• HABARI MPYA

    Wednesday, March 18, 2015

    SIKU ZINAKWENDA, MAMBO YANABADILIKA, LAKINI SIMBA NA YANGA NI ZILE ZILE,VILE VILE!

    MAMBO yanakwenda yanabadilika, baada ya uwekezaji mzuri katika klabu za PSG za Monaco za Ufaransa, chini ya wamiliki wapya, wa kigeni imeanza kulipa.
    Timu za England, Chelsea na Arsenal zimetupwa nje ya michuano ya Ulaya na timu za Ufaransa, PSG na Monaco. Habari ndiyo hiyo.
    Miaka ya nyuma ilikuwa kawaida kusikia timu za kwa Malkia Elizabeth  zimetolewa na timu za Ujerumani, Italia na Hispania- labda na Ureno mara chache, lakini si Ufaransa.
    Mwaka 2015 imetokea- na PSG na Monaco zimekwenda Robo Fainali ya michuano mikubwa ya Ulaya kwa mgongo wa Chelsea na Arsenal.
    Mafanikio haya ni matunda ya wamiliki wapya kwa PSG, kampuni ya Qatar Sports Investments chini ya Rais wake, Nasser Al-Khelaifi.

    Qatar Sports Investments iliinua PSG mwaka 2011 wakati ipo ‘dhoofu l’hal’ na kufanya uwekezaji wa nguvu kuanzia kusajili wachezaji wa kiwango cha juu na kocha pia. 
    Kuajiriwa kwa kocha Carlo Ancelotti baadaye na kumwaga noti nyingi kwenye kununua wachezaji kulianza kwa kuleta taji la Ligue 1 msimu wa 2012–2013.
    Na mwaka huu, timu inaenda Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya- tusubiri kuona zaidi kutoka PSG. 
    Kwa Monaco nako, timu ipo chini ya mmiliki mpya, bilionea Mrusi, Dmitry Rybolovlev mwenye asilimia 67 ya hisa dhidi ya 33 za House of Grimaldi.
    Dmitry Rybolovlev ambaye ndiye Mwenyekiti wa klabu, aliinua Monaco Desemba 2011, wakati ikiwa inasuasua Ligue 2 (ngazi ya pili ya ligi za Ufaransa).
    Alianza kwa kumtimua kocha Laurent Banide kufuatia mwanzo mbaya wa msimu wa 2011–2012, akamuweka Marco Simone, ambaye alifanikiwa kuipandisha klabu hadi nafasi ya nane mwishoni mwa msimu.
    Katika kuhakikisha inajiimarisha ili kupanda Ligue 1, bodi ya klabu ikamfukuza kocha huyo na kumchukua Claudio Ranieri, ambaye mfumo wake wa kushambulia uliifanya timu ifunge mabao 64 msimu wa 2012–2013. 
    Huku klabu ikiwa imepoteza mechi nne tu, Monaco ilimaliza msimu kama bingwa. 
    Ikitumia ‘mahela’ ya Rybolovlev, Monaco ilikuwa moja ya klabu zilizotumia fedha nyingi katika dirisha la usajili mwaka 2013 Ulaya, ikitumia jumla ya Pauni Milioni 140, zikiwemo Pauni Milioni 50 alizonunuliwa Radamel Falcao kutoka Atletico Madrid.
    Unaweza kuona siri ya mafanikio ya timu hizi mbili za Ufaransa ni uwekezaji wa maana chini ya wamiliki wapya.
    Klabu nyingi kwa sasa Ulaya zinakubali kubadilika na kuuza hisa zake kwa wafanyabiashara wakubwa, ambao mwisho wake wanazifanya zinakuwa tishio na kuwapa raha mashabiki.
    Yule Moise Katumbi Chapwe au Moise Soriano jina alilopewa baada ya kuzaliwa, ni mtu ambaye aliinunua tu Mazembe baadaye na akatumia fedha zake kuifaya iwe klabu kubwa Afrika.
    Katumbi ni mfanyabiashara mkubwa DRC na mwanasiasa pia, Gavana wa jimbo la Katanga.
    Yeye ana fedha, lakini kuna kaka yake anaitwa Raphael Katebe Katoto, anaishi Ubelgiji- ni mfanyabiashara mkubwa Ulaya, huyo ndiyo fedha ‘zimesaza’.
    Klabu nyingine kadhaa duniani kama Chelsea na Manchester City zilikuja kuwa kuwa tishio baada ya kuwa chini ya wamiliki wapya, waliowekeza fedha nyingi.
    Nchini Tanzania kuna klabu mbili kongwe, Simba na Yanga. Hizo zinapendwa mno na zina mashabiki wengi.
    Rahisi mno wafanyabiashara wakubwa, tena duniani, siyo Tanzania pekee kuzinunua wakipata wasifu wake. 
    Lakini suala la kuuzwa kwa klabu hizo ni gumu, kwa sababu kuna watu wanaitwa wanachama akina Sudi Tall, Peter Lee na wengine, hao huwaambii kitu!
    Matokeo yake sasa, klabu zinazidi kudumaa wakati zingekuwa na manufaa makubwa chini ya wamiliki wapya.
    Kilichopo sasa watu wanakwenda kuwarubuni wanachama wanagombea Uenyekiti, wanashinda- siku zinakwenda, hakuna Uwanja wa kisasa wala mradi wa Bunju. 
    Miaka inakatika Simba na Yanga ni zile zile, vile vile, wale jezi nyekundu, wale kijani na njano. 
    Majengo yanachakaa tu Msimbazi na Jangwani. Kilichobaki ni ushindani wa zeyewe kwa zenyewe na kugombea ubingwa wa Bara. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIKU ZINAKWENDA, MAMBO YANABADILIKA, LAKINI SIMBA NA YANGA NI ZILE ZILE,VILE VILE! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top