• HABARI MPYA

    Wednesday, October 29, 2014

    SIMBA SC WAKAFANYE TATHMINI YA PILI KUHUSU KIEMBA WATULETEE MAJIBU

    JUNI 9, mwaka huu, Clarence Clyde Seedorf alifukuzwa ukocha wa AC Milan, klabu aliyoichezea kwa mafanikio awali, kutokana na matokeo mabaya.
    Gwiji mwingine wa klabu hiyo, Filippo Inzaghi akapewa mikoba yake ikiwa ni miezi minne tangu aajiriwe, Januari 16, 2014. 
    Wapo makocha waliodumu kwa kipindi kifupi zaidi katika klabu na kufukuzwa kwa matokeo mabaya- kuliko Seerdof na AC Milan.
    Ni jambo la kawaida kwa makocha duniani kote kuondolewa kazini kwa matokeo mabaya bila kujali rekodi zao za nyuma- mfano Luis Andre de Pina Cabral e Villas-Boas, maarufu tu Andres Villas-Boas aliingia Chelsea akiwa mshindi wa Kombe la Ulaya, lakini alifukuzwa miezi tisa baadaye kwa matokeo mabaya.

    Alitua Stamford Bridge akitoka kuiongoza FC Porto ya kwao, Ureno kumaliza msimu wa 2010–11 wa Primeira Liga bila kupoteza mechi, akiipatia mataji manne na kuweka rekodi ya kuwa kocha ‘bwana mdogo’ daima kushinda mataji ya Ulaya.
    Mreno mwenzake, Jose Mourinho aliwahi kusema makocha wanaajiriwa, ili wafukuzwe na imeshuhudiwa makocha wengine nguli, kama Luiz Felipe Scolari wakifukuzwa kazi hata kwenye timu ambazo walisherehekea nazo mafanikio makubwa awali.
    Lakini ni nadra kusikia mchezaji anafukuzwa kwa matokeo mabaya, sana ataondolewa kwenye kikosi cha kwanza na baadaye kuuzwa au kuvunjiwa Mkataba, iwapo hataonyesha kiwango cha kuridhisha.
    Nchini Tanzania, wiki hii klabu ya Simba imewasimamisha wachezaji wake watatu, viungo Shaaban Kisiga ‘Malone’, Amri Kiemba na Haroun Chanongo kwa sababu ya matokeo mabaya.
    Simba SC inawatuhumu wachezaji hao kwa utovu wa nidhamu na kucheza chini ya kiwango, kiasi cha kuigharimu timu ikacheza mechi tano za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara bila kushinda, ikitoa sare zote.
    Simba SC imeweka wazi, baada ya tathmini za kitaalamu ilizofanya imegundua, Kiemba na Chanongo wanacheza chini ya kiwango, tofauti na wanavyokuwa timu ya taifa, Taifa Stars, wakati kesi ya Kisiga anadaiwa kuwabwatukia viongozi.
    Siku moja baada ya kuwarudisha Dar es Salaam wachezaji hao kutoka Mbeya, ambako timu ilicheza mechi yake ya mwisho na kutoa sare ya 1-1 na Prisons, Simba SC pia imempa angalizo kocha wake, Mzambia Patrick Phiri.
    Imemuambia inampa mechi mbili zijazo, dhidi ya Mtibwa Sugar Jumamosi na Ruvu Shooting wiki ijayo, ahakikishe timu inafanya vizuri, vinginevyo atavunjiwa Mkataba.
    Simba SC imesema inafanya hivyo kwa sababu, wakati inamuajiri Phiri Agosti mwaka huu, ilimtekelezea kila alichoomba katika maandalizi, ikiwemo kambi na michezo ya kujipima.
    Hakuna mtu wa soka duniani anaweza kushangaa kocha kufukuzwa baada ya matokeo mabaya katika mechi tano hadi saba- kwa sababu  imekwishatokea sana.
    Lakini kusimamisha wachezaji kwa kucheza chini ya kiwango, zaidi hiyo huwa inatokea Tanzania tu na kwa Simba SC hiyo si mara ya kwanza na wala si wao peke yao wenye desturi hiyo, hata mahasimu wao, Yanga SC na Azam FC wamekwishafanya sana tu.
    Kiungo wa kimataifa wa Ubelgiji, Marouane Fellaini-Bakkioui maarufu tu kama Marouane Fellaini, hakuwa na msimu mzuri wa kwanza (uliopita) Manchester United kutokana na kucheza kwa kiwango cha chini, kiasi cha kuwa nje ya Uwanja kwa muda mrefu.
    Msimu huu ameuanza vizuri na tayari ameanza kuheshimika kutokana na kufanuya vizuri. Chelsea ilimvumilia sana Fernando Jose Torres Sanz tangu imsajili kwa dau la rekodi (Pauni Milioni 50 kutoka Liverpool mwaka 2007) kabla ya msimu huu kumtoa kwa mkopo kwa AC Milan.
    Simba SC wanasema wamefanya tathmini zao wamegundua Kiemba hachezi vizuri kwao kama anavyocheza akiwa Taifa Stars. Basi, imetosha kuwa sababu ya kumsimamisha kipindi hiki timu inatoa sare ya tano mfululizo.
    Si vibaya, Simba SC sasa wakafanye tathmini ya pili ili kujua kwa nini Kiemba anacheza vizuri Taifa Stars- kwa kutazama tofauti ya mifumo, aina ya watu anaocheza nao katika klabu na timu ya taifa, na namna anavyotumika kila upande watuletee majibu tuanzishe mjadala mpya. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAKAFANYE TATHMINI YA PILI KUHUSU KIEMBA WATULETEE MAJIBU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top