![]() |
| Kikosi cha Yanga msimu huu |
NI maajabu tu ambayo sasa yataifanya klabu bingwa Tanzania ipate nafasi ya kucheza
michuano ya Afrika mwakani, baada ya kupoteza pointi tisa mfululizo dhidi ya
Coastal Union, Toto African na Kagera Sugar.
Tayari Yanga imekwishavuliwa ubingwa wa Ligi Kuu, kutokana
na watani wao wa jadi, Simba SC kutimiza pointi 56 ambazo hawawezi kuzifikia.
Nasema maajabu kwa sababu, Yanga inabidi ishinde mechi zake
zote zilizobaki wakati Azam inayohitaji kushinda mechi moja tu, ili kupata
tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho mwakani, ifungwe mechi zote zilizobaki.
Hakuna lisilowezekana chini ya jua, lakini sitaki kusadiki
kama Azam wanaweza kuwa wazembe kiasi hicho na kupoteza nafasi hii adhimu
waliyonayo hivi sasa.
Gumzo kubwa baada ya
matokeo haya mabaya ya Yanga ni uongozi mbovu, uongozi haufai.
Wengi wametoa maoni yao, Mwenyekiti wa Yanga Wakili Lloyd
Baharagu Nchunga ajiuzulu na Kamati yake nzima ya Utendaji.
Wanaamini hilo ndilo suluhisho- lakini ukizama ndani, wengi
wanaotoa maoni hayo wana hasira kutokana na matokeo mabaya na hawataki kujadili
tatizo la msingi la Yanga kukosa nafasi ni nini.
Kwa muda mrefu, binafsi nimekuwa nikililia ligi yenye
ushindani, ambayo naamini ndiyo itakuza soka letu- sasa sioni kwa nini leo
nisifurahi dalili za ushindani zinaanza kulingana na hali halisi ilivyo.
Simba bado haijawa bingwa- bali tu imekwishajihakikishia
kucheza tena michuano ya Afrika mwakani na ili wawe mabingwa, wanatakiwa
kumaliza biashara na si kubweteka.
Matokeo ya mwaka huu, dhahiri yatawafanya vigogo wa soka ya
nchi hii, Simba na Yanga kama kweli wanataka kuendelea kutamba katika ligi
hiyo, wajipange.
Wajipange kwa maana ya kutengeneza timu nzuri, kufanya
maandalizi mazuri na kuwa makini katika uchezaji wa Ligi, kuhakikisha wanakuwa
kwenye nafasi nzuri wakati wote.
Ligi ya aina hii ndiyo ambayo itawafanya wachezaji wetu wawe
na viwango vizuri, hivyo kutusaidia hata kupata timu nzuri ya taifa.
Lakini hiyo ni kama tu matokeo ya uwanjani yanakuwa halisi
na hayatokani na biashara ya kununua mechi- kwa sababu tunakuwa tunajidanganya
eti tuna ligi ya ushindani, wakati ni ligi ya rushwa.
Ligi ya rushwa itabadilisha mabingwa na hata Yanga watakosa
ubingwa, lakini haiwezi kusaidia kukuza soka yetu.
Ni wajibu wa kila mmoja kujitazama mara mbili na kuhakikisha
anachangia maendeleo ya soka katika njia halali, ambazo ndio suluhisho la
kweli.
MAZOEA YANA TABU:
Watu wamezoea ama bingwa Yanga, au Simba au mojawapo ya timu
kushika nafasi ya pili na kwa sababu hiyo, matokeo ya mwaka huu yamekuwa
shubiri.
Hata wakubwa nao sasa vichwa vinawauma, kwa sababu Azam
haiwezi kuvuta malefu ya mashabiki uwanjani hata ikicheza na bingwa wa Afrika.
Hivyo ule mgawo wanaopata kutokana na mechi, utashuka mno.
Hilo lazima wakubwa liwaumize sana tu kwa Yanga kukosa mechi za Afrika mwakani.
Lakini wana Yanga pia, hao ndio walioumia zaidi kutokana na
matokeo haya, kwa sababu ni timu yao wanaipenda na wanapenda ing’are. Iko wapi
sasa?
Kwa sababu hiyo wanaona wa kuwatupia lawama au kuwatoa
kafara na viongozi wao.
Sina uhakika kama hii ni sahihi, lakini napenda niseme
sikatai uongozi wa Yanga una matatizo na unahitaji kujitazama mara mbili kama
kweli unataka kuiletea maendeleo klabu.
Kuna dalili za kutosha sana kwamba uongozi wa Yanga
haujiamini na hauna mipango- zaidi kuna watu ndani ya Kamati ya Utendaji wapo
kwa maslahi yao binafsi tu.
Sitaki kuzama ndani juu ya hilo, kwa sababu si mada yangu
kwa leo- ila nataka kuwaambia wana Yanga huu si wakati mwafaka kunyoosheana
vidole, kwa sababu ligi haijaisha.
Yanga wanahitaji kutulia kumalizia ligi na baada ya hapo
sasa wafanye tathmini ya kina, watafute walikosea wapi na ndipo wachukue hatua.
Hawapaswi kuchukua hatua kwa shinikizo la kupagawa na
matokeo, bali wafanye tathmini ya kina kabisa juu ya kile au yale
yaliyosababisha matokeo haya msimu huu.
Baada ya kuchukua ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki
na Kati Julai mwaka jana, wengi waliamini Yanga itakuwa tishio msimu huu.
Lakini hali imekuwa tofauti, Yanga imekuwa kibonde msimu
huu- kwa nini?
Haya ni mambo ambayo Kamati ya Utendaji ya Yanga wanatakiwa
kujiuliza, tena kwa utulivu wa hali ya juu na si kukurupuka.
Yanga iliuanza msimu na kocha Mganda, Sam Timbe ambaye
aliwapa Kombe la Afrika la Mashariki na Kati na ubingwa wa Ligi Kuu msimu
uliopita, lakini baada ya mechi tatu ikamfukuza na kumrudisha Mseriba Kostadin
Papic.
Haya yalikuwa maamuzi sahihi? Kamati ijiulize. Seif Ahmad
‘Magari’ anasemaje sasa baada ya kumfukuza Timbe, kocha asiyeshaurika na
asiyependwa na wachezaji, lakini aliyeleta mataji na kumleta Papic kocha
anayeshaurika na kupendwa na wachezaji aliyeiporomosha timu hivi sasa?
Napenda nieleweke sana hapa- matatizo ya uongozi katika
sekta za michezo Tanzania hayataisha leo kutokana na mifumo mibovu- lakini bado
hayaingiliani na matokeo mabaya.
Fikra za viongozi wa Simba na Yanga zinaishia kwenye
kusimamia timu kwa ajili ya Ligi Kuu tu na hizo mechi mbili tatu za michuano ya
Afrika- hawana mtazamo wa mbali zaidi ya hapo.
Tusahau kuzifanya timu zao kuwa zenye mihimili madhubuti
kama Tout Puissant Mazembe iliyo midomoni mwetu, lakini hata kufanya vizuri
kwenye Ligi iwe tatizo?
Kushuka kwa nidhamu ya wachezaji sambamba na viwango vyao-
kocha asiyejali aliyethubutu kumchezesha mechi mchezaji mwenye kadi nyekundu-
yote haya yaangaliwe kwa kina.
Kocha ambaye kumbukumbu zinaonyesha aliwahi kumpanga kipa
aliyekuwa majeruhi, Obren Curkovic katika mechi ngumu dhidi ya watani wa jadi Simba,
Yanga ikafungwa 4-3.
Kila napozikumbuka baadhi ya mechi za Simba na Yanga
nilizowahi kuziona- huwa nayakumbuka mabao aliyokuwa akifungwa Obren siku ile-
hasa lile la nne lililofungwa Hillary Echesa kutoka katikati ya Uwanja.
Siwezi kumlaumu Obren, alikuwa majeruhi na hakutaka kucheza
ila kocha asiyejiamini na asiyewaamini wachezaji wake alimlaizmisha kucheza.
Kocha asiyemkubali kiungo aliyetoa krosi ya bao la ushindi
katika fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Rashid Gumbo hakuona
hatari ya kumpanga kipa asiye fiti.
Yanga aliyoiacha Profesa Duisan Savo Kondic ilikuwa kali
mno, lakini alihujumiwa na wenye timu walipomchoka ili aondoke na akaja kocha
anayefanana na rais wa zamani wa Marekani. Yanga kunani sasa?
Namkumbuka Stephen Bengo, eti aliachwa Yanga na Papic- na
Mrisho Ngassa aliuzwa Azam FC kwa sababu klabu, chini ya Mserbia huyo ilikataa
kuboresha mkataba wake.
Arsene Wenger aliamua Fabregas, Nasri waondoke kwa sababu
ana misingi ya kupandisha nyota wengine kutoka kwenye akademi, Yanga wana nini?
Ni mfululizo wa matatizo mengi, ambayo Yanga walijitakia na
haya ndio matunda yake- ila suluhisho si mtu kujiuzulu. Naamini viongozi wa
Yanga wamepata fundisho. Sasa wakae chini, wafanye tathmini na waibuke na sera
na mikakati mipya, ambayo itairudisha Yanga kwenye michuano ya Afrika mwaka
2014 ikiwa timu ya ushindani.
Alamsiki.



.png)
2 comments:
Ni kweli utumbo ni mwingi YANGA. lakini kuna kitu umesahau UTUMBO NI MWINGI SANA KWA BIN ZUBERI. wewe ni utumbo!!! na waaandishi aina yako ndo wameifikisha yanga hapo ilipo!UNAZI unatumia kalamu yako kutetea utumbo wa viongozi. ulijitahidi sana kuichafua kamati ya ligi. ionekane inaionea yanga. wakati ulikua unajua wazi kwamba yanga walikosea kumchezesha kanavaro. Lakini kwa sababu ya njaa, au unazi, au UKANJANJA. uliamua kuivua nguo kamati nzima. ukitoa mifano ya kijinga ili tu yanga warudishiwe point ambazo si halali kwao. Leo bila aibu un arudi na kusema utumbo mwingi yanga. Mimi ninasema waandishi aina yako ndo mnaharibu yanga. acha njaa
Asante sana mdau. Nimepost maoni yako ili na wengine wakupime. Ninashukuru kwa matuso yako, kwangu ni sehemu ya changamoto za kazi. Bin Zubeiry.
Post a Comment