• HABARI MPYA

    Friday, April 27, 2012

    HAIJAWAHI KUTOKEA SARE KAMA HII SIMBA NA YANGA


    Kikosi cha Yanga miaka ya 1990

    HADI sasa Simba na Yanga zilikuwa tayari zimekutana mara 87 katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania na Ligi ya Muungano - na katika mechi hizo, Yanga imeshinda mechi 33, imefungwa 23 na zimetoka sare mara 28.
    Katika sare hizo 28, kuna sare moja tu ambayo iliacha gumzo kubwa baina ya mashabiki wa timu hizo, wengine hadi hawaamini kilichotokea kama kilitokana na matokeo halisi ya uwanjani.
    Mechi hiyo iliyochezwa Novemba 9, mwaka 1996 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, ilimalizika kwa sare ya 4-4, tena Simba ikilazimika kuchomoa dakika ya mwisho kabisa ya mchezo, Yanga wakiamini wamekwishashinda 4-3.
    Nilizungumza na Nahodha wa Yanga katika kikosi hicho, Kenneth Pius Mkapa kuhusu sare hiyo, naye alikuwa ana haya ya kusema: "Ilikuwa sare ya kushangaza, Simba na Yanga kufungana 4-4! Ilikuwa ajabu sana, lakini ninachoweza kusema wakati ule timu zilikuwa nzuri, wachezaji walikuwa wana uwezo.
    Tulikuwa tunashambuliana, timu zilikuwa nzuri, washambuliaji wazuri. Unajua kwenye soka, magoli huwa yanatokana na uhodari wa timu," alisema Mkapa, beki wa kushoto wa Yanga enzi hizo.
    Mbali na Mkapa, pia nilizungumza na kiungo aliyeng'ara mno kwenye mchezo huo, Shaaban Ramadhan akiwa na klabu ya Simba, ambaye alisema kwamba kati ya mechi ambazo hawezi kuzisahau enzi zake akicheza soka ya nguvu, ni hiyo.
    "Mechi hii kwanza ndiyo niliyonipa nafasi ya kuitwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa mara ya kwanza. Kocha wa Taifa Stars wakati huo, Zakaria Kinanda (sasa marehemu) alivutiwa na kiwango changu baada ya mechi hiyo, akaniita timu ya taifa.
    Lakini pia hata kabla sijaingia Simba, nilikuwa sijawahi kusikia Simba na Yanga zikitoka sare ya aina hii, 4-4, haijawahi kutokea. Ni magoli mengi mno. Lakini unajua kipindi kile wachezaji walikuwa wana uwezo sana na wanajituma tofauti sana na siku hizi. Timu zilikuwa zinatumia nafasi, kwa hiyo kosa kidogo tu umeumia. Sisi tulisawazisha dakika ya mwisho kabisa," anasema Shaaban, ambaye baadaye alichezea Yanga kaunzia 1998 hadi 2000 alipokwenda Mauritius kucheza soka ya kulipwa.
    Katika mchezo huo, Thomas Kipese ndiye aliyekata utepe wa kutikisa nyavu, dakika ya saba, kabla ya Edibily Lunyamila kuisawazishia Yanga dakika ya 28 kwa mkwaju wa penalti.
    Ahmed Mwinyimkuu aliifungia Simba bao la pili katika dakika ya 43, kabla ya Mustafa Hozza kuizawadia Yanga bao kwa kujifunga dakika ya 64, akiwa kwenye harakati za kuokoa. Bao hilo, liliamsha hasira za Siimba na kuanza kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Yanga, hatimaye dakika ya 60, Duwa Said aliifungia timu yake hiyo bao la tatu.
    Simba wakiwa wanaamini matokeo yatabaki hivyo hivyo, hata baada ya dakika 90 za mchezo huo, Said Nassor Mwamba akiitwa Kizota kwa jina la utani, aliisawazishia Yanga bao dakika ya 70.
    Sanifu Lazaro, aliyekuwa akijulikana kwa jina la utani 'Tingisha' aliifungia Yanga bao la nne dakika ya 75, ambalo liliamsha shangwe kubwa ya wana Yanga. Lakini uzembe uliofanywa na wachezaji wa Yanga, kuchezea mpira kwenye eneo lao, uliwaponza, kwani Duwa Said aliyekuwa mwiba mchungu kwa Yanga enzi zake, aliisawazishia Simba bao dakika za majeruhi.
    Mechi ilimalizika kwa sare ya 4-4, Yanga ndiyo walikuwa kama wamefungwa, kwani walikuwa wanaamini wamekwishashinda mechi, lakini Simba wakachomoa dakika ya mwisho kabisa. Duwa Said alibebwa juu juu na mashabiki wa Simba baada ya mechi hiyo, kwani kama si jitihada zake, siku hiyo Wekundu wa Msimbazi walikuwa wanalala doro. Naam, hiyo ndiyo sare ya kihistoria ya watani wa jadi, Simba na Yanga. 
    Kikosi cha Simba SC tishio enzi miaka ya 1990

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAIJAWAHI KUTOKEA SARE KAMA HII SIMBA NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top