• HABARI MPYA

    Sunday, December 11, 2016

    SIMBA KUBADILI KATIBA LEO, MABILIONI YA MO YANUKIA MSIMBAZI

    Na Somoe Ng'itu, DAR ES SALAAM
    HATIMA ya Klabu ya Simba kubadili mfumo wake wa uendeshaji na kuwa wa hisa unatarajia kujulikana katika mkutano mkuu wa dharura utakaofanyika leo kwa wanachama wa klabu hiyo kuridhia mabadiliko katika ibara ya 49 ya katiba yao.
    Kupita kwa kipengele hicho ndiyo kutaruhusu mchakato wa kuuza hisa kuanza huku tayari bilionea Mohammed Dewji akiwa ameshawasilisha ofa ya kutaka kununua hisa asilimia 51 kwa thamani ya Sh. bilioni 20.
    Ibara hiyo inaeleza kuwa maamuzi yoyote yanayohusiana na klabu hiyo yatakuwa yamepata baraka endapo idadi ya 2/3 ya wanachama waliohudhuria mkutano watakubaliana na ajenda hiyo.
    "Kipengele hicho sasa kinatakiwa kusomeka kuwa maamuzi ya uwekezaji ndani ya klabu Simba yatakubaliwa endapo 2/3 ya wanachama wataridhia," mmoja wa wanachama wa Simba aliliambia gazeti hili jana.
    Baada ya ibara hiyo kupita, wanachama watakaohudhiria mkutano huo wa leo ambao utafanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi lililopo Oysterbay wataiboresha pia ibara ya 50 ambayo sasa inaeleza kuwa "Mali, kuvunjwa au kufutwa kwa Simba Sports Club kunahitaji ridhaa ya asilimia 2/3 ya wanachama ambao wako katika leja ya klabu".
    "Kipengele C katika ibara hiyo kinapendekezwa kusomeka kuwa mgawanyo wa hisa utafanywa na Kamati ya Utendaji," aliongeza mwanachama huyo.
    Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele, alisema jana kuwa maandalizi ya mkutano huo yamekamilika na anawaomba wanachama kujitokeza kuanzia saa 2:00 asubuhi.
    Kahemele alisema kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja huku pia ikipeleka mwaliko kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA KUBADILI KATIBA LEO, MABILIONI YA MO YANUKIA MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top