• HABARI MPYA

    Saturday, April 04, 2009

    YANGA YALALA TENA KWA AL AHLY


    Kocha wa Yanga, Dusan Kondic akimpongeza Flavio baada ya mechi jana


    “Ilikuwa ni mechi nzuri, tumepata nafasi tatu tumepoteza, Ahly walipata nafasi pekee ambayo waliitumia, hii ni timu yenye uwezo kuliko sisi, lazima tukubali, tunahitaji muda, hawa wamekaa pamoja karibu miaka saba,”.
    Naam, hayo yalikuwa maneno yake, kocha mkuu wa Yanga, Dusan Kondic, mara tu baada ya mchezo wa leo, ambao bao pekee la Flavio Amado katika dakika ya tano, liliizamisha timu yake kwenye Uwanja nyumbani, Taifa mjini Dar es Salaam ilipomenyana na Al Ahly ya Misri katika mchezo wa marudiano, raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Lilikuwa ni bao la kiulaini waliojipatia Waarabu hao, ambao baada ya kufanikiwa kuzima shambulizi la Yanga, walipiga mpira mrefu mbele wingi ya kulia, ambao pamoja na beki Wisdom Ndhlovu kuuwahi, lakini aliteleza kwenye eneo lililokuwa na maji, hivyo kiungo Ahmed Fathi akauwahi na kumtoka kabla ya kumpasia Mohamed Aboutrika aliyemuwekea Falvio, ambaye alikuwa peke yake hivyo kumchambua kiulaini kipa Juma Kaseja.
    Baada ya bao hilo, Yanga walionekana kama kucharuka kutaka kusawazisha, lakini wakaishia kukosa mabao matatu ya wazi, ambayo yaliokolewa wakati yakiwa yanaelekea kutinga nyavuni.
    Alianza Mrisho Khalfan Ngassa ambaye alifumua shuti kali lakini likiwa kama linaelekea kutinga nyavuni, kipa Ramzi Salman alilipangua na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
    Dakika nne baadaye, Mike Barasa aliukuta mpira kwenye njia, akiwa ndani ya eneo la hatari la Ahly, lakini licha ya kuupiga kuelekea nyavuni, beki mmoja aliyekuwa ndani ya lango aliuondosha hatarini, huku mashabilki wa Yanga wakiwa tayari kushangilia.
    Dakika ya 20, mpira uliotokana na kona iliyochongwa na Abdi Kassim ‘Babi’ ulisababisha kizaazaa langoni mwa Ahly na mchezaji mmoja wa Yanga alienda hewani na kuupiga ukawa kama unatinga nyavuni, lakini kipa aliuwahi na kuudaka.
    Hata hivyo, akiwa amekwishaudaka hewani, alipamiwa na mchezaji mmoja wa Yanga, hivyo ukamtoka na kudondokea nyavuni, wakati yeye akianguka chini, jambo ambalo lilimfanya mwamuzi Javier Bwegeya kutoka Rwanda apige filimbi ya faulo, iliyoelekezwa kwenye lango la wenyeji.
    Baada ya hapo, Waarabu walianza kuutawala tena mchezo huo, ingawa dakika tatu kabla ya mapumziko, Yanga walizinduka tena na kuanza kusukuma mashambulizi langoni mwa wapinzani wao hao, mabingwa mara sita Afrika.
    Kwa ujumla kipindi cha kwanza Ahly walicheza vizuri na walionekana kuizidi Yanga kiuwezo, ambayo hata hivyo wachezaji wake walipigana kiume kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
    Kipindi cha pili Yanga inayonolewa na Waserbia watatu, Kondic na wasaidizi wake Spaso Sokolovoski na Civojnov Serdan, ilianza na mabadiliko, ikimpumzisha Abdi Kassim ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Shamte Ally, lengo likiwa kuongeza kasi ya mashambulizi.
    Kweli ushirikiano wa wa Ngassa na Shamte uwanjani, kidogo uliongeza kasi ya Yanga mbele, lakini mabeki wa kati wa Ahly walikuwa makini mno kuondosha mipira yote ya krosi iliyotokana na ushirikiano wa wachezaji hao wawili wa zamani Kagera pamoja na beki Shadrack Nsajijgwa.
    Lakini baadaye Yanga mchezo uliwashinda kutokana na kuacha kucheza kitimu na kuamua kucheza kila mtu kivyake, yaani kila mchezaji akiupata mpira anataka awapangue wachezaji wote wa Ahly, kwani hilo liliwapa nafasi wapinzani kuutawala zaidi mchezo, wakigongeana pasi kibao.
    Kwa kifupi walikuwa wakiichezesha Yanga mchezo maarufu kwa jina la ‘hangaisha bwege’ na hapo ndipo mashabiki walipokata tamaa hadi dakika ya 75 wakaanza pole pole kuachia siti zao na kwenda kupanga foleni ya kurejea makwao.
    Kondic alifanya mabadiliko zaidi kwenye kipindi hicho akimtoa Mike Barasa na kumuingiza Ben Mwalala, baadaye Jerry Tegete aliingia kuchukua nafasi ya Boniphace Ambani, ambaye jana hakufurukuta kabisa. Kistaarabu unaweza kusema mpira ulimkataa kabisa, ila kwa watoto wa mjini, wanasema alichemsha.
    Mreno anayeinoa Ahly, Manuel Jose aliwapumzisha nyota wake Mohamed Barakat, akamuingiza Sayed Moawad, Falvio alimpisha Hanyfel Agizy na Aboutrika alimuachia Osama Hosny.
    Kwa ushindi huo, mbali na Ahly kuingia Raundi ya Pili kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-0, kutokana na kushinda awali mjini Cairo 3-0, pia imeendeleza ubabe wake kwa Yanga.
    Huo ulikuwa mchezo wa nne, Ahly wanaifunga Yanga na wa kwanza kuifunga nyumbani kwao, Dar es Salaam tangu zilipoanza kukutana mwaka 1982.
    Mara ya kwanza Yanga ilikutana na Ahly mwaka 1982, katika michuano hii, enzi hizo ikijulikana bado kama Klabu Bingwa na mchezo wa kwanza mjini Cairo wavaa jezi za njano na kijani walitandikwa mabao 5-0 na mchezo wa pili, uliokuwa wa marudiano mjini Dar es Salaam, walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1.
    Mara ya tatu, Yanga ilikutana na Ahly mwaka 1988 na katika mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam, Aprili 9 mwaka huo, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana na kwenye mchezo wa mwisho kuzikutanisha timu hizo, uliokuwa wa marudiano, Aprili 22, watoto wa Jangwani walitandikwa 4-0.
    Si Yanga tu, hata timu nyingine zote zilizowahi kukutana na Ahly hazikuweza kuvuka, wakiwemo Simba, Pamba FC na Majimaji ya Songea. Mwaka 1985, Simba iliifunga Al Ahly mabao 2-1 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, katika michuano ya Kombe la Washindi, kabla ya kwenda kufungwa 2-0 mjini Cairo. Mwaka 1993, Al Ahly iliifunga 5-0 Pamba mjini Cairo katika Kombe la Washindi pia, kabla ya kuja kulazimisha sare ya bila kufungana mjini Mwanza, wakati mwaka 1999, Waarabu hao walianza kwa kuichapa 3-0 Majimaji ya Songea, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya kwenda kuwaongeza 2-0 mjini Cairo.
    Pamoja na kuwapigia saluti Ahly kama ni bora, wakiwa mabingwa watetezi na mabingwa wa Super Cup, Kondic alilalamikia pia wachezaji wake kucheza bila viatu maalum vya kuchezea kwenye mvua, ambavyo timu yake haina, kwani kulichangia wachezaji wake kushindwa kucheza vizuri.
    Kondic alitolea mfano bao walilofungwa, kwamba Ndhlovu aliteleza kwenye maji na kumpa nafasi Fathi kuondoka na mpira. “Kama uliona walikuwa wanataleza sana na kuiacha mipira nyuma, hii haikuwa sawa, lakini yote kwa yote, tunakwenda kujipanga, nitakuwa na timu ya kushindana Afrika baada ya mwaka mmoja, tunahitaji muda,”alisema Mserbia huyo. Mvua kubwa ilinyesha Dar es Salaam tarkiban saa tatu mfululizo tangu saa 6:30 mchana.
    Kocha wa Ahly, Manuel Jose, alisema kwamba ametimiza azma yake ambayo ni kushinda na kuendeleza rekodi nzuri ya timu yake. “Ulikuwa mchezo mzuri kwetu, Yanga walicheza vizuri, lakini sisi tulikuwa kila kitu,”alitamba Jose akiwa mwenye tabasamu la bashasha.
    Pamoja na kufungwa na kutolewa, lakini Yanga itakuwa imenufaika na mapato makubwa kutokana na umati wa watu uliofurika uwanjani na kuwauzia haki za kurusha matangazo ya mchezo huo TV Al Ahly sambamba na kuwaruhusu kuweka mabango ya wadhamini wao uwanjani.
    Katibu Mkuu wa Yanga, Lucas Kisasa alisema mapema kabla ya mchezo huo, kwamba wamelipwa na Ahly kwa ajili ya kuweka mabango hayo uwanjani na pia kuutangaza mchezo huo, ingawa aligoma kutaja kiasi walichopata kutokana na biashara hiyo.
    Kikosi cha Yanga jana kilikuwa; Juma Kaseja, Nsajigwa Shadrack, Nurdin Bakari, Wisdom Ndhlovu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, George Owino, Mrisho Ngassa, Abdi Kassim/Shamte Ally, Boniphace Ambani/Jerry Tegete, Mike Barasa/Ben Mwalala na Athumani Iddi.
    Ahly: Ramzi Salman, Ahmed Sayed, Gilberto Sebastiano, Wael Gomaa, Shadi Mohamed, Hassan Ashour, Ahmed Fathi, Mohamed Aboutrika/Osama Hosny, Flavio Amado/Hanyfel Agizy, Mohamerd Barakat/Sayed Moawad na Elmotazbella Ahmed.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YALALA TENA KWA AL AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top