![]() |
| Marehemu Kanumba katika filamu ya Uncle JJ |
KAMA kuna mtu anayeteseka baada ya kifo cha mwigizaji Steven
Kanumba, basi ni mtoto Othman Njaidi OJ aliyeigiza naye kwenye filamu ya Uncle
JJ.
OJ ambaye aliibuliwa kipaji chake na Kanumba, ameigiza pia
filamu kadhaa zilizotamba.
Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini kuwa, tangu Kanumba
afariki, mtoto huyo amekuwa mpweke na na hana raha huku staili yake ya maisha
ikiwa imebadilika kwa kiasi kikubwa.
Ingawa mtoto huyo amekuwa hawezi kujieleza hali inayomkumba
kutokana na upweke huo, habari zilizothibitishwa na wanafamilia zinasema kuwa
hata kula analazimishwa na muda mwingi ni lazima asimamiwe na mama yake, jambo
ambalo halikuwepo awali.
Hali hiyo imeenda mbali zaidi kwani baada ya mazishi ya
Kanumba, OJ amekuwa akikurupuka usingizini na kupiga kelele akidai kutokewa na
msanii huyo, jambo ambalo limemfanya mama yake kumchukua na kulala naye.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mama wa Othman, Hidaya Njaidi,
alisema: "Mwanangu anapata shida sana tangu Kanumba afariki, usiku
anashtuka na kupiga kelele, ukimuuliza nini anakwambia ni Kanumba kamtokea.
"Mara nyingi hali hii inamsumbua sana, ndiyo maana sasa
nimeamua asilale peke yake. Nimemchukua nalala naye, kidogo naona hali hiyo
inaanza kupungua.
"Ukiangalia hata uwezo wake wa kula umepungua, amekuwa
mnyonge sana. Kila kitu inabidi kumsimamia, usipofanya hivyo anaweza asile
kabisa, kwa hiyo nafanya kazi ya ziada kuhakikisha anarudi kwenye hali ya
kawaida na kusahau yaliyopita.
"Alikuwa anafanya mambo mengi na Kanumba, ndiyo maana
amekuwa hivi, walishazoweana na mara kwa mara alikuwa anakutana naye."
Alisema pia kuwa, mtoto huyo amekuwa na msongo wa mawazo na
kila mara amekuwa akiuliza hatma yake kwenye fani ya uigizaji kwani anaona kama
ndiyo mwisho wake.
Mama huyo anasema mtoto wake alikuwa na ndoto ya kuwa msanii
mkubwa nchini na duniani miaka ijayo, lakini anahisi kama ndoto hiyo itafutika.
�Kila
siku anauliza swali moja tu kuwa 'mama kweli mimi nitaigiza tena kama
nilivyokuwa na Anko Kanumba?
"Ninatumia muda mwingi kumbembeleza maana nahisi hali
hiyo ikiendelea masomo yatamshinda, yupo katika majonzi mazito,� aliongeza mama huyo ambaye
anaishi na mwanaye Kimara Kona, Dar es Salaam.
Mama Njaidi anaelezea kuwa, mwanaye alikuwa ni rafiki mkubwa
wa Kanumba hata mikataba ya OJ ilisimamiwa na marehemu na kabla ya kifo alikuwa
asimamie mkataba wa kazi ya mtoto huyo na kampuni moja ya Dar es Salaam.
GAZETI LA MWANASPOTI LEO



.png)
0 comments:
Post a Comment