• HABARI MPYA

    Monday, October 27, 2014

    MTIBWA SUGAR IMEDHAMIRIA AU BASI TU IMETOKEA?

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    CHINI ya kocha mzalendo, beki na Nahodha wake wa zamani, Mtibwa Sugar imeanza vyema msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, hadi sasa ikiwa kileleni kwa pointi zake 13 za mechi tano.
    Haijapoteza mechi, ikitoa sare moja na Polisi Moro na kushinda mara nne dhidi ya Yanga SC 2-0, Ndanda FC 3-1, Mgambo JKT 1-0 na Mbeya City 2-0.
    Matokeo hayo yametosha kuwafanya mabingwa hao wa 1999 na 2000 wawe juu ya mabingwa watetezi, Azam FC na washindi wa pili wa msimu uliopita, Yanga SC.
    Jumamosi wanaingia kwenye mchezo wa sita Uwanja wa Jamhuri, Morogoro dhidi ya mabingwa wa zamani wa ligi hiyo, Simba SC wakiwa na matumaini ya kendeleza wimbi la ushindi.
    Mtibwa Sugar wakishangilia ushindi wao wa kwanza msimu huu dhidi ya Yanga SC

    Simba SC haijashinda mechi, lakini haijapoteza pia, ikitoa sare zote dhidi ya timu ngumu na dhaifu na Jumamosi itawania ushindi wa kwanza- maana yake hicho ni kipimo kingine kwa Mtibwa.
    Mtibwa ilikuwa moja ya timu tishio muongo uliopita, lakini mambo yakabadilika muongo huu na kuwa timu inayocheza Ligi Kuu ili iendelee kuwepo na si kwa dhamira ya ubingwa au nafasi ya pili.
    Bingwa wa Ligi Kuu hucheza Ligi ya Mabingwa Afrika na mshindi wa pili hucheza Kombe la Shirikisho- na Mtibwa Sugar haijaonyesha kiu ya kucheza michuano yote hiyo kwa miaka iliyopita katika muongo huu.
    Ila matokeo yake ya awali katika msimu huu wa 2014/2015 yanaleta picha tofauti na misimu iliyotangulia, kama Mtibwa imedhamiria kurejesha makali yake.
    Siku zote, Mtibwa imekuwa timu yenye uwezo licha ya kutoshika japo nafasi ya tatu, kwani imeendelea kuvipa tabu vigogo Simba na Yanga na hata Azam FC, lakini imekuwa ikikubali kupoteza kwa urahisi dhidi ya timu nyingine zisizo tishio.
    Hali inaonekana kuwa tofauti msimu huu, hususan baada ya ushindi wa jana wa 2-0 dhidi ya Mbeya City, maana yake Mtibwa Sugar imeingia katika msimu huu wa Ligi Kuu kushindana na si kucheza tu Ligi.
    Hata hivyo, bado ni mapema sana kuamini Mtibwa Sugar imefufua makali yake, angalau baada ya mzunguko wa kwanza, tunaweza kupata picha kamili, kama Wakata Miwa hao wa Manungu wamedhamiria, au inatokea tu wanashinda.     
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTIBWA SUGAR IMEDHAMIRIA AU BASI TU IMETOKEA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top