![]() |
| Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Dk Mwinyihajji Makame akizungumza na BIN ZUBEIRY katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort leo mchana. |
![]() |
| Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi Hindi Hamad Khamis akizungumza na BIN ZUBEIRY katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort leo mchana. |
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Zanzibar, Dk Mwinyihajji Makame amesema kwamba rais wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga anavuruga Muungano katika michezo kwa
kuitenga Zanzibar.
Katika mahojiano maalum na bongostaz.blogspot.com mchana huu
katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort visiwani hapa, Dk Makame amesema kwamba
TFF ya Tenga imekuwa ikichukua maamuzi mengi mazito kuhusu masuala ya soka yenye
kugusa maslahi ya pande zote mbili, bila kuwashirikisha ZFA (Chama cha Soka
Zanzibar).
Dk Makame ametolea mfano muundo wa timu ya taifa, Taifa
Stars kuanzia uteuzi wa kocha na hata suala la udhamini wa timu, Zanzibar huwa
hawashirikishwi jambo ambalo amesema ni baya ni linahatrisha muungano katika
michezo nchini.
Dk Makame amesema kwa
sasa anasikia timu ya taifa inataka kubadilishwa jina kutoka Taifa Stars na
kuwa Kili Stars, jina ambalo linatokana bia ya wadhamini wapya Kampuni ya Bia
Tanzania (TBL) na anakitika maamuzi hayo yanachukuliwa bila Zanzibar
kushirikishwa.
“Siungi mkono suala la Taifa Stars kubadilishwa jina, naomba
Wizara husika zote mbili, zisimamie hilo lisijitokeze,”alisema.
Dk Makame, ambaye pia ni Mlenzi wa timu ya Ikulu SC
amesitikishwa na kitendo cha TFF kutoikumbuka ZFA katika migawo wanayopata
kutoka FIFA.
Aidha, Dk Makame alisema kwamba muundo wa TFF pia unapaswa
kurekebishwa, ili uendane na muundo wa serikali mbili katika nchi hii.
“Kuna serikali ya Muungano na serikali ya mapinduzi, katika
serikali ya mapinduzi tuko wenyewe kwa sababu tunasimamia mambo yetu tu huku,
lakini serikali ya Muungano ipo kwa ajili ya taifa letu zima, inahusisha watu
wa pande zote mbili. Utaona Rais anatoka Bara, lakini Makamu wake anatoka Zanzibar.
Vivyo hivyo, katika muundo wa Baraza la Mawaziri pia,
unahusisha pande zote mbili, lakini ndani ya TFF, Zanzibar haihusishwi kabisa,
hii si sawa na matokeo yake soka ya huku inazidi kudidimia kwa sababu hatunufaiki
hata migawo ya FIFA,”alisema.
“Tunampenda sana Tenga, tangu akiwa mchezaji, Kocha na sasa kiongozi,
rais wa TFF, CECAFA na anaiwakilisha vema nchi yetu kwa kweli, ila lazima
ahakikishe anatenda haki,”alisema.
Aidha, kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Utalii
na Michezo, Bi Hindi Hamad Khamis amelaani vikali pia desturi ya TFF kuitenga
ZFA.
Bi Hindi, ameiambia bongostaz.blogspot.com mchana huu katika
hoteli ya Zanzibar Beach Resort visiwani hapa kwamba anasikia hivi sasa timu ya
taifa inataka kubadilishwa jina na kuwa Kili Stars wakati timu hiyo ni ya
muungano na ZFA hawajashirikishwa.
“Si haki kutoishirikisha ZFA ndani ya TFF, lazima kuwe na
ushirikiano kama tulionao kwenye serikali yetu ya Muungano.
Bi Hindi alipoulizwa kama amefanya jitihada zozote za
kukutana na Wizara inayohusika na Michezo katika serikali ya Jamhuri ya
Muungano, alisema; “Unajua hivi karibuni yamefanyika mabadiliko ya Baraza la
Mawaziri huku kwetu, ila Waziri aliyepita hakika alifanya hivyo na mimi napenda
niwaahidi wapenzi wa michezo Zanzibar na Wazanzibari kwa ujumla, kwamba tutafuatilia,”alisema
Bi Hindi.
Naye Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi jimbo la Raha Leo (CCM),
Nassor Salim Ali ‘Al Jazeera’ amelaani vikali pia kitendo cha TFF
kutoishirikisha ZFA katika masuala ya soka yenye kugusa maslahi ya pande zote
mbili.
Al Jazeera aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa ZFA Wilaya ya Mjini
Magharibi, alisema kwamba naye amesikia juu ya mpango wa timu ya taifa kutaka
kubadilishwa jina na kuwa Kili Stars, lakini anapinga.
“TFF hawawezi kubadilisha jina la timu ya taifa
inayoihusisha na Zanzibar pia, bila kuishirikisha ZFA, hii si sawa na mbaya
zaidi jina lenyewe ni la pombe kitu ambacho kipo tofauti na sisi kimaadili
yetu,”alisema.
Al Jazeera alisema Zanzibar wamekuwa wakijitahidi kulinda
Muungano katika michezo na ndiyo maana kila mwaka katika Kombe la Mapinduzi
hualika timu za Bara.
Lakini amesema anasikitika TFF au Bara kwa ujumla wanaitenga
Zanzibar. “Timu ya taifa ni yetu sote, lakini haiji kucheza huku hata mechi za
kirafiki, wakati sisi tunakuwa wenyeji wa michano mikubwa tu ya CECAFA hapa. Tunakosaje
sifa za kuandaa mechi ya timu ya taifa, japo ya kirafiki?”alihoji Al Jazeera.
Vigogo hawa wanatoa malalamiko hayo, katika wakati mwafaka
kwani ni leo Mkutano Mkuu wa TFF umeanza katika ukumbi wa NSSF Water Front, Dar
es Salaam na unatarajiwa kufungwa kesho.




.png)
0 comments:
Post a Comment