• HABARI MPYA

    Sunday, January 25, 2015

    PEPONI TUTAKWENDA, LAKINI BAADA YA KIFO

    SOKA ya Tanzania imekwishapewa majina mengi ya kifedhuli, kubwa ambalo nalikumbuka ni lile lililotolewa na Rais wa awamu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
    Mzee Mwinyi, kati ya viongozi wenye busara za hali ya juu kuwahi kutokea Tanzania, alisema; “Soka ya Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu, kila mtu anajifunzia kunyoa”.
    Mzee Mwinyi alisema hayo, baada ya klabu ya Simba kufungwa na Stella Abidjan mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993.
    Na ninakumbuka aliwahi kurudia kusema hivyo; “Soka ya Tanzania bado kichwa cha mwendawaimu,”, baada ya kushuhudia matokeo mengine mabaya.

    Lakini wengi wengine kati ya viongozi wetu na wataalamu mbalimbali, tukiwemo Waandishi wa Habari, tumekwishaibeza sana soka yetu.
    Waswahili wana msemo wao; “kibaya chako, kizuri cha mwenzako”. Mimi ni Mtanzania kama Watanzania wengine, basi sote ni waswahili- na kama ni hivyo basi, tuupokee msemo huu, kibaya chetu, kizuri cha wenzetu.
    Tutampenda, kumsifia hata kuvaa jezi zake Yaya Toure, Mwanasoka Bora Afrika raia wa Ivory Coast anayechezea Manchester City ya England, lakini hawezi kuwa Mtanzania. Mtanzania mwenzetu atabaki kuwa Mbwana Samatta wa TP Mazembe ya DRC, ama Mrisho Ngassa wa Yanga, John Bocco wa Azam, Rashid Mandawa wa Kagera Sugar na Elias Maguri wa Simba SC.
    Hii maana yake, tuna wajibu zaidi wa kuhangaikia soka yetu. Tuna wajibu wa kuunganisha nguvu zetu katika mapambano ya kuinua soka yetu.
    Kabla ya mwaka 2006, Ivory Coast na Ghana hakuna kati yao aliyewahi kucheza Fainali za Kombe la Dunia na hazikuwa nchi zenye kuheshimika sana katika ulimwengu wa soka, ingawa zilifanikiwa kutoa wachezaji waliowika hadi Ulaya, kama Abedi Pele aliyewahi hadi kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika.
    Lakini baada ya kucheza Fainali za kwanza za Kombe la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani, zote Ghana na Ivory Coast zimekuwa washiriki wa kudumu wa michuano iliyofuata, 2010 Afrika Kusini na 2014 Brazil.
    Na kwa sasa bado Ghana na Ivory Coast ni timu zenye msingi mzuri wa kuendelea kutamba katika soka ya kimataifa.
    Ghana ilikaribia kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kufika Nusu Fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2010, kama si Luis Suarez kuudaka mpira uliokuwa unaelekea nyavuni kuipa Black Stars bao la ushindi dhidi ya Uruguay katika Robo Fainali.
    Hakuna kisichowezekana kama kunakuwa na dhamira ya kweli, mipango thabiti, utekelezaji makini na uvumilivu- namaanisha, soka ya Tanzania haijafeli, bali bado haijawa na mvuto.
    Hakuna anayeweza kuifanya iwe na mvuto zaidi ya sisi wenyewe tunaojiita wadau wa mchezo huu. Lazima ufike wakati tuache, unafiki, chuki za kike, fitina, uzandiki, kuendekeza njaa, tamaa,  usaliti na majungu- halafu tuunganishe nguvu zetu kuisaidia soka yetu.
    Mama zangu, dada zangu naomba mniwie radhi kutumia neno chuki za kike, najaribu kuelezea namna ambavyo mwanamke ‘alivyojaaliwa’ uwezo wa kupenda na kuenzi, lakini pia kuchukia vibaya moyo wake unapochafuka.
    Miaka nenda rudi, wamepita viongozi tofauti kuanzia wa klabu hadi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), tangu enzi za FAT, soka yetu haijfanikiwa kujitutumua.
    Tatizo kubwa ni kwamba, Watanzania wa leo hatuna umoja, uzalendo wala mapenzi ya dhati na nchi yetu, ndiyo maana hata kuleta mageuzi inakuwa vigumu.
    Wahenga walisema; “kidole kimoja, hakivunji chawa”- ni misemo ambayo bado ina maana sana, kwa mfano leo Rais wa TFF ni Jamal Malinzi, hata awe ana nia nzuri kiasi gani ya kuleta mageuzi katika soka yetu, bila kuungwa mkono ni vigumu kufanikiwa.
    Na Malinzi naye anatakiwa kutambua kwamba, amepewa dhamana na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa TFF kuongoza soka ya Tanzania. Ni mali ya Watanzanua wote, akiwemo yeye. Si mali yake peke yake.
    Anahitaji kuungwa mkono, basi aonyeshe kwamba anafanya vitu kwa maslahi ya taifa. Asionyeshe chembe za ubinfasi ndani yake.
    Miradi yote miwili aliyoingia nayo Malinzi kwa ajili ya maendeleo ya soka yetu ni mizuri, ule wa mpito wa maboresho na ule wa muda mrefu wa kuanza kuunda timu ya vijana chini ya umri wa miak 17.
    Lakini miradi hii inahitaji kuungwa mkono na wadau, hususan sisi Waandishi wa Habari ili ieleweke vizuri na watu waweze kuisapoti.
    Tunafahamu, soka ya vijana haina mvuto wa kibiashara, si nchini kwetu tu, bali nchi nyingi nyingi duniani. Tazama hata zinapofanyika Fainali za Kombe la Dunia za U17 na U20, huwa hazivutii watu wengi viwanjani.
    Na kuandaa timu inahitaji fedha, kama huwezi kupata fedha za milangoni kutokana na soka ya vijana na pia huna wadhamini, kwa nchi masikini kama Tanzania hilo ni janga.
    Ndipo hapo unapoonekana umuhimu wa sisi Watanzania, kuunganisha nguvu zetu, kwa ajili ya kupambana kuiinua soka yetu. Si jukumu la mtu mmoja, ni jukumu letu sote.
    Tutaidharau na kuipa majina ya kifedhuli tutakavyo soka yetu, wachezaji wetu na timu zetu, lakini hivyo vibaya, vilivyoozaa, ndivyo vya kwetu. Vizuri vya wenzetu. Lazima tujue kwamba, mwanadamu hawezi kwenda peponi akiwa hai.
    Lazima tufe kwanza, ndiyo tufikirie pepo. Nasi kama tunataka soka yetu iwe kubwa kama Ivory Coast, tuwe na nyota kama Yaya Toure, lazima tusumbuke, lazima tuteseke kwanza, tukivuja jasho na kulia pamoja, ili baadaye tuje tufurahi pamoja pia kama taifa.  Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PEPONI TUTAKWENDA, LAKINI BAADA YA KIFO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top