• HABARI MPYA

    Saturday, May 30, 2009

    VUGUVUGU LA USAJILI LAJA NA MAPYA...




    VX la Boban lazua gumzo
    .Mwenyewe asema: Sina mkataba na Simba


    GARI aina ya Toyota Land Cruiser VX anayotanua nayo takriban kwa wiki nzima hivi sasa mchezaji Haruna Moshi ‘Boban’ imezua gumzo kwa watu wanaomfahamu, wakijiuliza kapewa na nani katika kipindi hiki cha wachezaji kuvuna mamilioni kwa ajili ya usajili?
    Boban, kiungo mshambuliaji halali wa Simba anayewaniwa na klabu za Yanga, African Lyon na Azam FC, amekuwa akitanua na gari hilo lenye rangi ya damu ya mzee mitaa ya Sinza, Dar es Salaam.
    “Amekuwa akija nalo mazoezini (ya timu ya mkoa Tabora) na kuondoka nalo, tukimuuliza anasema gari lake,”alisema rafiki mmoja wa karibu wa Boban.
    Rafiki huyo aliyeomba jina lake lisitajwe gazetini, alisema kwamba Boban aliyekuwa akimiliki Balloon awali, tangu mwanzoni mwa mwaka huu amekuwa kwenye pilika za kutaka kununua gari hilo, ambalo thamani yake si chini ya Milioni 60.
    Boban alipopigiwa simu kuulizwa juu ya gari hilo, alisema: “Jamani haya ni maisha yangu binafsi, mimi ninacheza mpira, mnadhani nacheza bure, napata hela kwa hiyo nikifanya mambo ya maendeleo ni vibaya?”alihoji.
    Wiki iliyopita, Boban alikaririwa na gazeti hili akisema kwamba anaweza kusaini Yanga, iwapo tu atakutanishwa na mfadhili wa klabu hiyo Yussuf Manji na kuzungumza naye wakiwa wawili tu.
    Lakini Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Simba, Mulamu Ng’hambi aliionya Yanga isiingie mtegoni kumsajili Boban, kwani ana mkataba wa miaka mitatu na Simba.
    Kuhusu hilo, Boban alikanusha akisema kwamba hana mkataba na Simba: Mkataba wangu Simba umeisha,”alisema Boban.


    Owino aikoga Yanga; Niacheni nirudi Simba
    .Asema kama hawataki wamuuze Iran



    BEKI wa kimataifa wa Kenya, George Owino amesema kwamba anataka kurejea klabu yake ya zamani, Simba ya Dar es salaam kwani haelewi kinachoendelea kati yake na klabu yake ya sasa, Yanga.
    Akizungumza kwa simu kutoka Nairobi, Kenya, Owino alisema amesikia taarifa kwamba Yanga wanataka kumuacha, hiyo haimtishi lakini anawaasa wasithubutu kumchagulia timu.
    “Wanataka kuniuza Serbia, niende kufanya nini huko, kama hawataki nichezee timu yao, waniache nirudi Simba, au kama hawataki nirudi Simba mimi kuna timu nimepata Iran, waniache niende huko,”alisema Owino.
    Owino alisema kwamba hawezi kuingilia uamuzi wa Yanga kumuacha yeye, kwani hayo ni matakwa yao, lakini haifai klabu hiyo kumchagulia timu ya kuhamia msimu ujao.
    “Wachukue wachezaji wanaowataka, waniache mimi, lakini wasinichagulie timu, kama nitatoka Yanga, napenda nirudi Simba au niende Iran, lakini siyo Serbia,”alisema Owino.
    Owino alijiunga na Yanga msimu uliopita, akitokea Simba aliyoichezea kwa misimu miwili tangu ajiunge nayo kutoka Tusker ya Kenya. Lakini akiwa Yanga, licha ya kuanza vizuri na kuwavutia mashabiki wa timu hiyo, baadaye alijikuta anasota benchi kutokana tuhuma kadhaa.
    Kubwa zaidi, Owino anatuhumiwa kucheza chini ya kiwango chake kwa makusudi ili kuihujumu Yanga na kwa sababu hiyo, klabu hiyo iliamua kumuuza timu nyingine.
    Kocha Dusan Kondic wa Yanga, aliwahi kumuambia mwandishi wa Habari hizi kwamba, atamuuza Owino Serbia.




    Amir Maftah: Mimi na Yanga, Yanga na mimi

    AMIR Mohamed Maftah, kiungo awezaye kucheza kama beki pia, amesema hana mpango wa kuihama Yanga kwani bado ana mkataba nayo na hatababaika kwa ofa yoyote itakayotolewa na timu nyingine.
    Akizungumza na DIMBA mjini Dar es Salaam juzi, Amir alisema kwamba amesikia fununu kwamba naye ana mpango wa kuiacha Yanga, lakini anasikitika kwamba si kweli.
    “Siyo kweli, mimi ninabaki Yanga, bado nina mkataba na Yanga, naomba wapenzi na wanachama wa Yanga, wasiyumbishwe na habari za mimi kuondoka, nasistiza si za kweli,”alisema mpwa huyo wa mshambuliaji wa zamani wa kimataifa Tanzania, Juma Amir Maftah.
    Maftah alisema ni kweli soka ni ajira yake kama ilivyo kwa wachezaji wengine wote, hivyo anaweza kuhamia timu nyingine yoyote wakati wowote akitakiwa, ila kwake angependa afanye hivyo kwa sababu ya msingi.
    “Hii inaweza ikawa fundisho hata kwa wachezaji wenzangu pia, mtu lazima ujifikirie mara mbili kabla ya kuihama timu, siyo tu maslahi, kama unapata nafasi kwenye timu, makocha wanakupenda, klabu inakuthamini, mashabiki wanakuunga mkono na unalipwa vizuri kwa wakati, kwa nini uondoke?”alihoji Maftah.
    Nyota huyo kipenzi cha Profesa Dusan Kondic, kocha wa Yanga alijiunga na Yanga mwaka 2007, akitokea Mtibwa Sugar yan Morogoro, ambayo nayo ilimsajili kutoka AFC ya Arusha.
    Maftah ni mchezaji aliyepikwa katika chuo cha soka cha Rollingston na tangu akiwa hapo aliteuliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, mwaka 2004, Serengeti Boys.
    Nyota huyo ambaye mjini Arusha, alikuwa akiitwa Maradona, akifananishwa na gwiji la zamani la soka duniani, Diego Armando Maradona wa Argentina, ni kati ya wachezaji waliowezesha Serengeti Boys kupata tiketi ya kucheza fainali za Afrika nchini Gambia mwaka 2005.
    Hata hivyo, Serengeti ilipokwa tiketi hiyo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutokana na kudaiwa kumtumia mchezaji aliyezidi umri, Nurdin Bakari. Mwaka 2006, Amir alipandishwa timu ya wakubwa na kuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo hadi Februari mwaka huu, alipotemwa baada ya kutofautiana na kocha Mbrazil, Marcio Maximo.
    Maftah, akiwa na nyota wenzake Haruna Moshi ‘Boban’ na Athumani Iddi ‘Chuji’, walitibuana na Maximo, wakati Stars ilipokuwa kwenye Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) nchini Ivory Coast, Februari mwaka huu na tangu hapo Mbrazil huyo ameamua kuwapa ‘shiti’.

    MICHUANO YA KILI TAIFA CUP…
    Mumbara aiwekea mkwara Temeke

    NAHODHA timu ya mkoa wa Mwanza, Mwanza Heroes katika michuano ya Kili Taifa Cup, Castory Mumbara amesema kwamba wana uhakika wa kuifunga Temeke katika Nusu Fainali ya Kombe hilo.
    “Temeke ni timu ya kawaida, iliwafunga Kilimanjaro 7-2 siyo kwa sababu wao ni wakali sana wala nini, Kilimanjaro walijitakia wenyewe kufungwa, kwa sababu siku moja kabla ya mechi walifanya mazoezi magumu mno, nilijua lazima watafungwa,”alisema Mumbara, anayechezea klabu bingwa Tanzania, Yanga.
    Mumbara mchezaji mrefu mwenye umbo la miraba minne, alisema kwamba wamekuja kwenye Kili Taifa Cup kwa ajili ya kuchukua ubingwa na si kushiriki tu, hivyo hawana hofu hata chembe dhidi ya Temeke.
    Alipoulizwa kuhusu nani kwenye timu yao anaweza kumdhibiti kiungo mwenye kasi, Shamte Ally anayechezea pia Yanga, Mumbara alisema: “Utaona siku hiyo nani atamtuliza Shamte, sisi tupo sawasawa,”alisema.
    Mwanza Heroes imeingia Nusu Fainali ya Kili taifa Cup, baada ya kuifunga Ruvuma ‘Wana Lizombe’ 2-0 wakati Temeke iliitandika Kilimanjaro 7-2, mechi zote zikichezwa Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam.

    Kondic amzawadia Kayuni


    “ANDIKA nawashukuru sana, andika Kondic anasema ahsanteni sana, anashukuru kwa kutambua ubora wake, hii ni heshima kubwa kwake, na anawatakia kila heri katika shughuli zenu,”.
    Naam, hayo yalikuwa maneno ya kocha wa Yanga, Profesa Dusan Kondic alipozungumza na DIMBA juzi, kuhusu kuteuliwa kwake kuwa kocha bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Moja kwa moja salamu hizo, zinakwenda kwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni ambaye Kamati yake ndiyo inahusika na michakato hiyo ya kitaalamu ndani ya shirikisho hilo.
    Kamati ya Kayuni ilimteua Kondic raia wa Serbia anayeishi Afrika Kusini, kuwa kocha bora Tanzania mwaka 2008/2009 baada ya kuiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom, ikiwa haijacheza mechi zake tano za mwisho.
    Kondic ambaye wakati wa utoaji wa tuzo hizo alikuwa nyumbani kwake Afrika Kusini ambako mwanawe alikuwa anaumwa, alisema tuzo hiyo imemjengea heshima kubwa ndani na nje ya nchi, hivyo anaishukuru sana TFF.
    “Hadi napanda ndege kwenda Afrika Kusini, sikuwa na matarajio kabisa kama nitapewa tuzo hii, nilijua tuzo hii ni kwa ajili ya makocha wa hapa hapa, lakini nilipopigiwa simu kuambiwa nimeshinda tuzo hii, nilijiona nami ni sawa na makocha wote wa hapa.
    Nawapongeza TFF kwa hili, hii imenihamasisha kuendelea kufanya kazi Tanzania, hii ni heshima kubwa kwangu, sasa watu wote wanajua mimi ndiye kocha bora hapa.
    Sikuwa peke yangu kocha wa kigeni, walikuwapo wengine kutoka Brazil, Bulgaria na Zambia, lakini leo mimi nasherehekea ubingwa na tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu, ni jambo zuri kwangu,”alisema Kondic.
    Kondic alisema kwa sasa yupo kwenye mchakato wa kuunda kikosi bora cha msimu ujao ili Yanga iendelee kutawala soka ya Tanzania. “Nipo kwenye mchakato, leo (Jumatatu ya juzi) tena nitakuwa nikiwafanyia majaribio wachezaji wapya ninaotaka kuwasajili,”alisema Kondic.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VUGUVUGU LA USAJILI LAJA NA MAPYA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top