• HABARI MPYA

    Saturday, August 01, 2015

    NINI KILIMSIBU PONDAMALI KATIKA SIKU HII?

    Kocha wa makipa wa Yanga SC, Juma Pondamali (kushoto) akiwa na mabosi wake, Charles Boniface Mkwasa (katikati) na Hans van der Pluijm (kulia) Jumatano wakati wa mchezo dhidi ya Azam FC
    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    IMEZOELEKA Juma Pondamali ‘Mensah’ ni mchangamfu na mcheshi wakati wote, tangu anacheza.
    Kipa huyo wa zamani wa kimataifa nchini aliyewika Yanga SC na Pan African- ambaye alipewa jina la utani Mensah enzi zake, alikuwa katika hali tofauti kabisa Jumatano wiki hii.
    Katika siku ambayo Yanga SC ilitolewa na Azam FC kwa mikwaju ya penalti, Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Pondali alikuwa mnyonge tangu mwanzo.
    Baada ya makocha wa Yanga SC kuingia uwanjani na kwenda kuketi katika benchi lao, Pondamali alikuwa mnyonge aliyeshika tama muda mwingi wakati mabosi wake, Mholanzi, Hans vand der Pluijm na mzalendo, Charles Boniface Mkwasa wakitafakari mchezo.
    Dakika 90 za mchezo huo uliofanyika Jumatano jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zikamalizika kwa sare ya 0-0 na sheria ya mikwaju ya penalti ikachukua nafasi yake kuamua mshindi.
    Makocha wote wa Yanga SC na wachezaji wa akiba waliungana na wenzao waliotoka uwanjani kuwapa ‘mawili matatu’ kuelekea kwenye matuta, lakini Pondamali hakuinuka kwenye benchi.
    Mkwasa akimuelekeza Barthez namna ya kudaka penalti
    Dida akimuandaa Barthez kwenda kudaka penalti

    Ikabidi kazi ya kumuandaa kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ kuelekea kwenye matuta ifanywe na kipa mwenzake, Deo Munishi ‘Dida’. Na baadaye, kocha Mkwasa akamuita Barthez na kuanza kumpa maelekezo namna ya kucheza penalti.
    Mkwasa hajawahi hata kuwa kipa, enzi zake alikuwa beki na kiungo- lakini akawa anamuelekeza Barthez namna ya kudaka penalti.
    Hata wakati wa dua ya kabla ya wachezaji wa Yanga SC kurudi uwanjani kwa ajili ya penalti, Pondamai aliinuka mwishoni kabisa kwenda kujiunga na mduara.
    Hakuwa katika hali ya kawaida Pondamali, kama ambavyo amezoeleka, mchangamfu na mcheshi muda mwingi.
    Barthez akaenda kutunguliwa penalti zote tano na Mwinyi Hajji Mngwali akakosa penalti moja ya Yanga, Azam FC ikasonga mbele kwa ushindi wa penalti 5-3. Nini kilikuwa kimemsibu Pondamali siku hiyo?
    Dua ya kuelekea kwenye penalti imeanza, lakini Pondamali hajajiunga na mduara
      
    Pondamali (kushoto) alitokea mwishoni kabisa kujiunga na mduara wa dua
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NINI KILIMSIBU PONDAMALI KATIKA SIKU HII? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top