• HABARI MPYA

    Friday, October 31, 2014

    DK NDUMBARO AIBUKA TENA, YEYE NA MALINZI TU

    Na Samira Said, DAR ES SALAAM
    HUKU Dk. Damas Ndumbaro, akiwa amekata rufaa kupinga adhabu ya kifungo cha miaka saba kujihusisha na soka ndani na nje ya nchi iliyotolewa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), amesema ataendelea kufanya kazi zake za kuwawakilisha wadau wa soka watakaohitaji huduma yake ya uwakili.
    Akizungumza leo mjini Dar es Salaam, Ndumbaro alisema kuwa TFF na Kamati zake hazina mamlaka ya kumfungia kufanya kazi za uwakili, isipokuwa Jaji Mkuu wa Tanzania na serikali.
    Dk Ndumbaro akiwaonyesha Waandishi wa Habari hati iliyosainiwa na klabu

    Ndumbaro alisema kuwa anashangaa kuona amehukumiwa na Kamati ya Nidhamu kwa kosa la maadili na kuongeza kwamba kamati hiyo haikupaswa kusikiliza tuhuma zilizokuwa zinamkabili.
    Alisema kuwa adhabu hiyo aliyopewa ni dalili za wazi za 'chuki' dhidi yake kwa sababu yeye alichokizungumza ilikuwa ni maamuzi ya klabu 12 za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ambazo zilikubaliana na kumteua yeye kupitia Kampuni yake ya Uwakili ya Maleta & Ndumbaro ya jijini.
    "Sikuzungumza kwa niaba yangu, nilikuwa na ridhaa ya klabu 12, isipokuwa Stand United na Coastal Union, Kamati hii inatumiwa na Jamal Malinzi, ndio kamati iliyoipa ushindi Stand United kupanda Ligi Kuu," alisema Ndumbaro.
    Wakili huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba alisema kuwa alianza kuonekana ni adui mara baada ya kukataa kushiriki katika ufujaji wa fedha ambapo kwa vipindi vitatu tofauti alikataa kusaini hundi za fedha ambazo TFF iliomba kutoka kwenye Bodi ya Ligi Kuu (TPL).
    Alisema kwamba kwa sasa shirikisho hilo linakabiliwa na ukata baada ya kutumia kiasi cha Dola za Marekani 696,823 bila ya kupata kibali cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambao wamezitoa kwa ajili ya udhamini wake wa timu ya Taifa (Taifa Stars).
    Mbali na matumizi hayo, pia Jamal Malinzi anadaiwa kujilipa binafsi Dola za Marekani 159,140 ndio maana sasa wanaamua kufidia fedha hizo katika gharama nyingine ikiwamo makato ya Sh.1,000 kwa kila tiketi," alisema Ndumbaro.
    Aliongeza kuwa anashangaa kuona TFF inaendelea kukata Sh. 1,000 katika kila tiketi za mashabiki wanaoingia uwanjani kushuhudia mechi za Ligi Kuu Bara na kutaja kiasi kilichokatwa hadi kufikia jana ni Sh. milioni 193.2 zilizotokana na mashabiki 193,257 walioingia viwanjani kushuhudia michezo ya ligi iliyoanza Septemba 20 mwaka huu.
    Alisema pia anashangaa kuona rufaa yake aliyokata tangu Oktoba 21 mwaka huu haijapangiwa siku ya kusikilizwa lakini kikao cha Kamati ya Nidhamu kilichokutana kumjadili kilichukua siku mbili.
    Aliongeza kuwa leo Oktoba 31 mwaka huu siku ya 10 na hakuna dalili za kusikilizwa, tutaendelea kuhesabu,  mambo mengi yako katika rufaa.
    Alisema kwamba yeye hajawahi kutoa siri za shirikisho na kueleza kuwa kanuni za ligi na mikataba inayoingiwa si siri.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DK NDUMBARO AIBUKA TENA, YEYE NA MALINZI TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top