• HABARI MPYA

  Friday, July 06, 2018

  BIN KLEB: NITAENDELEA KUISAIDIA YANGA NIKIWA NJE YA UONGOZI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIONGOZI wa zamani wa klabu ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema kwamba ameshindwa kukubali uteuzi wake kwenye Kamati Maalum ya Kusimamia Shughuli mbalimbali za klabu hiyo kwa sasa kwa sababu za kiafya na kubanwa na majukumu yake mengine ya biashara zake.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam, Bin Kleb amesema kwamba pamoja na kujiondoa, lakini ataendelea kutoa michango yake kwenye Kamati hiyo kulingana na nafasi yake.
  “Kwanza niseme ninashukuru kwa wana Yanga kuendelea kuwa na imani na mimi na kuendelea kunipa majukumu, hii inaonyesha ni jinsi gani heshima yangu ni kubwa kwenye klabu,”amesema.
  Lakini Bin Kleb amesema; “Ila ninasikitika kwa mara nyingine sitaweza kuitikia wito wa kuwa kwenye Kamati kwa sababu za kiafya na pia kutingwa na shughuli zangu nyingine za kibiashara. Nimechelewa kutoa taarifa hizi, kwa sababu wakati wa uteuzi sikuwepo nchini”.
  Abdallah Bin Kleb (kulia) ameshindwa kukubali uteuzi wake kwenye Kamati Maalum ya Kusimamia Shughuli za Yanga kwa sababu za kiafya

  Bin Kleb amesema kwamba tayari amewajibu kwa barua Yanga juu ya uamuzi wake huo na amewahakikishia kuendelea kutoa michango na misaada yake kama ambavyo amekuwa akifanya siku zote. “Hata msimu uliomalizika huu nimekuwa nikitoa michango yangu, (Hussein) Nyika ni shahidi, sijawahi kuacha kuisaidia Yanga kwa sababu ninaipenda kutoka moyoni mwangu,”ameongeza. 
  Juni 10, mwaka huu katika Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam, wanachama wa Yanga pia waliunda Kamati ya watu tisa chini ya Rais wa zamani wa klabu, Tarimba Abbas na wanachama wa Yanga Kusimamia Shughuli mbalimbali za klabu hiyo kufuatia kile kinachoonekana kuelemewa kwa uongozi uliopo madarakani sasa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga.
  Mwenyekiti Mteule wa Kamati hiyo ni Tarimba Abbas, Makamu wake, Saidy Meckysadik na Wajumbe wa Kamati hiyo ni Abdallah Bin Kleb, Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Lucas Mashauri, Yusuphed Mhandeni, Hamad Islam, Makaga Yanga, Ridhiwani Kikwete, Majjid Suleiman na Hussein Ndama.
  Hiyo ni kutokana na Yanga SC kuwa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti tangu Mei mwaka jana kufuatia kujiuzulu kwa Mwenyekiti, Manji.
  Lakini idadi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka uongozi wa Manji uliochaguliwa Juni mwaka 2016 imepungua pia baada ya kujizulu kwa Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.  Waliobaki katika Kamati ya Utendaji pamoja na Sanga ni Wajumbe watatu, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala na Hussein Nyika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BIN KLEB: NITAENDELEA KUISAIDIA YANGA NIKIWA NJE YA UONGOZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top