• HABARI MPYA

    Sunday, August 02, 2015

    AZAM FC BINGWA KOMBE LA KAGAME 2015, GOR MAHIA WAFA 2-0 TAIFA

    Nahodha wa Azam FC, John Raphael Bocco akishangilia baada ya kuifungia Azam FC bao la kwanza katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Gor Mahia leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    AZAM FC wametwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya kuifunga mabao 2-0 Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wa fainali uliofanyia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.
    Azam FC wanakuwa timu ya kwanza ya Tanzania nje ya Simba na Yanga SC kutwaa taji hilo- wakishiriki kwa mara ya tatu tu mashindano hayo baada ya mwaka 2012 walipofika fainali na kufungwa na Yanga SC 2-0 Dar es Salaam na mwaka jana kutolewa kwa penalti 4-3 mjini Kigali, Rwanda baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika ya 90 katika Robo Fainali na El Merreikh ya Sudan walioibuka mabingwa.
    Timu hiyo yenye maskani yake Azam Complex, Chamazi, Mbade, Temeke mjini Dar es Salaam imeshinda mechi zake zote kuanzia Kundi C bila kuruhusu nyavu zake kuguswa hata mara moja- na ‘ilipata shida’ kidogo tu mbele ya Yanga SC katika Robo Fainali ilipolazimika kushinda kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 0-0 dakika 90, wakati Nusu Fainali iliilaza KCCA 1-0. 

    Kikosi cha Azam FC kilichoanza leo; Waliosimama kutoka kulia ni John Bocco, Shomary Kapombe, Serge Wawa Pascal, Aggrey Morris, Ame Ali 'Zungu' na Jean Baptiste Mugiraneza. Walioinama kutoka kulia ni Said Mourad, Himid Mao, Aishi Manula, Farid Mussa na Kipre Herman Tchetche 
    Kwa ushindi huo, timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake inazawadiwa kitita cha dola za Kimarekani 30,000 (Sh. Milioni 60), wakati Gor Mahia wanapozwa na dola 20,000 (Sh. Miliioni 40).
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Louis Hakizimana wa Rwanda aliyesaidiwa na Nagi Ahmed wa Sudan na Suleiman Bashir wa Somalia, hadi mapumziko tayari Azam FC walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0.
    Bao hilo lilipatikana dakika ya 16, mfungaji Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyemalizia kwa kichwa krosi ya Kipre Herman Tchetche kutoka upande wa kulia.
    Azam FC walitawala mchezo vizuri kwa dakika 20 za mwanzo, lakini baada ya hapo kasi yao ikapunguzwa na uchezaji wa rafu wa wachezaji wa Gor Mahia ambao hawakuchukuliwa hatua yoyote na refa Hakizimana. 
    Wachezaji wa Gor walikuwa wakiwapiga viwiko na mateke wachezaji wa Azam FC na kuanguka chini wakitokwa hadi damu, lakini hiyo haikumfanya refa Hakizimana japo kutoa kadi ya njano.
    Hali hiyo iliwafanya washambuliaji wa Azam waanze kucheza kwa woga na kupunguza kasi yao ya mashambulizi- huku Gor Mahia wakitumia mwanya huo nao kuanza kushambulia.
    Medie Kagere alikaribia kuisawazishia Gor Mahia dakika ya 22 kama si beki muhimili wa ukuta wa Azam FC, Serge Wawa Pasacal kuokoa.
    Kipindi cha pili, kocha Stewart Hall wa Azam FC alianza na mabadiliko akimtoa winga Farid Mussa Malik na kumuingiza beki David Mwantika.
    Mabadiliko hayo yaliyolenga kuimarisha ulinzi yaliisaidia Azam FC kupunguza kasi ya Gor Mahia na kufanikiwa kuendelea kutawala mchezo. 
    Mshambuliaji nyota kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche akaifungia bao la pili Azam FC dakika ya 64 kwa shuti la mpira wa adhabu lililompita kama mshale kipa wa Gor Mahia, Boniphace Olouch.
    Mfungaji wa bao la pili la Azam FC, Kipre Herman Tchetche akimtoka beki wa Gor Mahia
    Mshambuliaji aliyechezeshwa nafasi ya kiungo leo, Ame Ali 'Zungu' kulia akizuia shuti la beki wa Gor Mahia, Harun Shakava
    Winga machachari wa Azam FC, Farid Mussa Malik akiruka na mpira wake kwanja la beki wa Gor Mahia, Harun Shakava   

    Faulo hiyo ilitokana na beki Harun Shakava kumuangusha beki wa Azam FC, Shomary Kapombe nje kidogo ya boksi.
    Mchezo uliotangulia mchana wa leo, KCCA ya Uganda iliifunga 2-1 Khartoum N ya Sudan na kumaliza katika nafasi ya tatu.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Aggrey Morris, Morald Said, Pascal Wawa, Farid Mussa/Erasto Nyoni dk46, Shomari Kapombe, Jean Mugiraneza, Himid Mao, Ame Ali/Frank Domayo dk69, John Bocco na Kipre Tchetche/dk88.
    Gor Mahia; Boniphace Olouch, Mussa Mohammed, Sibomana Abouba, Harun Shakava, Karim Nzigiyimana, Innocent Wafula/Enock Agwanda dk83, Khakid Aucho, Godfrey Walusimbi, Medie Kagere/George Odhiambo dk83, Michael Olunga na Erick Ochieng/Ali Abondo dk74. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC BINGWA KOMBE LA KAGAME 2015, GOR MAHIA WAFA 2-0 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top