• HABARI MPYA

  Sunday, April 01, 2012

  KOCHA COASTAL ALIA YANGA ILIBEBWA MKWAKWANI

  Julio
  KOCHA wa Coastal Union ya Tanga, Jamhuri Mussa Kihwelo ‘Julio’ amesema kwam ba wapinzani wao Yanga katika mchezo wa jana wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzanika Bara, Uwanja wa Mkwakwani Tanga, walibebwa ndio maana wakashinda 1-0.
  Katika mchezo huo, bao pekee la Yanga lilifungwa dakika ya 85 na Mganda Hamisi Kiiza aliyeunganisha pasi ya Kigi Makasi.
  Mechi hiyo ilitawaliwa na vurugu ambapo wachezaji wa timu zote mbili walionekana kukamiana, hali iliyomlazimu mwamuzi wa mchezo huo kutoa kadi saba za njano, nne kwa Yanga, tatu kwa Coastal Union.
  Akizungumza baada ya mchezo, Kocha wa Coastal Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alilalamikia uamuzi wa mwamuzi wa mchezo ulikuwa wa kuibeba Yanga.
  “Mimi ninavyojua Yanga walibebwa, lakini naamini timu yangu ilicheza vizuri kuwazidi,” alisema.
  Naye kocha wa Yanga Kostadin Papic alisema anachoshukuru, timu yake imepata pointi tatu ambazo kwa upande wao ni muhimu. Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 47.
  Vinara wa ligi hiyo, Simba, nao jana walizidi kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 50 baada ya kuichapa African Lyon mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar
  Katika mechi ya Uwanja wa Taifa, Simba ilitawala vipindi vyote vya mchezo na kama washambuliaji wake wangekuwa makini hasa Emmanuel Okwi, wangeweza kupata mabao zaidi ya hayo waliyoyapata.
  Simba ilianza kuandika bao la kwanza katika dakika ya 29 likifungwa na Salum Machaku baada ya kupiga mpira wa kone uliokwenda moja kwa moja kutikisa nyavu za African Lyon.
  Kona hiyo ilitokana na mpira uliopigwa na Felix Sunzu ambaye nae alipokea pasi murua kutoka kwa Shomari Kapombe.
  Bao la pili lilipatikana katika dakika ya 45, mfungaji akiwa Haruna Moshi ‘Boban’. Alifunga bao hilo baada ya kuunganisha krosi safi ya Machaku kutoka wingi ya kulia.
  Bao hilo lilikuja baada ya Lyon kufanya shambulizi kabla ya kipa wa Simba, Juma Kaseja kudaka shuti hilo ambalo ndilo lilikuwa la kwanza kwa timu hiyo iliyokuwa mwenyeji wa mechi ya jana.
  Katika mechi hiyo, Simba ilimpumzisha Kelvin Yondani katika dakika ya 68 na nafasi yake kuchukuliwa na Victor Costa ambaye almanusura aizawadie bao Lyon baada ya kumrudishia Kaseja pasi fupi na mpira kunaswa na Semmy Kessy lakini alishindwa kutikisa nyavu baada ya mpira wake kutoka nje.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA COASTAL ALIA YANGA ILIBEBWA MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top