• HABARI MPYA

    Tuesday, August 04, 2015

    ZUTTAH, COUTINHO WATUPIWA VIRAGO YANGA SC, BEKI MTOGO, MIDO LA ZIMBABWE MBIONI KUTUA JANGWANI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BEKI Mghana Joseph Tetteh Zutah na kiungo Mbrazil Andrey Coutinho wanaweza kutemwa Yanga SC kupisha wachezaji wengine kabla ya dirisha la usajili la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa wiki.
    Dirisha la usajili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara linatarajiwa kufungwa Agosti 6, mwaka huu na baada ya hapo kutakuwa na nafasi ya kusajili wa wachezaji huru tu kwa wiki moja ya mwisho kabla ya kuanza msimu mpya. 
    Baada ya Yanga SC kutolewa katika Robo Fainali michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame imekitathmini kikosi chake na kugundua Zuttah na Coutinho hawana faida.
    Joseph Tetteh Zuttah (kulia) na Andrey Coutinho (kushoto) wote wapo hatarini kutemwa Yanga SC

    Coutinho alijiunga na Yanga SC msimu uliopita akiletwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mbrazil mwenzake, Marcio Maximo na hadi sasa ameichezea timu hiyo mechi 33 na kuifungia mabao sita.
    Mbrazil huyo alikuwa ana wakati mzuri chini ya kocha Maximo, lakini tangu ujio wa Mholanzi, Hans van der Pluijm amepoteza nafasi katika kikosi cha kwanza.
    Zuttah amesajiliwa Juni mwaka huu kufuatia kupendekezwa na kocha Pluijm, lakini baada ya wiki mbili za Kombe la Kagame, uongozi umeona hana umuhimu.
    Mbali na Sherman, Coutinho na Zuttah wachezaji wengine wa kigeni Yanga SC ni Mkongo, Mbuyu Twite, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma.
    Yanga SC ilifungwa kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 katika Robo Fainali ya Kagame dhidi ya Azam FC wiki iliyopita na tathmini ya baada ya mashindano, inaonyesha timu inahitaji marekebisho madogo. 
    Na kwa kuona uimara wa Azam FC iliyotwaa Kombe la Kagame mwishoni mwa wiki na namna wapinzani, Simba SC wanavyojiimarisha, Yanga SC imeona kuna umuhimu wa kuleta wachezaji wengine bora zaidi kuchukua nafasi za Coutinho na Zuttah.
    Nahodha wa FC Platinum ya Zimbabwe kiungo, Thabani Kamusoko, tayari yuko kwenye rada za Jangwani achukue moja ya nafasi hizo mbili. 
    Aidha, wakala Mganda, Gibby Kalule aliyewahi kuwauzia Yanga SC, mshambuliaji Mliberia, Kpah Sherman amependekeza beki wa kimataifa wa Togo, Vincent Bossou mwenye umri wa miaka 29 anayechezea Goyang Hi FC ya Korea Kusini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ZUTTAH, COUTINHO WATUPIWA VIRAGO YANGA SC, BEKI MTOGO, MIDO LA ZIMBABWE MBIONI KUTUA JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top