| Samatta |
MBWANA Ally Samatta na Patrick Ochan watakutana tena na wachezaji wenzao wa zamani, viongozi wao- kwa ujumla na timu ya zamani, Simba SC.
Katika kuhakikisha Simba inazidi
kuimarika kwa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika,
mfanyabiashara maarufu na mwanamichezo Azim Dewji anakusudia kuileta nchini timu
ya soka ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa
ajili ya kuipa makali Simba kabla ya
wawakilishi hao wa Tanzania
hawajaivaa Al Ahly Shandy ya Sudan.
Dewji aliyeifadhili Simba kwa
miaka mingi, alisema jana Dar es Salaam kuwa ziara inaratibiwa na
kampuni yake ya Simba Trailers na kwamba
ameshazungumza na kuafikiana na
Rais wa Mazembe, bilionea Moise Katumbi Chapwe na pia uongozi wa
Simba.
“Pamoja na kuwazawadia pesa wachezaji wa
Simba, nimeona nitoe mchango zaidi kwa kuwaletea mechi ya
kujipima nguvu na timu bora ya Mazembe ya
Kongo,” alisema Dewji aliyetoa
sh milioni 15 kwa Simba baada ya kuitoa ES Setif ya Algeria.
Kwa mujibu wa Dewji, mchezo
baina ya Mazembe na Simba unatarajiwa kufanyika Aprili 22 mwaka huu
jijini Dar es Salaam, ikiwa ni wiki moja kabla ya `Wekundu wa Msimbazi’
kuumana na Al Ahly.
Alisisitiza kuwa, Mazembe
itakuwa kipimo sahihi kwa Simba kutokana na kuwa na kikosi chenye hadhi ya
juu.
Mazembe iiliyotwaa ubingwa wa
Afrika mara nne, ikiwa pamoja na mwaka 2009 na 2010 kabla ya kuondolewa
mashindanoni mwaka jana kutokana na
dosari katika usajili wake,
inajivunia utajiri mkubwa wa fedha na vipaji vya mastaa kama Muteba
Kidiaba, Tresor Mputu, Given Singuluma, Stoppila Sunzu, Rainford Kalaba,
Patrick Ochan na washambuliaji raia
wa Tanzania, Mbwana Samata na
Thomas Ulimwengu.
Licha ya kutikisa katika Ligi ya
Mabingwa Afrika katika miaka ya hivi karibuni, Mazembe pia ilitamba
katika Klabu Bingwa wa Dunia mwaka 2010 huko Japan ambako ilifika
fainali, hatua ambayo haikuwahi kufikiwa na klabu yoyote ya Afrika katika
michuano hiyo.
“Kupambana na kikosi bora kwa
Afrika wakati kama huu itakuwa bahati kubwa kwa Simba, tuombe Mungu
mambo yote yaende vizuri ili wawakilishi
wetu wanoe makali ya kuitikisa
zaidi Afrika katika Kombe la Shirikisho,” alisema.
Wakati Simba imetinga raundi ya
tatu kwa kuing’oa Setif kwa faida ya bao la ugenini, baada ya sare ya jumla ya 3-3, Al Ahly Shandy
imeitupa nje ya michuano ya mwaka huu Ferroviario ya Msumbiji kwa
jumla ya mabao 3-0.
Mshindi baina ya Simba na Al
Ahly Shandy atatinga hatua ya Nane Bora ambayo timu nne kuchuana katika
kila kundi kusaka tiketi ya nusu fainali.
Nayo Mazembe, licha ya kujipima
na Simba kwao itakuwa fursa ya kuongeza makali ya kushiriki
katika Ligi ya Mabingwa Afrika, kwani nayo imesonga mbele baada ya
mwishoni mwa wiki kuifumua Power Dynamos ya Zimbabwe kwa 6-0. Timu hizo
zilifungana 1-1 katika mchezo wa kwanza huko Harare, Zimbabwe.


.png)
0 comments:
Post a Comment