• HABARI MPYA

    Tuesday, January 29, 2013

    WAPAMBE MARUFUKU KWENYE PINGAMIZI, USAILI TFF

    Jamal Malinzi 

    KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema waliowekewa pingamizi na wa walioweka pingamizi hawaruhusiwi kufika katika kikao cha kesho (Januari 30 mwaka huu) wakiwa na vikundi vya ushangiliaji au wapambe.
    Kikao cha kupitia pingamizi kitafanyika saa 4 asubuhi na wapambe au washabiki wa waombaji uongozi pamoja na waweka pingamizi hawakiwi kuwepo kwenye eneo la kikao hicho.
    Wote walioweka pingamizi na waliowekewa pingamizi barua zao za mwito wa kuhudhuria kikao cha  Kamati ya Uchaguzi ya TFF zimeshatumwa kwenye anwani za barua-pepe zilizo kwenye taarifa za pingamizi au kwenye fomu za maombi ya uongozi.
    Leo waombaji uongozi watatumiwa barua za mwito kwa barua-pepe wa kuhudhuria usaili utakaofanyika tarehe 01-02 Februari 2013. Tarehe 01 Februari 2013 watasailiwa waombaji uongozi wa TPL Board na waombaji ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 1 hadi Kanda ya 8. Waombaji uongozi kupitia Kanda ya 9 hadi ya 13 na waombaji uongozi wa Makamu wa Rais na Rais wa TFF watasailiwa tarehe 02 Februari 2013 kuanzia saa 4 asubuhi.
    Vyombo vingi vya habari vimeonyesha nia ya kuwepo mdahalo wa wagombea uongozi katika TPL Board na TFF. Kanuni za Uchaguzi za TFF hazizuii jambo hilo kufanyika, bali tu lizingatie Kanuni za Uchaguzi za TFF. Mojawapo ya mambo ya kuzingatiwa ni kwamba mdahalo huo ufanyike wakati wa kipindi cha Kampeni na usiwe na taswira ya kuwapendelea au kuwabagua baadhi ya wagombea. Kanuni hazimlazimishi mgombea kushiriki mdahalo.
    Pia ni vema mdahalo ukaandaliwa na kuratibiwa  na Taasisi inayounganisha vyombo vya habari au waandishi wa habari kama TASWA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF lazima ijulishwe kwa maandishi nia hiyo ya kufanyika mdahalo na utaratibu utakaotumika mapema kabla ya kufanyika mdahalo huo ili kujiridhisha kuwa utaratibu utakaotumika kuandaa na kuendesha mdahalo haukiuki kanuni za Uchaguzi za TFF.
    Kamati ya Uchaguzi ya TFF inavishukuru vyombo vya habari kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi hadi sasa na kuwaomba waendelee kufanya hivyo hadi mwisho wa mchakato wa uchaguzi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: WAPAMBE MARUFUKU KWENYE PINGAMIZI, USAILI TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top