• HABARI MPYA

  Monday, July 16, 2018

  YANGA SC YAONDOKA LEO ASUBUHI KUWAFUATA GOR MAHIA KOMBE LA SHIRIKISHO, MECHI JUMATANO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha Yanga SC kinatarajiwa kuondoka mjini Dar es Salaam asubuhi ya leo kwenda Nairobi nchini Kenya kwa ajili yake mechi yake ya Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Gor Mahia Jumatano.
  Hakutakuwa na mchezaji yeyote mpya kati ya waliosajiliwa dirisha dogo Feisal Salum, Jaffar Mohammed, Mrisho Ngassa na Deus Kaseke kwa sababu ambazo hazijajulikana.
  Bahati mbaya zaidi hata mshambuliaji Heritier Makambo kutoka DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye ilielezwa jina lakde lilitumwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) pamoja na Ngassa na Kaseke kwa ya kucheza Kombe la Shirikisho naye hayumo kwa sababu usajili wake umekwamishwa na Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).

  Kelvin Yondan (kulia) na Hassan Kessy (kushoto) wamegoma kusafiri na timu kwenda Kenya hadi wasaini mikataba mipya

  Mbaya zaidi ni kwamba mabeki Hassan Kessy na Kelvin Yondan wamegoma kabisa kusafiri na timu wakishinikiza kwanza wapewe mikataba mipya ndiyo warejee kazini.
  Wachezaji wanaotarajiwa kusafiri na timu ni makipa Mcameroon, Youthe Rostand na Beno Kakolanya, mabeki Juma Abdul, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Mwinyi Haji Mngwali, Pato Ngonyani na Gardiel Michael.
  Viungo ni Said Juma ‘Makapu’, Said Mussa ‘Ronaldo’, Juma Mahadhi, Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita, Ibrahim Ajib, Geofrey Mwashiuya na Emmanuel Martin pamoja na washambuliaji Yohana Oscar Nkomola na Mrundi, Amisi Tambwe.
  Yanga SC inatarajiwa kuteremka uwanjani Jumatano ya Julai 18, mwaka huu mjini Nairobi nchini Kenya kumenyana na wenyeji, Gor Mahia nchini Kenya katika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika, kabla ya timu hizo kurudi Dar es Salaam kwa mchezo wa marudiano Julai 29.
  Na kwa mara ya kwanza Jumatano timu hiyo itaongozwa na kocha wake mpya, Mkongo Mwinyi Zahera aliyesaini mkataba Mei mwaka huu kuchukua nafasi ya Mzambia, George Lwandamina.
  Yanga SC haijashinda mechi hata moja kati ya mbili za awali za Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa 4-0 na USM Alger nchini Algeria Mei 6 na kutoa sare ya 0-0 na Rayon Sports ya Rwanda mjini Dar es Salaam Mei 16.
  Baada ya hapo, Yanga SC itacheza tena nyumbani, Uwanja wa Taifa ikiwakaribisha USM Alger Agosti 19 kabla ya kwenda kukamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na wenyeji, Rayon Sport Agosti 28.
  Timu mbili za juu katika kundi hilo zitaungana na washindi sita wa makundi mengine manne kwa mechi za nyumbani na ugenini za Robo Fainali na zitakazofuzu zitasonga mbele, Nusu Fainali na baadaye Fainali.
  Bingwa wa Kombe la Shirikisho atapata zawadi ya dola za Kimarekani, 1 250, 000, mshindi wa pili dola 432, 000 wakati timu zitakazoshika nafasi za pili kwenye kila kundi zitapata dola 239, 000 kila moja, nafasio ya tatu dola 239, 000 na za nne dola 150, 000.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAONDOKA LEO ASUBUHI KUWAFUATA GOR MAHIA KOMBE LA SHIRIKISHO, MECHI JUMATANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top