAVYO SIMBA HAWAKUMUELEWA MO DEWJI KUHUSU UWEKEZAJI WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top