• HABARI MPYA

    Sunday, March 15, 2015

    ETI TFF WAMEKOSA NDEGE YA KUUSAFIRISHA MWILI MARSH MWANZA, SASA ATAPELEKWA KWA BARABARA, ANAAGWA MCHANA HUU MUHIMBILI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeiambia familia ya marehemu Sylvester Marsh, limekosa ndege ya kuusafirisha mwili wa marehemu Mwanza kwa mazishi- na sasa mwili wa kocha huyo wa zamani wa timu za taifa, kuanzia za vijana hadi ya wakubwa, Taifa Stars utasafirishwa kwa gari.
    Ndugu wa marehemu, Abubakar Balingula ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba, kwa sababu hiyo ratiba ya kuuaga mwili wa Marsh imebadilika na sasa unaagwa mchaa huu katika Hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam.
    “Majibu tuliyopewa na viongozi wa TFF ni kwamba wamekosa ndege ya kuusafirisha mwili wa marehemu hadi Mwanza kwa mazishi. Kwa hivyo, imebidi tufanye jitihada za haraka kuusafirisha Mwanza mwili wa ndugu yetu, ili tuwahi kumhifadhi,”amesema Balingula.
    Sylvester Marsh kushoto akiwa na Kim Poulsen enzi za uhai wake

    Marsh anatarajiwa kuzikwa kesho jioni mjini Mwanza na safari ya kuusafirisha mwili wake itaanza jioni ya leo.
    Marsh alifariki dunia Alfajiri ya jana katika hospitali ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya saratani ya koo na ilielezwa alikuwa amekuja Muhimbili kuhudhuria kliniki yake ya kawaida juu ya maradhi yake kabla ya hali yake kubadilika hadi kufariki dunia.
    Marsh alianza kuwa Kocha Msaidizi wa timu za vijana Tanzania mwaka 2003 chini ya Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ kabla ya mwaka 2006 kupandishwa timu ya wakubwa, akianza kumsaidia Mbrazil, Marcio Maximo na baadaye Wadenmark, Jan Poulsen na Kim Poulsen.
    Hata hivyo, baada ya Jamal Malinzi kushinda Urais wa TFF Oktoba mwaka juzi, alibadilisha benchi zima la ufundi la Taifa Stars na Marsh akaondoka pamoja na Kim Poulsen. Sasa Mholanzi, Mart Nooij ndiye kocha Stars, anasaidiwa na Salum Mayanga.
    Tangu hapo Marsh amerudi kufanya kazi katika kituo chake cha Marsh Academy mjini Mwanza, lakini mwaka jana ndipo maradhi ya saratani koo yalipoibuka na akaletwa Muhimbili kwa matibabu.
    Mfanyabiashara Abdulfatah Salim, mmiliki wa hoteli ya Sapphire Court, alimsaidia kocha huyo hadi akafanyiwa upasuaji na hali yake kuimarika Februari mwaka jana na kurejea Mwanza.
    Marsh alipata ahueni ya kutosha na kuanza tena kazi ya kufundisha watoto wake wa Marsh Academy, kabla ya wiki hii kuletwa Dar es Salaam kuhudhuria kliniki.
    Mbali na timu za taifa, Marsh pia amefundisha klabu za Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba na Azam FC ya Dar es Salaam.
    Miongoni mwa mafanikio yake akiwa kocha, mwaka 2005 aliiwezesha Kagera Sugar kutwaa Kombe la Tusker, ikiifunga Simba SC katika fainali mabao 2-1 Dar es Salaam.
    Mwaka 2004, akiwa Msaidizi wa Kibadeni katika U17, maarufu Serengeti Boys, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza Fainali za Afrika nchini Gambia, baada ya kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe. 
    Hata hivyo, timu hiyo iliyoibua vipaji vya wachezaji waliogeuka nyota wa taifa kwa miaka 10 iliyopita kama Nizar Khalfan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Amir Maftah na wengine, ilienguliwa fainali za Gambia kwa kashfa ya kumtumia Nurdin Bakari aliyekuwa amezidi umri.
    Mwaka 2009, Marsh akiwa Msaidizi wa Maximo Taifa Stars, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza fainali za kwanza za CHAN nchini Ivory Coast.
    Inaelezwa kwa muda wote wa Marsh kufanya kazi na timu za taifa hakuwahi kuwa na Mkataba, bali alikuwa kama ‘deiwaka’ maana yake hakuweka mbele maslahi, bali uzalendo. 
    Bwana ametoa, bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Mbele yake, nyuma yetu. Mungu ampumzishe kwa amani mwalimu Sylvester Marsh. Amina. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ETI TFF WAMEKOSA NDEGE YA KUUSAFIRISHA MWILI MARSH MWANZA, SASA ATAPELEKWA KWA BARABARA, ANAAGWA MCHANA HUU MUHIMBILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top