• HABARI MPYA

    Saturday, November 29, 2014

    EL MERREIKH WAPATA MRITHI WA TRAORE, NI MKALI WA MABAO GHANA

    Na Gary Al-Smith, KUMASI
    KATIKA kujiandaa na maisha bila mshambuliaji wa Mali, Mohamed Traore aliye mbioni kwenda Azam FC ya Tanzania, El Merreikh imemsajili mfalme wa mabao Ligi Kuu ya Ghana, Augustine Okrah.
    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alishika chati ya ufungaji mabao katika Ligi Kuu ya Ghana msimu wa 2013/2014 kwa mabao yake 16 na pia kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu.
    Juzi jioni, alikamilisha uhamisho wake kutoka Bechem United ya Ghana kwenda kwa vigogo wa Omdurman, ambao wamemaliza Ligi Kuu ya Sudan katika nafasi ya pili.
    Augustine Okrah amesaini Merreikh kwenda kuziba pengo la Mohamed Traore aliye mbioni kutua Azam FC

    Lakini mazungumzo ya uhamisho wake yalipatwa na ukakasi kidogo, kutokana na historia ya maumivu ya goti aliyoyapata wakati anacheza kwa muda BK Hacken ya Sweden, Merreikh wakihofia kama anaweza kuwa amepona kabla ya msimu mpya wa Ligi ya Sudan.
    Lakini BIN ZUBEIRY inafahamu Okrah atakwenda kwa muda kucheza kwa mkopo Ahli ya Khartoum, ambayo imemsaini Mghana mwenzake, winga Francis Coffie. 
    Kipindi hicho kifupi cha mkopo ni kwa ajili ya kumpa fursa mkali huyo wa mabao arejeshe makali yake baada ya kupona maumivu ya goti, kabla ya kwenda kuanza kazi rasmi Omdurman.
    Okrah aliibuka miaka mitatu iliyopita, wakati kocha wa sasa Msaidizi wa timu ya taifa ya Ghana, Maxwell Konadu alipomsajili kwa mabingwa wa Ligi, Asante Kotoko kutoka akademi ya RedBull.
    Msimu wake wa kwanza alitolewa kwa mkopo Liberty Professionals, ambako alijijengea uzoefu kabla ya kurudishwa Kotoko ambako moja kwa moja alifanikiwa kung’ara.
    Alihamia Bechem United mwanzoni mwa msimu wa 2013/2014 ambako aliendeleza moto wake na kuisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu.
    Merreikh wanamchukua mshambuliaji huyo, wakati tayari inafahamika Mmali, Mohamed Traore yuko mbioni kuhamia Azam FC ya Tanzania.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: EL MERREIKH WAPATA MRITHI WA TRAORE, NI MKALI WA MABAO GHANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top