• HABARI MPYA

    Tuesday, May 05, 2009

    MWALALA AWAPASHA AKINA MADEGA, KISASA


    MSHAMBULIAJI Ben Mwalala wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, amesema kwamba anasikitika viongozi wa klabu hiyo hawapendi kuambiwa ukweli na ikitokea hivyo wanadai mchezaji ni mtovu wa nidhamu.
    Akizungumza na bongostaz Jumapili, Mwalala alisema kwamba yeye alikuwa mchezaji wa kwanza kusema kama uongozi wa klabu hiyo unaweka nguvu nyingi kwenye maandalizi ya mechi za Simba na kupuuza michuano ya Afrika, ambayo ndiyo ina manufaa zaidi. “Sisi tulitolewa na timu mbovu kabisa ya Uarabuni mwaka jana, ile Akhdar ya Libya, ilikuwa ya kututoa ile? Yote kwa sababu uongozi wa Yanga huwa hauna kawaida ya kuiandaa timu vizuri kwa ajili ya mechi za kimataifa, na kama hawatabadilika, basi tutaendelea kufanya vibaya,” alisema Mwalala.
    Mwalala alikerwa na kitendo cha Mwenyekiti wa Yanga kumkandia Mkenya mwenzake, Boniphace Ambani, kwa sababu tu aliuambia uongozi ukweli.
    “Ambani alisema kweli, Yanga ilikuwa ina uwezo wa kuitoa Al Ahly kama maandalizi yangekuwa mazuri, lakini baadaye anaonekana mtovu wa nidhamu, hii si sawa. Lazima tuukubali ukweli ili tujifunze, sisi tulikuwa tunaweza kuitoa Ahly kama tungeandaliwa vizuri,” alisema.
    Yanga ilitolewa na Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 4-0, baada ya kufungwa 3-0 Cairo, na baadaye 1-0 mjini Dar es Salaam, katika raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika. Awali, mwaka jana ilitolewa kwa jumla ya mabao 2-1 na Al Akhdar, baada ya kulazimisha sare na Tripoli 1-1 na kuja kufungwa nyumbani 1-0, ilihitaji sare ya 0-0 kusonga mbele.
    Wachezaji wa Yanga wamejikuta wanaumia mno baada ya Ahly kutolewa na Kano Pillars ya Nigeria kwa faida ya bao moja la ugenini. Kano, iliyoanza kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani Nigeria, ilikwenda kulazimisha sare ya 2-2 Cairo na kuwavua ubingwa wa Afrika Al Ahly.
    Sasa mabingwa hao mara sita Afrika watakwenda kujaribu kupoza machungu yao kwenye Kombe la Shirikisho kwa kucheza mechi ya mchujo, kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo.


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWALALA AWAPASHA AKINA MADEGA, KISASA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top