• HABARI MPYA

  Saturday, December 17, 2016

  MSUVA APIGA MAWILI, YANGA YAUA 3-0 SHAMBA LA BIBI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA imepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Ruvu jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 36 baada ya kucheza mechi 16 na kuishusha Simba iliyomalizia kileleni mzunguko wa kwanza kwa pointi zake 35. Lakini Simba inaweza kurejea kileleni kesho ikishinda dhidi ya wenyeji, Ndanda FC mjini Mtwara.
  Shujaa wa Yanga leo alikuwa ni winga Simon Happygod Msuva aliyefunga mabao mawili kipindi cha pili baada ya kuseti moja kipindi cha kwanza.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na Heri Sasii aliyesaidiwa na Hellen Mduma na Kassim Mpanga wote wa Dar es Salaam hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.

  Simon Msuva (kushoto) akipongezwa na wenzake Haruna Niyonzima na Deus Kaseke (kulia) baada ya kazi nzuri leo

  Bao hilo lililokuja baada ya muda mrefu wa timu zote kushambuliana kwa zamu, lilifungwa na beki Michael Aidan Pius aliyejifunga dakika ya 38 katika harakati za kuokoa krosi ya Simon Msuva iliyokuwa inafuatiliwa vizuri na winga Deus Kaseke.  
  JKT Ruvu pamoja na kuondoka uwanjani baada ya nusu ya kwanza wakiwa nyuma, lakini walicheza vizuri na kupeleka mashambulizi mawili ya hatari langoni mwa Yanga ambayo yaliokolewa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’.
  Yanga nayo ilicheza vizuri pia, lakini wachezaji wake walishindwa kutengeneza nafasi nzuri za kufunga katika kipindi cha kwanza zaidi ya hiyo waliyotumia kupata bao la kwanza.
  Dakika 10 baada ya kuanza kipindi cha pili, kocha Mzambia wa Yanga, George Lwandamina alimtoa mshambuliaji Amissi Tambwe na kumuingiza kiungo Said Juma ‘Makapu’.
  Mabadiliko hayo yaliifanya Yanga ianze kutawala sehemu ya kiungo na kupika mashambulizi yenye shibe hatimaye kupata mabao mawili zaidi.
  Msuva alifunga bao la pili kwa kichwa dakika ya 57 akimalizia krosi ya Kaseke baada ya kazi nzuri ya kiungo mwenzake Haruna Niyonzima. Msuva tena akafunga bao la tatu dakika ya 90 akimalizia pasi ya Niyonzima dakika ya 90.
  Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm alikuwepo jukwaa kuu kufuatilia mchezo, wakati kiungo mpya kutoka Zambia, Justin Zulu alikuwa jukwaani kwa sababu bado hajapatiwa kibali cha kufanya kazi nchini. 
  Baada ya mchezo, kocha Lwandamina alisema timu haijaanza kucheza kwa kiwango chake kwa kuwa bao anajaribu wachezaji.
  Matokeo ya mechi nyingine za Ligi Kuu leo; Mzima. Mwadui imeilaza 1-0 Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Mbeya City imelazimishwa sare ya 0-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Ruvu Shooting imetoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.
  Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Haruna Niyonzima, Mwinyi Hajji Mngwali, Kelvin Yondan, Vincent Bossou, Simon Msuva, Thabani Kamusoko/Geoffrey Mwashiuya dk84, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Said Juma ‘Makapu’ dk55na Deus Kaseke/Obrey Chirwa dk90.
  JKT Ruvu: Hamisi Seif, Michael Aidan, Edward Charles, Yussuf Chuma, Kelvin Nashon/Naftal Nasho dk66, Rahim Juma, Ally Bilal/Mussa Juma dk77, Hassan Dilunga, Najim Magulu, Atupele Green/Saad Kipanga dk77 na Edward Joseph.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MSUVA APIGA MAWILI, YANGA YAUA 3-0 SHAMBA LA BIBI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top