• HABARI MPYA

    Saturday, April 28, 2012

    HATA MTIBWA IKISHUSHWA DARAJA, SIMBA BINGWA TU NA YANGA MAUMIVU PALE PALE


    Simba SC, mabingwa watarajiwa

    MEI 5, mwaka huu nyasi za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitawaka moto kwa mpambano mkali wa watani wa jadi, Simba na Yanga katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Ingawa mchezo huo unachukuliwa kama wa kukamilisha ratiba tu, kwa kuwa Simba ilikwishajisogeza jirani na ubingwa na Yanga imekwishatoka kwenye matumaini ya kupata hata nafasi ya pili, baadhi wana dhana tofauti- tena inayowadanganya.
    Hiyo inafuatia kuvunjika kwa mechi kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar, Uwanja wa Azam, Chamazi, Mbagala, Dar es Salaam wiki iliyopita, wanadhani mambo yamebadilika.
    Mtibwa ndiyo walikuwa sababu ya kuvunjika mechi hiyo, baada ya kugomea penalti, na matokeo yake Kamati ya Ligi Kuu imewapa ushindi Azam.
    Lakini katika kutoa adhabu, Kamati ya Ligi Kuu imeonyesha mapungufu kulingana na kanuni inavyosema; kwamba timu inayosababisha mechi kuvunjika inashushwa daraja. Wao hawajatoa adhabu kwa ukamilifu kulingana na maelekezo ya kanuni.
    Nini kinachofuata Mtibwa ikishushwa daraja? Matokeo yake yatafutwa, ina maana timu zilizonufaika kwa kubeba pointi nyingi dhidi ya Mtibwa, yenye maskani yake Uwanja wa Manungu, Turiani ambayo tangu ipande Ligi Kuu mwaka 1996, haijawahi kushuka zitaathirika.
    Simba ni timu pekee iliyovuna pointi zote sita kwa Mtibwa, kwanza ikiifunga 1-0 Septemba 25, mwaka jana mjini Morogoro na baadaye 2-1 katika mchezo wa marudiano Machi 18, mwaka huu.
    Azam ilivuna pointi tatu tena za mezani, kwani mechi ya kwanza Oktoba 25, mwaka ilifungwa 1-0 kabla ya mechi ya marudiano iliyovunjika na Yanga ilivuna pointi nne, kutokana sare ya bila kufungana katika mechi ya kwanza Septemba 11, mwaka jana kabla ya kushinda 3-1 katika mchezo wa marudiano Februari 8, mwaka huu.
    Iwapo adhabu ya Mtibwa ingetokana na maelekezo ya kanuni, Azam ingenufaika zaidi- kwa sababu ingekatwa pointi tatu, wakati Simba ingekatwa pointi sita na Yanga pointi nne.
    Kwa sasa Simba ina pointi 59 na ikishinda mechi ya mwisho itatawazwa rasmi kuwa bingwa, kwa kufikisha pointi 62, lakini kama Mtibwa itashushwa daraja, Wekundu wa Msimbazi watamaliza na pointi hizo hizo 59 iwapo wakiifunga Yanga katika mechi ya mwisho.
    Azam wana pointi 53 na wakishinda mechi zao mbili za mwisho dhidi ya Kagera na Toto, watafikisha pointi 59- lakini Mtibwa ikishushwa watamaliza na pointi 56. Ina maana hata kama Simba ikifungwa na Yanga na Mtibwa ikashushwa, bingwa ataamuliwa kwa wastani wa mabao.
    Kama Mtibwa ikishushwa, katika hesabu zake za sasa Yanga itajiongezea pointi moja tu, je wataipiku Azam? Jua la mwakani.
    Nataka niwaambie tu wadau wenye kudhani Mtibwa ikishushwa Top 3 ya Ligi Kuu ya Bara itabadilika, wanajidanganya. Itabaki vile vile.

    MECHI ZA MTIBWA DHIDI
    YA TOP 3 LIGI KUU BARA
    J’tano 07/09/11  Mtibwa    0 – 0    Yanga
    J’nnee 25/10/11 Mtibwa    1 – 0   Azam
    J’pili   25/09/11  Simba      1 – 0   Mtibwa Sugar
    J’tano 08/02/12  Yanga      3 – 1   Mtibwa Sugar
    J’pili   18/03/12  Simba      2 – 1   Mtibwa Sugar
    J’tatu  23/04/12  Azam       1 – 1   Mtibwa Sugar 
    (Mechi ilivunjika, Azam ikapewa pointi tatu)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HATA MTIBWA IKISHUSHWA DARAJA, SIMBA BINGWA TU NA YANGA MAUMIVU PALE PALE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top