• HABARI MPYA

    Sunday, March 15, 2015

    KAZI YA MUNGU HAINA MAKOSA, LAKINI KWA NINI MARSH HAKUWA MWANASIASA?

    TAIFA lipo katika majonzi, kufuatia kifo cha aliyekuwa kocha wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Sylvester Marsh aliyefariki dunia Alfajiri ya jana.
    Marsh alifariki dunia Alfajiri ya Jumamosi, Machi 14, 2015 katika hospitali ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya saratani ya koo.
    Mwili wa Marsh unatarajiwa kuagwa Jumatatu kuanzia Saa 4:00 asubuhi Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa Mwanza kwa mazishi.
    Marsh alianza kuwa Kocha Msaidizi wa timu za vijana Tanzania mwaka 2003 chini ya Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ kabla ya mwaka 2006 kupandishwa timu ya wakubwa, akianza kumsaidia Mbrazil, Marcio Maximo na baadaye Wadenmark, Jan Poulsen na Kim Poulsen.

    Hata hivyo, baada ya Jamal Malinzi kushinda Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Oktoba mwaka juzi, alibadilisha benchi zima la ufundi la Taifa Stars na Marsh akaondoka pamoja na Kim Poulsen. 
    Sasa Mholanzi, Mart Nooij ndiye kocha Stars, anasaidiwa na Salum Mayanga.
    Baada ya hapo Marsh akarudi kufanya kazi katika kituo chake cha Marsh Academy mjini Mwanza, lakini mwaka jana ndipo maradhi ya saratani ya koo yalipoibuka na akaletwa Muhimbili kwa matibabu.
    Rais wa TFF, Malinzi alikwenda kumtembelea Marsh awali alipolazwa, lakini inaelezwa hakuna msaada wa maana aliompatia.
    Ikabidi mfanyabiashara Abdulfatah Salim, mmiliki wa hoteli ya Sapphire Court, Dar es Salaam ajitolee kugharamia matibabu ya kocha huyo wa taifa hadi akafanyiwa upasuaji na hali yake kuimarika Februari mwaka jana, hivyo kurejea Mwanza.
    Marsh alipata ahueni ya kutosha na kuanza tena kazi ya kufundisha watoto wake wa Marsh Academy, kabla ya wiki hii kuletwa Dar es Salaam kuhudhuria kliniki.
    Nilibahatika kupata taarifa mapema juu ya Marsh kurejeshwa Muhimbili na hata hali yake kubadilika kuwa mbaya na mara zote nilifanya jithada za kuwasiliana na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa kumuelezea.
    Bila shaka, Mwesigwa na viongozi wote wa TFF walikuwa wametingwa na maandalizi ya Mkutano Mkuu- hatimaye hadi Marsh anafikwa na umauti hakupata msaada wao.
    Kweli kifo ni mipango ya Mungu na tunaamini kuna maradhi yasiyotibika, lakini vyote hivyo havipotezi ukweli, kwamba kocha Marsh alitengwa wakati wa maradhi yake.
    Labda angekuwa mwanasiasa mkubwa angesafirishwa Asia au Ulaya kwenda kutibiwa, lakini kwa sababu ni ‘kocha tu’, aliachwa hadi akasaidiwa na wasamaria wema. 
    Mbali na timu za taifa, Marsh pia amefundisha klabu za Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba na Azam FC ya Dar es Salaam, lakini wote kati yao hakuna aliyeguswa na matatizo ya mwalimu huyo.
    Miongoni mwa mafanikio yake akiwa kocha, mwaka 2005 aliiwezesha Kagera Sugar kutwaa Kombe la Tusker, ikiifunga Simba SC katika fainali mabao 2-1 Dar es Salaam.
    Mwaka 2004, akiwa Msaidizi wa Kibadeni katika U17, maarufu Serengeti Boys, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza Fainali za Afrika nchini Gambia, baada ya kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe. 
    Hata hivyo, timu hiyo iliyoibua vipaji vya wachezaji waliogeuka nyota wa taifa kwa miaka 10 iliyopita kama Nizar Khalfan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Amir Maftah na wengine, ilienguliwa fainali za Gambia kwa kashfa ya kumtumia Nurdin Bakari aliyekuwa amezidi umri.
    Mwaka 2009, Marsh akiwa Msaidizi wa Maximo Taifa Stars, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza fainali za kwanza za CHAN nchini Ivory Coast.
    Inaelezwa kwa muda wote wa Marsh kufanya kazi na timu za taifa hakuwahi kuwa na Mkataba, bali alikuwa kama ‘deiwaka’ maana yake hakuweka mbele maslahi, bali uzalendo.
    Kweli Marsh alifanya kazi timu za taifa, wakati Rais wa TFF ni Leodegar Tenga, lakini shirikisho hilo chini ya rais mpya, Malinzi bado lilistahili kumsaidia wakati wa maradhi yake, kwa sababu alifanya kazi ya timu ya taifa.
    Lakini katika hali ya kawaida, bodi hiyo ya soka nchini inaweza kumsaidia mchezaji au kocha yoyote mwenye matatizo. Hizo ndizo hisani zenyewe. Huo ndiyo uungwana wenyewe, mambo ambayo yanaupaka rangi nzuri mchezo wa soka duniani kote.
    Naenda mbali zaidi, hata Wizara inayohusika na michezo ilishindwa kumsaidia Marsh licha ya mchango wake mkubwa katika mchezo huo, ambao uko wazi?
    Sitaki kuingia katika mtego wa kumkufuru Mungu katika hili- narudia kusema, kifo ni kazi ya Mungu, lakini haiondoi ukweli kwamba Marsh alitengwa wakati wa maradhi yake. Labda angekuwa mwanasiasa nguli, angepelekwa Asia au Ulaya, hata Amerika kwa matibabu ya kuokoa uhai wake.
    Mungu ampumzishe kwa amani kocha Marsh. Marsh Academy imepoteza baba mlezi. Mwanza imepoteza mtu muhimu na taifa limempoteza kocha bora. Buriani Sylvester Marsh.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAZI YA MUNGU HAINA MAKOSA, LAKINI KWA NINI MARSH HAKUWA MWANASIASA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top