• HABARI MPYA

    Wednesday, July 04, 2018

    DIDA AMEREJEA SIMBA ‘KUMLAZA MACHO’ AISHI MANULA…AKIBWETEKA ITAMGHARIMU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BAADHI ya wapenzi wa Simba SC wanajiuliza kwa nini klabu yao imemsajili kipa mkongwe Deogratius Munishi ‘Dida’ wakati tayari ina makipa wawili wazuri, wazoefu na ambao hawajatumika sana, Aishi Manula na Said Mohammed ‘Nduda’.
    Na wakati huo, kikosini kuna kipa chipukizi Ally Salim aliyepandishwa kutoka timu ya vijana anafanya vizuri na ameonyesha uwezo wake katika mechi mbili za mwanzo za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Dahadaha FC ya Somalia na APR ya Rwanda.
    Aishi ni kipa wa muongo huu aliyeibukia Azam FC mwaka 2012 akipandishwa kutoka akademi ya timu hadi akaenda kuwa chaguo la kwanza na sasa ni kipa namba moja wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

    Deogratius Munishi 'Dida' ni kipa mzoefu nchini anayekwenda kushindania namba na makipa wengine bora Simba SC

    Ndunda aliibuka mwishoni mwa muongo uliopita na baada ya kudakia Maji Maji ya Songea, Yanga SC ya Dar es Salaam na Mtibwa Sugar ya Morogoro huyu ni kipa mzoefu anayeweza kuwa anatosha kumpa changamoto Aishi kwa mtazamo mmoja.
    Na kama una makipa vijana wadogo mfano wa Ally Salim wanaoweza kudaka vizuri hata kwenye mashindano makubwa kama Kombe la Kagame – basi baada ya kuwa na Aishi na Ndunda unaweza kudhani hauhitaji kitu zaidi langoni mwako.
    Lakini kwa sababu Simba SC wanaofanya usajili ni viongozi na si benchi la Ufundi, haikuwa ajabu wiki iliyopita akatambulishwa mlinda mlango mwingine bora nchini na mzoefu zaidi, Dida. 
    Dida aliyezaliwa mwaka 1989 Moshi mkoani Kilimanjaro, baada ya kuibukia Temeke kisoka mwaka 2004 alisajiliwa na Coastal Union ya Tanga ikiwa Ligi Daraja la Kwanza, kabla ya 2005 kujiunga Chuoni ya Ligi Kuu ya Zanzibar na kwa sababu za kimaslahi mwaka 2006 alirejea nyumbani kucheza ndondo tu hadi mwaka 2007 alipojiunga na Manyema FC ya Daraja la Kwanza na kufanikiwa kuipandisha Ligi Kuu.
    Hapo ndipo uwezo wake ulipoivutia Simba na kumsajili Novemba mwaka huo huo, 2007 kwa ajili ya msimu wa 2008-2009 na kukutana na makipa wawili wazoefu, Juma Kaseja na Ali Mustapha ‘Barthez’.
    Akafanikiwa kuanza kudaka mapema Simba baada ya Kaseja kuhamia Yanga mwaka 2009 na Barthez kuwa majeruhi na hiyo ikampa nafasi ya kuitwa pia Taifa Stars mwaka 2009 chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo.
    Kaseja aliporejea Simba kutoka Yanga na kuwa namba moja tena, ndipo Dida aliondoka Simba kwenda kujiunga na timu ya kumpa nafasi ya kudaka kulinda kipaji chake na hapo ndipo alipochezea Azam FC, Mtibwa Sugar na Yanga SC.
    Akiwa Yanga, kuna wakati akakutana tena na wote, Barthez na Kaseja lakini hapo wakawa wanadaka kwa kupokezana hadi Kaseja alipoondoka na mwaka jana wakaondoka kwa pamoja yeye na Ally Mustapha.

    Sasa Aishi Manula atahitaji kuongeza bidii kuhakikisha anaendelea kuwa kipa wa kwanza Simba SC

    Kwake Dida kuwa katika kundi la makipa bora si jambo geni na halimtishi na ndiyo maana amekubali kusaini tena Simba SC ikiwa na ‘Tanzania One’ Aishi Manula na Nduda kipa bora wa mashindano ya COSAFA mwaka jana.
    Dida anarejea nyumbani baada ya msimu mmoja wa kuidakia timu ya Chuo Kikuu cha Pretoria, inayofahamika kama Tuks FC ya Daraja la Kwanza aliyojiunga nayo akitokea Yanga, ambako inaaminika aliondoka kupisha kelele za eti anafungwa mabao rahisi wakati mwingine.
    Na anarejea Simba SC wakati Yanga pia walikuwa wanataka kumrejesha kufuatia msimu mmoja wa kukosa huduma zake na kuona umuhimu wake.
    Simba wanataka huduma bora langoni na kwa sasa imani ipo kwa kipa bora wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo, Aishi Manula, maana yake Dida na Nduda watalazimika kupambana kupata nafasi ya kucheza, ama wasubiri mwenzao aumie, au wangoje mechi zisizo na umuhimu sana kugombea namba na Ally Salim.

    Said Mohammed 'Nduda' anapaswa kuongeza juhudi sasa ili kulinda ajira yake Simba SC

    Faida ya ziada ya usajili wa Dida Simba SC ni kumfanya Aishi asibweteke hata kidogo, akijua fika anapokuwa langoni, jukwaani na benchi kuna makipa wawili bora wa kiwango chake na ambao wanamzidi uzoefu, wakati huo huo Ally Salim anaonyesha uwezo pia.    
    Hivyo usajili wa Dida hata kama haukutokana na ushauri wa kitaalamu wa benchi la Ufundi, lakini unaweza kuwa faida kwa maana sasa anakwenda kumfanya Aishi asibweteke na Ndunda naye aongeze bidii kulinda ajira yake Msimbazi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DIDA AMEREJEA SIMBA ‘KUMLAZA MACHO’ AISHI MANULA…AKIBWETEKA ITAMGHARIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top