• HABARI MPYA

    Friday, January 25, 2013

    MJUE ABDULFATAH, MILIONEA KIJANA ANAYEMILIKI HOTELI MAARUFU DAR, MJUMBE KAMATI YA MASHINDANO SIMBA SC

    Abdulfatah akiwa Nahodha wa Simba SC, Juma Kaseja

    Abdulfatah Salim Saleh
    Na Mahmoud Zubeiry
    HIVI karibuni, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage alitaja Kamati mpya ndogo ndogo za klabu hiyo, baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Hiyo ilifuatia baadhi ya Wajumbe kutotekeleza majukumu yao vizuri, hali ambayo ilisababisha klabu hiyo kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara ikiwa katika nafasi ya tatu, na hivyo kuweka rehani taji lake la ubingwa wa ligi hiyo.
    Simba ilimaliza na pointi 24 mzunguko huo, ikiwa inazidiwa pointi tano na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC waliomaliza kileleni na kuzidiwa pia pointi moja na Azam iliyomaliza katika nafasi ya pili na pointi 25.
    Miongoni mwa watu wapya katika Kamati za Simba SC, ni milionea kijana mwenye umri wa miaka 32, Abdulfatah Salim Saleh, ambaye yeye ni Mjumbe wa Kamati ya Mashindano.
    Abdulfatah

    Abdulfatah ni nani?
    Ni mfanyabiashara na mmiliki wa hoteli maarufu Dar es Salaam, ambazo ni Sapphire iliyopo Kariakoo, Mtaa wa Sikukuu na Lindi na Al Uruba iliyopo Mtaa wa Mkunguni na Sikukuu, Kariakoo pamoja na maduka ya jumla ya vifaa vya mbalimbali, yaitwayo Al Ahly Diaper’s yaliyopo Mtaa wa Aggrey na Nyamwezi, na lingine Mtaa wa India na Moscow na nyumba za kupangisha (apartments) ziitwazo Samsa Real Estate Limited, zilizopo barabara ya Morocco.
    Ni kijana anayeendeleza utajiri wa ukoo wao, mfano wa wafanyabiashara wengine vijana waliondeleza vema bishara za wazazi wao, kama Yussuf Manji, Mohamed Dewji, Abubakar Bakhresa na wadogo zake, Abdallah Bin Kleb na wengineo.
    Abdulfatah

    Abdelfatah na Simba SC
    Abdulfatah alianza kuipenda Simba tangu akiwa mdogo, anasoma shule ya Msingi St. Austine Academy Nairobi, Kenya na kila alipokuwa likizo Dar es Salaam alikuwa hakosi mechi za timu hiyo.
    Anasema kilichomshawishi kuipenda Simba SC ni baba yake mdogo, Hassan Afif aliyeichezea na kuifundisha klabu ya Simba miaka ya 1990 mwanzoni. “Wakati baba mdogo anakuwa kocha mchezaji na kuipa Simba ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1991, nilihudhuria mechi zote hadi wanachukua ubingwa kwa kuifunga SC Villa ya Uganda, wakati huo nilikuwa likizo hapa,”anasema.
    Abdullfatah anasema wakati huo pia alikuwa anacheza mpira katika nafasi ya mshambuliaji na alikuwa ana ndoto za kufuata nyayo za baba yake mdogo kuvaa uzi wa Simba, lakini baba yake mzazi alimkataza na kutaka atilie mkazo masomo.
    “Baba alitaka nisome tu ili nije kuendeleza biashara, lakini ukiuliza niliocheza hata hapa Dar es Salaam wakati wa utoto, watakuambia nilikuwa mshambuliaji hatari sana,”anasema.
    Abdulfatah akiwa na mshambuliaji wa Simba SC, Emmanuel Okwi ambaye ameuzwa Etoile du Sahel ya Tunisia

    Ameingizwaje Kamati ya Mashindano?
    Anasema kwa kuwa yeye ni mfanyabiashara na ni mwanachama wa Simba SC, aliamua kuisaidia klabu yake sehemu ya kuwekea kambi kwa gharama nafuu na kusaidia baadhi ya mambo, ambayo hakupenda kuyataja.
    Kutokana na hilo, Abdulfatah anasema alijikuta anakuwa karibu na viongozi wa Simba SC, ambao aliiva nao kiasi cha kuamua kumuingiza kwenye Kamati hiyo.
    Anasema kwa moyo mkunjufu amekubali majukumu hayo na atashirikiana na wajumbe wenzake pamoja na Kamati ya Utendaji, kuhakikisha Simba SC inafanya vizuri katika mashindano yoyote inayoshiriki.
    “Tunaanza Ligi Kuu kesho, timu imetoka Oman, imefikia katika kambi nzuri kwenye hoteli yangu hapa Sapphire, wachezaji wanaishi vizuri na wanafurahi na wana ari kubwa, kuna matumaini ya ushindi, na tutahakikisha ubingwa wa Bara tunachukua na kwenye Ligi ya Mabingwa tunafika mbali”anasema.
    Huyo ndiye Abdulfatah, baba wa watoto watatu, milionea kijana anayeipiga jeki Simba SC.
    Abdulfatah, the boss

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MJUE ABDULFATAH, MILIONEA KIJANA ANAYEMILIKI HOTELI MAARUFU DAR, MJUMBE KAMATI YA MASHINDANO SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top