• HABARI MPYA

  Sunday, July 15, 2018

  SALAMBA APATA AJALI AKITOKEA MWANZA, GARI YAKE YAGONGWA NYUMA, NAYO YAGONGA GARI KUBWA

  Na Mwandishi Weti, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Adam Salamba amepata ajali ya gari akiwa njiani kurejea mjini Dar es Salaam kutoka kwao Mwanza, lakini bahati nzuri hakuumia.
  Salamba amesema kwamba ajali hiyo imetokea eneo la Vigwaza, Bagamoyo mkoani Pwani baada ya kugongwa kwa nyuma na kusababisha naye agonge gari nyingine kubwa mbele.
  “Nilikuwa natoka Mwanza kuja Dar, nilipofika Vigwaza kulikuwa kuna foleni, nikasimama mara kama dakika mbili nasikia nyuma kishindo gari imegongwa, ikasukumwa mbele ikangonga gari nyingine, cha kushukuru sijaumia, niko salama kabisa air bag zimeniokoa,”amesema Salamba katika ujumbe aliotuma baada ya ajali hiyo.
  Gari ya Adam Salamba kwa nyuma baada ya kugongwa leo eneo la Vigwaza
  Hili ndilo gari lililogonga gari ya Adam Salamba leo Vigwaza
  Gari la Salamba nalo likaenda kugonga gari ingine kwa mbele
  Adam Salamba akiwa na gari lake alilonunua baada tu ya kusajiliwa Simba SC mwezi Mei

  Salamba amejiunga na Simba SC Mei mwaka huu kutoka Lipuli FC ya Iringa ambayo aliichezea kwa nusu msimu tu baada ya kujiunga nayo kutoka Stand United ya Shinyanga.
  Tayari Salamba amekwishaichezea Simba SC katika mashindano mawili, kwanza michuano ya SportPesa Super Cup nchini Kenya na baadaye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
  Lakini Salamba baada ya mwanzo mzuri katika hatua ya makundi Kombe la Kagame aliumia katika mchezo wa Robo Fainali dhidi ya AS Ports ya Djibouti na kukosa mechi mbili zilizozofuta Nusu Fainali dhidi ya JKU Simba ikishinda 1-0 na Fainali dhidi ya Azam FC, Wekundu hao wa Msimbazi wakifungwa 2-1, mechi zote Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SALAMBA APATA AJALI AKITOKEA MWANZA, GARI YAKE YAGONGWA NYUMA, NAYO YAGONGA GARI KUBWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top