![]() |
| Jeneza lake likishushwa kaburini |
![]() |
| Jeneza lake likishushwa kaburini |
![]() |
| Mama Kanumba kushoto akiwasili makaburini akisaidiwa na Asha Baraka |
![]() |
| Jeneza lake likipelekwa makaburini |
MWILI wa nyota wa filamu
Tanzania, mareheumu Steven Charles Kanumba, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi
umezikwa jioni hii makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam, baada ua kuagwa
viwanja vya Leaders, Kinondoni.
Umati mkubwa wa watu ambao
haujawahi kuonekana kwenye mazishi tangu kifo cha marehemu baba wa taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere Oktoba 1999, ulihudhuiria mazishi hayo kuanzia kwenye kuagwa
Leaders.
Watu wengi walizimia na kupoteza
fahamu. Ilikuwa majonzi huzuni na vilio vya kila namna.
Mke wa Rais Jakaya Kikwete, Mama
Salma Kikwete na Makamu wa rais Dk Ghalib Mohamed Bilal ni miongoni mwa
viongozi wa serikali waliohudhuria.
Lakini pia viongozi wa vyama vya
siasa, dini na asasi nyingine za kijamii, ikiwemo michezo, sanaa na burudani
walifika.
Jeneza la marehemu lilibebwa na
wasanii wenzake waliokuwa wamevalia nadhifu. Huruma kwa mama wa marehemu,
Florence Mtegoa aliyekuwa akisaidiwa na Asha Baraka.
Hakika kwa ujumla ni huzuni. Huzuni
kubwa. Wengi hawaamini kama Kanumba ameondoka na leo hii ndio alipumzishwa
katika nyumba yake ya milele,
Kanumba amebaki Kinondoni. Hatutamwona
tena. Tutabaki kumuangalia kupitia filamu zake nzuri, ambazo daima zitatamba na
kufanya vizazi na vizazi vimjue, alikuwa nani.
Kanumba alifariki dunia ghafla
usiku wa kuamkia Jumamosi na chanzo cha kifo chake inaelezwa ni kugombana na
mpenzi wake, mwigizaji mwenzake, Lulu.
Imeelezwa Lulu alikuwa
anazungumza na simu na Kanumba akataka kujua anaongea na nani.
Lulu hakutaka kumpa simu Kanumba
na ndipo wakaanza kuvutana na mwenzake akadondoka chini.
Inaelezwa alidondokea kisogo
katika eneo gumu na ndipo hali ikawa mbaya kabla ya kifo chake.
Lulu bado anashikiliwa kituo cna
Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.
AMEACHA NINI?
STEVEN Charles Kanumba alikuwa
anamiliki kampuni ya Kanumba The Graet Film, iliyokuwa na maskani yake eneo la
Sinza Meeda.
Kampuni hiyo, iliyokuwa imeajiri
watu watano, ambao ni Zakayo, Kiullo, Sethi, Biggie, Junior, Mya na dada
mwingine wa mapokezi, ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja.
Meneja wa kampuni hiyo,
inayojihusisha na utayarishaji wa filamu, Mayasa Mrisho ‘Mya’ amefanya
mahojiano na bongostaz mchana huu juu ya mustakabali wa kampuni hiyo, baada ya
kifo cha marehemu.
Katika mahojiano hayo, Mya
anasema kwamba kampuni iko vizuri na inaweza kuendelea na kazi, lakini
wanasubiri familia ya marehemu waamue.
“Sisi ni wafanyakazi, ila
kampuni ipo na inahitaji muendelezaji tu, wafanyakazi wapo na wenye uzoefu wa
kutosha, sisi tutasubiri tamko la familia ya marehemu tujue mustakabali
wetu,”anasema Mya.
Mya ambaye alimpokea Kanumba
katika kundi la Kaole mwaka 2002, anasema kwamba binafsi kwake kifo cha msanii
huyo ni pigo mara mbili.
PATO LA MAREHEMU NA TAARIFA ZA
FEDHA:
Mya hajui kampuni ilikuwa
inaingiza kiasi gani japo kwa mwezi, lakini pia hafahamu zaidi kuhusu sehemu
ambazo Kanumba alikuwa akiweka fedha zake au fedha za kampuni.
“Kwa watu ambao tunatakiwa
tunawalipa tulikuwa hatulipi kwa cheki, (Kanumba) alikuwa ananipa fedha cash
nalipa watu. Yaani mishahara nini au hata kama malipo yote kwa niaba ya
kampuni,”anasema Mya.
Lakini Mya anasema anakumbuka
marehemu alikuwa mteja wa benki ya NBC na benki nyingine.
Ni kiasi gani cha faida walikuwa
wanatengeneza kwa filamu moja?
“Mmh! Sijui,”anasema Mya. “Hiyo
ni siri yake mwenyewe na tulikuwa hatumuingilii,”.
Lakini uchunguzi wa bongostaz
umegundua katika kila filamu moja iliyokuwa ikiingia sokoni ya Kanumba kwa
takriban miaka miwili sasa, kama alilipwa kidogo ni Sh. Milioni 20.
Kwa miaka miwili Kanumba amekuwa
akifanya kazi na kampuni ya Steps Entertainment Limited iliyo chini ya
Mkurugezni wake Dilesh Solanki.
Siku za mwanzoni, Kanumba
alikuwa anaingiza filamu mpya kila mwezi sokoni ingawa sasa utaratibu
umebadilika na filamu moja ilikuwa kila baada ya miezi miwili au mitatu.
Jitihada za bongostaz kuzungumza
na Dilesh leo hazikuzaa matunda. “Tafadhali naendesha gari na leo niko bize
sana hatuwezi kuzungumza, labda umpigie msaidizi wangu Jay,”alisema Dilesh
alipopigiwa simu na bongostaz kuzungumzia kuhusu Kanumba.
Jay hakupatikana alipopigiwa
simu, na Mya anasema kwamba Kanumba alikuwa anapata fedha pia mikataba ya
matangazo ya biashara aliyokunayo.
“Kwa sasa nayojua ni tangazo la
Oxfam, Zantel na Star Times,”anasema.
MKE, MCHUMBA, MTOTO?
Mya anasema yeye kwake Kanumba
alikuwa zaidi ya bosi kazini, alikuwa kama ndugu yake na wote kila mmoja alikuwa
ana siri za ndani za mwenzake.
“Mimi nina siri nyingi za
Kanumba na yeye ana siri zangu nyingi, yaani alikuwa zaidi ya bosi pale
kazini,”anasema Mya.
Je, Mya anafahamu chochote
kuhusu Kanumba alikuwa ana mototo? “Kwa kweli katika siku zote za kuwa na Kanumba,
tangu tukiwa Kaole hadi anakutwa na umauti, sijawahi kusikia akiniambia habari
za kuwa na mototo.
Sijui. Na sidhani kama angekuwa
ana mtoto asingeniambia,”anasema Mya.
Kuhusu mchumba au mwenza wa
Kanumba katika maisha yake, Mya alikataa kuzungumzia hilo. “Hilo kwa kweli
siwezi kuzungumzia hata kidogo,”anasema.
ZAIDI YA NYUMBA YA KUPANGA?
Mauti yamemkuta Kanumba alikuwa
anaishi kwenye nyumba ya kupanga Sinza Vatican, aliyohamia takriban mwaka mmoja
kutoka kwao Tandika alipokuwa akiishi.
Je, Mya anafahamu kama Kanumba
alikuwa ana nyumba au alikuwa anajenga sehemu yoyote?
“Ndiyo,”anasema Mya. “Kanumba
alikuwa anajenga nyumba nzuri na ya kifahari Mbezi ya Kimara, ambayo ilikuwa
inakaribia kuisha masikini,”anasema.
KAZI ZILIZO JIKONI:
Mya anasema kwamba Kanumba
anafariki dunia, wakati filamu yake moja iitwayo Ndoa Yangu ikiwa njiani
kuingia sokoni.
“Hii nafikiri itakuwa
imeshalipwa na ni Steps hao hao ndio wanaiuza. Ni filamu moja kali sana kwa
kweli, nafikiri itaingia sokoni mwezi huu,”anasema Mya.
Lakini pamoja na hiyo, Mya
anasema kuna filamu nyingine ambayo rasmi hiyo ndio itakuwa picha ya mwisho
Kanumba.
Hiyo ni Mr Price ambayo kwa sasa
inafanyiwa editing na ilitakiwa kuingia sokoni baada ya Ndoa Yangu.
HISTORIA YAKE:
Steven Charles Kanumbaa
alizaliwa Januari 8, mwaka 1984 mkoani Shinyanga kabla ya umauti kumfiia Aprili
6, mwaka 2012.
Elimu ya msingi alipata katika
shule ya Bugoyi, na baadaye akajiunga na
sekondari ya Mwadui, kabla ya kuhamia Dar Christian Seminary.
Baada ya kumaliza Kidato cha Nne
Dar Christian, Kanumba alijiunga na sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam pia
kwa elimu ya Kidato cha Tano na Sita.
Ni ni wakati huo akiwa Jitegemee
Kanumba alianza shughuli za sanaa katika Kundi la Kaole Sanaa Group la Magomeni,
Dar es Salaam.
Baada ya kukomaa Kaole, Kanumba
aliamua kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya filamu na hadi anakutwa na umauti
alikuwa mwigizaji anayefahamika Afrika nzima.
Ameshirikiana na wasanii wakubwa
duniani kama Ramsey Nouah wa Nigeria na amefanya kazi na mastaa wengine kadhaa
wa Nigeria.
Miongoni mwa filamu ambazo
alifanya ni Dar To Lagos, She is My Sister, Ancle JJ, Oprah, Tufani, Johari,
Gharika, Baragumu, Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Cross My Sin, Village
Pastor, Family Tears na kadhalika.
Hivi karibuni, alikaririwa
akisema atagombea Ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
Kanumba atakumbukwa na wengi
sana kwa ucheshi wake- upole na ushirikiano mzuri na wenzake katika kazi.
Kifo cha Kanumba ni pigo katika
tasniya ya filamu Tanzania. Taifa limempoteza mtu ambaye alikwishaanza
kuitangaza vema nchi kupitia sanaa hiyo na ambaye angetarajiwa kuitangaza zaidi
katika anga za kimataifa zaidi kupitia sanaa hii.
Nigeria sasa wanajua Tanzania
sasa filamu. Nchi nyingi za Afrika zinajua sasa nah ii sehemu ya kazi nzuri kwa
Kanumba.
Mwenyewe aliwahi kukaririwa
alifika hadi Hollywood hadi Marekani, ambayo ni ‘makka’ ya wacheza filamu. Kwa
sasa mwili wa marehemu upo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es
Salaam.
![]() |
| Mama Kikwete |
Mungu aiweke pema peponi roho ya
marehemu. Amin.







.png)
0 comments:
Post a Comment