![]() |
| Nizar alipokuwa Marekani |
KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Nizar Khalfan aliyekuwa
anacheza soka ya kulipwa Marekani, amejiunga rasmi na `Mabingwa Watarajiwa’ wa
Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu, Simba.
Habari za kutoka ndani ya klabu hiyo ambazo bongostaz.blogspot.com imezipata zinasema kuwa,
usajili wa mchezaji huyo umefanikishwa na mmoja wa wafadhili wa zamani wa klabu
hiyo, Azim Dewji.
Dewji mwenyewe alipotafutwa kuzungumzia hilo, alikiri na
kusema kuwa, aliombwa na uongozi wa Simba kufanikisha usajili wa mchezaji huyo
na kwamba baada ya kufanikiwa, ameshamkabidhi Nizar kwa uongozi wa klabu.
“Kama Mwanasimba, nimetimiza wajibu wangu kama nilivyokuwa
nimeombwa na uongozi. Nimeambiwa ataungana na wenzake kuanza mazoezi wakati
wowote kuanzia Jumatatu (leo),” alisema na kuongeza kuwa, mchezaji huyo wa
zamani wa Mtibwa Sugar na Moro United atakuwa na nafasi ya kuanza kuichezea
Simba katika michuano ya kimataifa mwaka huu endapo itaingia hatua ya makundi
ya Kombe la Shirikisho.
Baada ya kuzing’oa ya Kiyovu ya Rwanda na Setif ya Algeria,
wiki hii Simba itaishukia Al Ahly Shandy ya Sudan na kama ikifanikiwa kuvuka
kiunzi hicho, itaingia katika raundi nyingine itakayoamua timu za kucheza Nane
Bora Afrika.
Habari zaidi zinasema kuwa, Nizar leo atakabidhiwa rasmi
jezi atakayoitumia akiwa Simba. Atakabidhiwa jezi hiyo siku moja kabla ya
mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Moro United unaotarajiwa kuanza saa kumi alasiri.
Mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hata hivyo hakuwa tayari
kutajwa jina akisema si msemaji, alikiri kukamilika kwa taratibu za Nizar kutua
Simba huku akiongeza kuwa, ataisaidia klabu hiyo katika michuano ya ligi na ile
ya kimataifa kuanzia msimu ujao.
“Ni kweli, timu inazidi kuimarika. Kumpata staa wa kimataifa
kama Nizar ni jambo la kujivunia, tunashukuru kwa juhudi zilizofanyika na
hatimaye kumpata mchezaji huyu,” alisema.
Nizar ambaye Juni 21 mwaka huu atatimiza umri wa miaka 24,
kabla ya kutua Simba aliichezea Philadelphia Union ya Ligi Kuu ya Marekani
aliyodumu nayo kwa miezi mitatu tu baada ya kujiunga nayo akitokea Vancouver
Whitecaps. Alikuwa Vancouver tangu Agosti 22, mwaka 2009 akitokea Moro United.
Katika soka ya ushindani, nyota huyo aliibukia timu ya taifa
ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys mwaka 2004 na baadaye
akajiunga na Mtibwa Sugar kabla ya kutimkia Kuwait kuichezea Al Tadamon ya huko
msimu wa 2007-2008. Kutoka Tadamon alikwenda Lebanon na kuichezea Tadamon Sour
ya huko na mwaka 2009 aliichezea Moro United.



.png)
1 comments:
Haya Khalfan tumekumiss hapa Vancouver...hongera sana kwa kujiunga na Simba, ingawa ulituambia siku moja wewe soka la bongo ni basi tena...kila la kheri.
Post a Comment