• HABARI MPYA

    Monday, December 12, 2016

    SIMBA YACHEZEA KIPONDO KWA MTIBWA

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    MTIBWA Sugar imepata ushindi wa kufungia mwaka dhidi ya Simba SC, baada ya kuichapa mabao 2-1  jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog aliwaanzisha Waghana wote, kipa Daniel Agyei na kiungo James Kotei, lakini wakashindwa kuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo.
    Mtibwa Sugar ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya kwanza tu ya mchezo huo, mfungaji Stahmili Mbonde aliyefumua shuti kali lililompoita kipa mpya kutoka Ghana, Daniel Agyei baada ya kufanikiwa kuwapiga chenga mabeki wa Simba.
    Simba ilicharuka na kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Mtibwa Sugar kutaka kusawaziha, hata hivyo safu ya ulinzi ya Wakata Miwa wa Manungu iliyokuwa ikiongozwa na Salim Mbonde ilisimama imara kuzuia hatari zote
    Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Stahmili Mbonde (kushoto) akikimbilia mpira dhidi ya kiungo wa Simba, Jonas Mkude (kulia) katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Mtibwa Sugar imeshinda 2-1, mabao yake yakifungwa na Mbonde dakika ya kwanza na Jaffar Salum dakika ya 34, wakati la Simba lilifungwa na Mohammed Ibrahim. 
    Kiungo aliye katika majaribio James Kotei (kushoto) akifukuzia mpira
    Kipa Daniel Agyei amefungwa mabao mawili leo katika mechi na Mtibwa Sugar

    Mtibwa Sugar ikafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 34 mfungaji Jaffari Salum aliyewapiga chenga mabeki wa Simba baada ya kupokea pasi nzuri ya Ally Shomary na kumchambua Agyei tena.
    Dakika mbili baadae Simba wakapata bao, dakika ya 36 lililofungwa na kiungo wa zamani wa Mtibwa, Mohamed ‘Mo’ Ibrahim kwa shuti la kushitukiza lililompita kwa urahisi, kipa Said Mohammed aliyekuw amezubaa.
    Kipindi cha pili, Simba iliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Mtibwa, lakini bado wapinzani wao hao waliendelea kuwa makini katika kujilinda. 
    Beki Janvier Besala Bokungu aliikosesha Simba SC bao la kusawazisha dakika ya 88 baada ya kugongesha mwamba wa kulia mkwaju wa penalti kufuatia mshambuliaji Ibrahim Hajib kuangushwa na Nahodha na kiungo Shaaban Nditi.
    Refa Michale Magoli aliwatoa kwa kadi nyekundu viungo Mohammed Ibrahim wa Simba na Mohammed Issa wa Mtibwa Sugar dakika ya 86 baada ya kupigana uwanjani.
    Kwa timu zote mchezo huo ulikuwa wa maandalizi ya mzunguko wa pili Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unaoanza wiki ijayo, Simba wakifungua dimba na Ndanda FC mjini Mtwara na Mtibwa Sugar wakianza na Ruvu Shooting.   
    Kikosi cha Simba kilikuwa; Daniel Agyei, Jenvier Bukungu, Mohammed Hussein, Novaty Lufunga/Abdi Banda dk46, Method Mwanjali, James Kotei/Muzamil dk73, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Jamal Mnyate dk84, Fredrick Blagnoon/Laudit Mavugo dk70, Mussa Ndusha/Ibrahim Hajib dk60 na Mohammed Ibrahim. 
    Mtibwa Sugar: Said Nduda, Ally Shomary, Hassan Timbe, Henry Joseph, Salim Mbonde, Shaban Nditi, Kelvin Friday, Mohamed Banka, Stamili Mbonde, Jafary Salum/Mandawa dk73 na Haruna Chanongo/Vincent Baranabas dk76.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YACHEZEA KIPONDO KWA MTIBWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top