• HABARI MPYA

    Saturday, January 26, 2013

    SIMBA YAUA KWA SUMU YA OMAN, AZAM NAYO MOTO ULE ULE KWELI LIGI MSIMU HUU NI BALAA

    Ngassa akipiga pushapu za kutambaa baada ya kufunga bao la tatu, aliyesimama jirani yake ni Haruna Chanongo na kushoto ni kipa Abdul Seif akitahari


    Ngassa akiwa amejilaza kwenye nyavu baada ya kufunga. PICHA ZAIDI BAADAYE
    Na Mahmoud Zubeiry

    SIMBA SC leo imeanza vyema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa mabao 3-1 African Lyon ya Dar es Salaam katika mchezo wa ufunguzi wa duru hilo.
    Ushindi huo, unaifanya  
    Hadi mapumziko Simba SC walioweka kambi ya wiki mbili Oman kujiandaa na mzunguko huu, tayari walikuwa mbele kwa mabao 3-0, yaliyotiwa kimiani na Mrisho Khalfan Ngassa mawili dakika za 19 na 39 na Ramadhan Suleiman Chombo ‘Redondo’ dakika ya tatu ya mchezo huo.
    Redondo aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya tatu, akiunganisha krosi nzuri ya Ngassa kutoka wingi ya kushoto na kufumua shuti akiwa katikati ya msitu wa mabeki wa Lyon.
    Bao hilo liliwatia chaji Simba SC na kuanza kucheza soka maridadi zaidi, wakionana kwa pasi za mitindo yote, ndefu, fupi, za juu, chini hadi visigino na haikushangaza dakika ya 19 walipopata bao la pili.
    Ilikuwa ni kazi nzuri ya Ngassa mwenyewe, ambaye baada ya kupata pasi ya Mwinyi Kazimoto Mwitula aliitoka ngome ya Lyon kabla ya kumchambnua kipa wa timu hiyo, Abdul Seif.
    Baada ya kufunga bao hilo, Ngassa alikwenda moja kwa moja kwenye benchi la wachezaji wa akiba na kukumbatiana na Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ kisha kuwapa mikono wachezaji kadhaa na kurejea uwanjani.
    Lyon walipoteza nafasi nzuri ya kupata bao dakika ya 31, baada ya Shamte Ally Kilalile kukosa penalti.
    Refa Israel Mujuni alitoa penalti hiyo baada ya beki Paul Ngalema kumkwatua beki Fred Lewis aliyepanda kusaidia mashambulizi, hata hivyo mkwaju wa kwanza wa Shamte ulipanguliwa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja, lakini mwamuzi akaamuru irudiwe kwa madai kipa huyo alitokea kabla ya mpira kupigwa na safari hiyo mpigaji akapiga nje kabisa.
    Simba iliongeza kasi ya mashambulizi ikitumia mipira ya pembeni, kulia akiteleza Chanongo na kushoto Ngassa, timu ikichezeshwa vyema na viungo watatu katikati, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Jonas Mkude. Ilikuwa burudani kwa mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi, kwa jinsi ambayo timu yao ilitawala mchezo.
    Kazi nzuri ya Chanongo aliyeteleza wingi ya kulia huku akiruka madaluga ya mabeki wa Lyon, iliipatia Simba bao la tatu baada ya krosi yake nzuri kuunganishwa vyema kimiani na Ngassa.  
    Baada ya kufunga, Ngassa alishangilia kwa aina yake bao hilo, kwanza akitambaa hadi langoni na kisha kujilaza kwenye nyavu kubwa kama yeye ndio mpira.
    Baada ya hapo, aliinuka na moja kwa moja kwenda tena kwenye benchi la wachezaji wa akiba akianza kushangilia na Boban, baadaye wachezaji wengine na kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ambaye alitumia kama sekunde 30 akizungumza naye jambo.  
    Kipindi cha pili, Lyon walibadilika na kuwabana Simba SC wasiongeze mabao zaidi, huku wao wakifanikiwa kupata bao la kufutia machozi, lililofungwa na Bright Ike dakika ya 59, pasi ya Fred Lewis. 
    Dakika ya 64 Ngassa alipoteza nafasi ya kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja, baada ya kukosa penalti.
    Katika mechi nyingine, Mtibwa Sugar ililala 1-0 nyumbani mbele ya Polisi Morogoro, bao pekee la Muzamil Said dakika ya 76,  Coastal Union iliifunga Mgambo JKT 3-1, Ruvu Shooting iliilaza 1-0 JKT Ruvu, bao pekee la Abdulrahman Seif dakika ya 90 Azam FC imeshinda 3-1 dhidi ya Kagera Sugar na JKT Oljoro imeilaza 3-1 Toto Africans.
    Ushindi wa Azam ulitokana na mabao ya Abdi Kassim ‘Babbi’ dakika ya 20 na Khamis Mcha dakika za 31 na 66, wakati la Kagera lilifungwa na Paul Ngway dakika ya 82 na sasa timu hiyo imejiimarisha katika nafasi ya pili kwa kutimzia pointi 27, sasa ikizidiwa mbili tu Yanga iliyo kileleni.
    Uwanja wa Mkwakwani, Tanga mabao ya Coastal yalifungwa na Philip Mugenzi dakika ya 18, Daniel Lyanga dakika ya 78 na Joseph Mahundi dakika ya 81, wakati la Mgambo lilifungwa na Peter Mwalyanzi dakika ya 89.
    Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, mabao ya Oljoro yalifungwa na Hassan Isihaka dakika ya 15, Paul Nonga dakika ya 51 na 57, wakati la Toto lilifungwa na Selemani Kibuta dakika ya 73.
    Ligi hiyo itaendelea kesho wakati vinara, Yanga SC watakapomenyana na TZ Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Paul Ngalema/Kiggi Makassy, Mussa Mudde/Komabil Keita, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo, Mrisho Ngassa/Abdallah Seseme, Amri Kiemba na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
    African Lyon; Abdul Seif, Fred Lewis, Jacob Massawe, Mohamed Samatta, Abdulaghan Gulam/Hood Mayanja, Yussuf Mlipili, Jackson Kanywa, Aman Kyata/Yussuf Mgwao, Job Ibrahim, Shamte Ally/Bright Ike na Juma Seif ‘Kijiko’.

    MSIMAMO WA LIGI KUU YA VODACOM 2012/2103:   
                                    P    W  D   L    GF GA GD Pts
    1    Yanga                13 9    2    2    25 10 15 29
    2    Azam                 14 8    3    3    20 12 8    27
    3    Simba SC           14 7    5    2    23 12 11 26
    4    Mtibwa Sugar     14 6    4    4    18 13 5    22
    5    Coastal Union    14 7    4    3    19 15 4    25
    6    Kagera Sugar     14 5    6    3    16 13 3    21
    7    Ruvu Shooting   14 7    2    5    20 17 3    23
    8    Mgambo JKT      14 5    2    7    11 16 -5  17
    9    JKT Ruvu            14 4    3    7    13 21 -8  15
    10 JKT Oljoro           14 5    5    5    16 17 -1  17
    11 TZ Prisons           13 3    5    5    8    12 -4  14
    12 Toto African         14 2    6    6    11 18 -7  12
    13 African Lyon         14 2    3    9    10 23 -13 9
    14 Polisi Moro           14 1    4    9    5    16 -11 7

    MATOKEO KAMILI MECHI ZA LEO:
    Mtibwa Sugar 0-1 Polisi Morogoro
    Coastal Union 3-1 Mgambo JKT
    Ruvu Shooting 1-0 JKT RUVU
    Azam FC 3-1 Kagera Sugar
    JKT Oljoro 3-1 Toto Africans
    KESHO; Januari 27, 2013
    Yanga SC Vs TZ Prisons
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA YAUA KWA SUMU YA OMAN, AZAM NAYO MOTO ULE ULE KWELI LIGI MSIMU HUU NI BALAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top