• HABARI MPYA

  Saturday, May 02, 2009

  WAKENYA WOOTE YANGA WAITWA HARAMBEE


  MSHAMBULIAJI wa kutumainiwa wa mabingwa wa soka nchini, Yanga, Mike Barasa, ameitwa tena kujiunga na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, yenye wachezaji 23, itakayoanza mazoezi keshokutwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani jijini Nairobi.
  Katika kikosi hicho kilichotangazwa Alhamisi iliyopita, chini ya kocha raia wa Ujerumani, Antoine Hey, Barasa atakuwa pamoja na mchezaji mkongwe, Ibrahim Shikanda wa Azam FC pia ya jijini Dar es Salaam.
  Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Kenya, alikuwa mmoja kati ya chachu ya ushindi wa kikosi cha Yanga kilichotetea ubingwa wa bara hata kabla ya kumalizika kwa Ligi Kuu msimu uliokwisha majuzi.
  Alinga’ra katika mchezo dhidi ya Simba kwa kuipangua ngome ya ilinzi ya Simba na kutoa pasi maridadi, iliyotumiwa vema na Jerry Tegete kusawazisha bao, wakati mwamuzi akivuta pumzi kumaliza mchezo na kufanya ubao wa matokeo usomeke 2-2 mwishoni mwa mechi hiyo, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
  Mwanzoni Hey alimwacha Barasa katika kikosi chake kilichofungwa 2-1 na Tunisia katika mechi yake ya kwanza ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za mwakani, lakini juhudi zake katika timu ya Yanga zimezaa matunda na sasa amerejeshwa kikosini.
  Harambee Stars inatarajiwa kuanza mazoezi ya kujiandaa na mechi ngumu dhidi ya Nigeria; mchezo utakaofanyika Juni 6, huko Abuja.
  Wachezaji wengine wa Yanga walioingia tena katika timu hiyo ni mfungaji bora wa ligi ya bara, Boniface Ambani, Ben Mwalala na George Owino, ikiwa ni pamoja na Joseph Shikokoti na John Njoroge, ambao kwa sasa wako kwa mkopo wakichezea mabingwa wa Kombe la Kagame, Tusker FC.
  Wachezaji wa Azam FC raia wa Kenya walioitwa kujiunga na Harambee, mbali na Shikanda ni Osborne Monday na Francis Ouma, anayetajwa kuwa na mpango wa kujiunga na timu ya Serie B ya Italia, Parma.
  Hey, ambaye amepania kuifanyia makubwa Kenya, amemwita kikosini kwake mchezaji wa Mathare United, Edgar ‘Fighter’ Ochieng, aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho wakati wa michuano ya Chalenji, Uganda mwanzoni mwa mwaka huu, na kiungo mzoefu, Titus Mulama.
  Kocha huyo, anayehaha kupata ushindi wake wa kwanza akiwa na Harambee Stars, alisema kikosi chake kitaondoka Nairobi Mei 18 kwenda Ujerumani, ambako kitafanya mazoezi kwa wiki mbili kikicheza mechi kadhaa za kirafiki na baadaye kuelekea moja kwa moja jijini Lagos.
  (Pichani ni Barasa akichuana na Hussain Yasser wa Al Ahly mjini Cairo)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAKENYA WOOTE YANGA WAITWA HARAMBEE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top