• HABARI MPYA

  Tuesday, December 13, 2016

  MALINZI AWAPONGEZA MABOSI WAPYA TOC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amewapongeza viongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), waliochaguliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
  Katika salamu zake za kuwapongeza viongozi hao, Rais Malinzi amesema huu ni wakati mwafaka wa kujipanga katika kufuzu michuano ya kimataifa tukianzia hii Olimpiki ya mwaka 2020 itakayofanyika Tokyo, Japan.
  Kuonyesha namna TFF ilivyopjipanga kwa ajili ya maandalizi hayo, msimu huu imeendesha Ligi Kuu ya Soka Taifa kwa upande wa wanawake na wavulana wenye umri wa chini ya miaka 23, lengo likiwa ni kupata timu ya kutafuta kufuzu.
  Rais wa TFF, Jamal Malinzi amewapongeza viongozi wa TOC waliochaguliwa mwishoni mwa wiki iliyopita

  Tumewaomba wanafamilia wa mpira wa miguu kupendekeza majina majina ya timu za taifa za wanawake na wavulana wenye umri wa chini ya miaka 23 kabla ya timu hizo hazijaingia kwenye kalenda ya kutafuta timu za kufuzu kwa kushirikiana na TOC.
  Kwa Malengo yote hayo na mengine, TFF inaahidi kushirikiana na TOC na vyama vingine vya michezo kikiwamo cha riadha ambacho pia kimepata viongozi wake hivi karibuni.
  TFF inaamini itapata ushirikiano wa kutosha kutoka timu nzima ya Viongozi wa TOC watakaoongoza kwa miaka minne ijayo, kuanzia sasa hadi kipindi cha Olimpiki ya Tokyo 2020 ambao ni Rais Gulam Rashid aliyepata kura za ndiyo 48 na mbili za hapana na Makamu wa Rais, Henry Tandau aliyepata kura za ndiyo 44, tano zikimkataa na moja ikiharibika.
  Wengine ni Katibu Mkuu, Filbert Bayi aliyetetea kwa kishindo nafasi yake hiyo baada ya kupata kura za ndiyo 49, huku hapana moja huku Katibu Msaidizi Suleiman Mohamed Jabir akichomoza kwa kura 49 huku moja ikimkataa na Mweka Hazina ni Charles Nyange kura za ndiyo 47 huku hapana ni tatu na Mweka Hazina Msaidizi alichaguliwa Juma Khamis Zaidy kura 47, moja ikiharibika na hapana ni mbili.
  Katika uchaguzi huo ulioendeshwa na kufanyika kwa utulivu mkubwa, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uchaguzi, Wakili Lloyd Nchunga, aliwataja walioshinda nafasi tano za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka Bara na kura zao kwenye mabano kuwa ni Irene Mwasanga (50), Noorelain Sharrif (48), Muharam Mchume (39), Amina Lyamaiga (32), na Donath Massawe (30).
  Kwa upande wa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji Zanzibar walishinda ni Kocha wa Timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’, Nasra Juma Mohamed (44), Katibu wa Chama cha Riadha Zanzibar (ZAAA), Suleiman Ame Khamis (42), Mussa Abdulrabi Fadhi (37), Ramadhan Zimbwe Omar (33), na Sheha Mohammed Ali (30).
  Kwa upande wa Wana Olimpiki, Mwanariadha wa kike, Zakia Mrisho alishinda kwa kura 49, Samuel Mwera kura 48 na Fabian Joseph kura 44. Nafasi za juu ambazo zilikuwa na mgombea mmoja mmoja.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MALINZI AWAPONGEZA MABOSI WAPYA TOC Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top