• HABARI MPYA

  Tuesday, May 05, 2009

  KONDIC: SITAKI WACHEZAJI WA SIMBA TENA
  KOCHA wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Profesa Dusan Kondic, amesema kwamba hatasajili tena mchezaji kutoka kwa mahasimu wao wa jadi, Simba, kwani amejifunza mengi baada ya msimu uliopita kufanya hivyo.
  Msimu uliopita, Kondic alisajili wachezaji watatu wa Simba, ambao ni kipa Juma Kaseja na viungo wenye uwezo wa kucheza kama mabeki pia, Nurdin Bakari na George Owino, raia wa Kenya.
  Aidha, kauli hiyo inakuja siku moja tu baada ya mshambuliaji wa Simba, Mussa Hassan Mgosi, kukaririwa akisema kwamba yupo tayari kusaini Yanga kwa dau la Sh Milioni 50.
  “Sitasajili tena mchezaji wa Simba, nataka hiyo ijulikane, nitasajili wachezaji wangu mwenyewe, ambao tayari nimeshawaona na wengine nimeshaanza kuwafanyia majaribio, nataka kuleta kitu tofauti msimu ujao,” alisema Kondic katika mahojiano na bongostaz jana mjini Dar es Salaam.
  Alipoulizwa kwa nini ameamua kutosajili tena mchezaji wa Simba, Kondic alisema: “Nimekuwa na wachezaji kutoka Simba msimu huu, nimejifunza mengi, kama mazuri nimeona na mabaya nimeona,” alijibu.
  Mserbia huyo alisema jana alianza kuwafanyia majaribio wachezaji watatu kutoka Cameroon, ambao kati yao kuna kipa mmoja na washambuliaji wawili.
  “Sisajili kwa sababu huyu ametoka Cameroon au ametoka wapi, hapana, nataka kuangalia uwezo mtu kwanza uwanjani, kwa wale ambao nimewaona kwenye mashindano moja kwa moja na kupenda uchezaji wao, hao hakuna haja ya kuwajaribu,” alisema.
  Kondic, anayetimiza miaka miwili Yanga Novemba mwaka huu, akiwa ameipa ubingwa wa Tanzania mara zote mbili, alisema kwamba anatoa kipaumbele kwa wachezaji chipukizi zaidi kwenye kikosi chake cha msimu ujao, kwani anataka kujenga timu ya kudumu.
  “Nataka kuwa na wachezaji ambao watanifanya nitulie nao kwa miaka hata mitano, kama itakuwa hivyo, wachezaji wenye umri mkubwa ukiwa nao wawili au watatu si mbaya, lakini wakiwa wengi ni mbaya,” alisema.
  Kondic alisema kwa sasa anajivunia wachezaji watatu chipukizi aliowapandisha kutoka timu ya vijana, ambao ni Razack Khalfan, Nurdin Msiga na Iddi Mbaga, ambao siku hadi siku wamekuwa wakiongezeka ubora.
  Alisema kuna wachezaji pia wengine watatu kutoka kikosi cha vijana cha Yanga waliomvutia, anaanza kufanya nao mazoezi kuwaandaa kwa ajili ya msimu ujao, wakati tayari alisema amekwishaona wa kuongeza kutoka nje ya nchi ili kuimarisha timu.
  Ingawa hakuwa tayari kutaja atakaowaongeza akidai ni mapema sana, lakini uchunguzi wa bongostaz umegundua nyota hao ni pamoja na mfungaji bora wa Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), Given Sunguluma wa ZANACO, kiungo aliyeng’ara na Zambia kwenye michuano hiyo, Dennis Banda na kipa namba moja wa Zambia, Kaumbwa Davy.
  Aidha, tayari kuna habari kwamba wachezaji 10 wataachwa kwenye timu hiyo kwa sababu mbalimbali, kama viwango kushuka, nidhamu na umri mkubwa.
  Kati ya hao, wengine wataachwa kwa staili ya kuuzwa kwenye klabu nyingine, ili Yanga ifidie gharama zake za kuwasajili.
  Wanaotajwa kutemwa ni beki Abubakar Mtiro na washambuliaji Gaudence Mwaikimba na Maurice Sunguti, wakati wengine saba wataachwa kwa staili ya kuuzwa, ambao ni mabeki Nsajigwa Shadrack, Hamisi Yussuf na viungo George Owino na Vincent Barnabas.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KONDIC: SITAKI WACHEZAJI WA SIMBA TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top