• HABARI MPYA

    Tuesday, January 29, 2013

    DHAIRA, MUDDE WAANZA MAZOEZI SIMBA, SUNZU NA WENGINE WATATU NJE

    Felix Sunzu kushoto akitibiwa na Dk Cossmas Kapinga wa Simba kulia katika moja ya mechi za Ligi Kuu mzunguko wa kwanza msimu huu

    Na Mahmoud Zubeiry
    KIPA wa Simba SC, Abbel Dhaira na beki Mussa Mude wote raia wa Uganda waliokuwa majeruhi wamepona na leo wamefanya mazoezi na timu yao kwenye Uwanja wa Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam.
    Hata hivyo, wachezaji wengine wa timu hiyo wanne leo wameshindwa kufanya mazoezi kwa sababu mbalimbali.
    Msemaji wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ezekiel Kamwaga ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, wachezaji ambao hawajafanya mazoezi leo ni beki Paul Ngalema, viungo Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’ na mshambuliaji Felix Sunzu, raia wa Zambia.
    “Hawa wana kesi tofauti, wengine Malaria wengine maumivu maumivu tu madogo, lakini kuna matumaini kesho wataendelea na mazoezi,”alisema Kamwaga.   
    Lakini kurejea kwa Dhaira ni faraja kwa wapenzi wa timu hiyo, wenye hamu ya kumuona kwa mara ya kwanza akiwa amesimama kwenye milingoti mitatu tangu asajiliwe kutoka Uganda.
    Kipa huyo namba moja wa Uganda, hakuingizwa kwenye programu ya mechi ya kwanza ya timu yake ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara juzi dhidi ya African Lyon kutokana na maumivu ya nyonga.
    Katika mchezo huo, ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, ‘Tanzania One’ Juma Kaseja alianza langoni na kufanya kazi nzuri, ikiwemo kuokoa mkwaju wa penalti ya Shamte Ally.
    Hata hivyo, refa Israel Mujuni aliyetoa penalti hiyo baada ya beki Paul Ngalema kumkwatua Fred Lewis, aliamuru irudiwe kwa madai Kaseja alitokea kabla ya mpira kupigwa na safari hiyo mpigaji akapiga nje kabisa.
    Kwa upande wake, Mudde kiungo Mganda ambaye sasa anarudishwa kucheza nafasi ya ulinzi, Mussa Mudde alitolewa kipindi cha pili kwenye mechi dhidi ya Lyon, kutokana na kuumia misuli, lakini naye yuko fiti na ameanza mazoezi tena.
    Aidha, Kamgwa alisema kikosi cha Simba SC kinarudi kambini leo, katika hoteli maridadi na adilifu ya Sapphire, iliyopo Kariakoo, Dar es Salaam, kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu, dhidi ya JKT Ruvu, Februari 3, mwaka huu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: DHAIRA, MUDDE WAANZA MAZOEZI SIMBA, SUNZU NA WENGINE WATATU NJE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top