• HABARI MPYA

    Saturday, December 03, 2016

    MZEE MZIMBA AFARIKI DUNIA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KIONGOZI wa zamani wa klabu ya Yanga, Yussuf Mzimba amefariki dunia Alasiri ya leo mjini Dar es Salaam.
    Mtoto wa marehemu, Ramadhani Yussuf Mzimba ‘Kampira’ ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba baba yao amefariki katika hospitali ya Mwananyamala alipopelekwa kwa matibabu.
    “Mzee kwa muda alikuwa anasumbuliwa na maradhi ni kwa sababu ya utu uzima. Tulimpeleka hospitali leo kwa matibabu, akatibiwa, akaachwa apumzike na wakati amepumzika ndiyo umauti ukamfika,”amesema.
    Kampira amesema Mzee Mzimba alikwenda hospitali akitokea nyumbani kwa mwanawe mkubwa, Khalid eneo la Magomeni Kondoa na hapo ndipo msiba wake utakapowekwa.
    Yussuf Mzimba amefariki dunia Alasiri ya leo mjini Dar es Salaam
    Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete (kushoto) akimjulia hali Mzee Mzimba alipokuwa amelazwa hospitali ya Muhimbili wakati fulani mwaka 2013 
    Mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho jioni kjijini Msoga, Chalinze na mwili wa marehemu utaondokea Magomeni Kondoa, mtaa maarufu kwa jina la Bi Nyau Saa 4:00 asubuhi. 
    Mzimba amefariki dunia akiwa ana umri wa miaka 84 na enzi za ujana wake alikuwa Katibu Mwenezi wa Yanga miaka ya 1970 chini ya Mwenyekiti, Tarbu Mangara (marehemu pia).
    Ni sehemu ya viongozi waliofanikisha ziara maarufu za nje za klabu hiyo, Brazil mwaka 1973 na Romania mwaka 1978.
    Baada ya hapo, akaibuka kama mwanaharakati mwishoni mwa miaka ya 1990 kupinga timu hiyo kugeuzwa Kampuni.
    Alipambana na uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti Tarimba Abbas na baadaye chini ya Francis Kifukwe kabla ya kupatanishwa na Mwenyekiti wa sasa, Yussuf Manji.
    Baada ya suluhu hiyo Mzimba akawa miongoni mwa Wazee wa heshima wa Yanga kabla ya kujiweka kando na shughuli za klabu mwaka 2013 kufuatia kuanza kusumbuliwa kiafya. 
    Mungu ampumzishe kwa amani Mzee Mzimba. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MZEE MZIMBA AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top