• HABARI MPYA

    Monday, March 16, 2015

    BENDI KUSHIRIKIANA NI JAMBO JEMA LAKINI MASHARTI NA VIGEZO VIZINGATIWE

    Kama mambo yataenda kama yalivyopangwa, Jumapili hii ya tarehe 22 tutashuhudia onyesho kubwa la taarab kati ya Jahazi Modern Taarab na Mashauzi Classic Modern Taarab ndani ya ukumbi wa Travertine Hotel Magomeni jijini Dar es Salaam na baada ya hapo tutapata mpambano wa FM Academia na Twanga Pepeta Machi 28 katika ukumbi wa Escape One. Ni jambo jema sana.
    Onyesho la Jahazi na Mashauzi Classic limepewa jina la Usiku wa Baba na Mwana na linafanyika baada ya miaka minne tangu makundi hayo mawili yenye mashabiki wengi kukutana kwa mara ya kwanza mwaka 2011 katika ukumbi huo huo wa Travertine na kilichotokea katika onyesho la kwanza bado kinaendelea kuwa historia isiyofutika. FM Academia na Twanga Pepeta wao wanakuja na ‘title’ ya Nani Zaidi na hii inakuwa ni mara yao ya kwanza kukutana kwa staili hiyo.

    Kufanyika kwa maonyesho hayo kunaonyesha kuwa maonyesho ya pamoja kwa bendi kubwa zenye mashabiki wengi ni jambo linalowezekana tofauti na wengi wanavyodhani kuwa ni kitu kisichowezekana.
    Jana asubuhi nilibahatika kusikiliza kipindi cha taarab cha “Tam Tam za Mwambao” cha East Africa Radio kinachotangazwa na Mwanne Othman “Toto la Matashtiti” na nikavutiwa na mada yake ilosema: “Kwanini bendi za taarab hazina ushirikiano wa kufanya maonyesho ya pamoja kwa kuhofia bendi kubwa kuipandisha chati bendi ndogo”.
    Katika kusherehesha mada yake Mwanne akasema mara nyingi maonyesho yanayofanikiwa kuzikutanisha bendi mbili au zaidi ni yale yanayoandaliwa na mapromota lakini si baina ya bendi na bendi.
    Watu kadhaa wakapiga simu kuchangia mada hiyo na wengi wao wakaishia kutaja roho mbaya kama sababu kubwa, wachache wakasema labda ni ile tabia ya waimbaji wa taarab kupigana vijembe kwenye nyimbo zao ndiyo inayochangia bendi kushindwa kufanya maonyesho ya pamoja.
    Hakika ilikuwa mada nzuri lakini inayohitaji majibu yaliyojaa uchambuzi wa kina na si majibu mepesi mepesi yaliyokosa mashiko.
    Nilifurahishwa sana na majibu ya mkurugenzi wa Mashauzi Classic, Isha Ramadhan pale alipotafutwa na Mwanne ili kutoa ufafanuzi juu ya mada hiyo. Yalikuwa ni majibu ya kiufundi ambayo ndiyo yamenilazimisha kuweka kichwa cha habari cha makala hii: “Bendi kushirikiana ni jambo jema lakini masharti na vigezo vizingatiwe.” Naandika hivi nikiamini kuwa mada hiyo pia inagusa hadi kwenye muziki wa dansi kwa vile hata upande huo imani hiyo pia ipo ingawa tumeshashuhudia maonyesho mengi tu kama vile Sikinde na Msondo, Mapacha na FM, Mashujaa na FM, Twanga na Msondo, Mashujaa na Akudo.
    Labda nirudie kwa kifupi sana kusema kile alichokisema Isha. Mwimbaji huyo alisema si kweli kuwa bendi za taarab hazifanyi maoyesho ya pamoja, akatoa ushahidi kuwa ndani ya miaka miwili East African Melody wameshafanya maonyesho matatu ya taarab yaliyoandaliwa na bendi na si promota.
    Isha akataja onyesho lao na Jahazi la Jumapili inayokuja kama mfano mwingine ambapo alisema ni yeye na Mzee Yussuf walikaa na kukubaliana kufanya onyesho hilo na wakaamua kumshirikisha mdau mmoja ili kuongeza uzito wa tukio hilo.
    Katika kunogesha zaidi Isha akafafanua kuwa maonyesho yanayoshindikana kufanyika ni yale yanayoshindwa kukidhi vigezo. “Anatokea kiongozi wa bendi fulani akiwa anajua kabisa kuwa thamani ya show ya bendi anayoitaka labda ni shilingi milioni moja au mbili lakini yeye anataka atoe laki mbili au laki tano, anapoambiwa haiwezekani basi anakwenda kuwa kinara wa kupaka matope kuwa bendi fulani ina roho mbaya,” alisikika Isha akifafanua.
    Binafsi nimekuwa muumin mkubwa wa kuhimiza ushirikiano wenye faida baina ya bendi za taarab na bendi za dansi lakini kamwe sitathbutu kuhimiza ushirikiano utakaozalisha hasara baina ya bendi na bendi. Tujifunze kusoma alama za nyakati, ni mara ngapi tumekuwa tukishuhudia uzinduzi wa bendi au albam mpya halafu wasanii waalikwa wakashindwa kulipwa pesa zao?
    Bendi yako ndogo halafu unataka mambo makubwa, unaalika bendi kubwa na wasanii wakubwa kwa bei za kulalia lakini mbaya zaidi ni kwa mkopo, malipo ni baada ya show ukiamini kuwa utauza tiketi nyingi, mwisho wa siku biashara inakataa na unashindwa kulipa madeni. Baada ya mwaka mmoja unasahau kilichokusibu na unathubutu kurudia tena kitu kile kile, bendi au wasanii waalikwa wanakuchomolea, unaondoka na malalamiko kibao, unachafua kila kona na watu wanakuamini. Inakera sana.
    Jambo lingine ni hili: Umeanzisha bendi kwa nia ya kuanzisha vita vya kibiashara (si ushindani wa kibiashara) na bendi fulani, dhamira yako iko wazi kabisa kuwa ni kuiteketeza kabisa bendi hiyo lakini mwisho wa siku dhamira yako haifanikiwi na unaanza kutafuta njia za kufanya ushirikiano wa kinafiki lakini wenyewe hawakupi nafasi hiyo. Kinachofuata baada ya hapo ni malalamiko kuwa mtu fulani au bendi fulani ina roho mbaya. Hatuendi hivyo waungwana.
    Muziki ni kazi, muziki ni maisha tusiwe wepesi wa kulalamika ovyo kwa kila jambo, tuzingatie gharama za uendeshaji wa bendi, tuheshimu kazi za watu, tuheshimu taratibu walizojiwekea watu, tusiwe na mazoea ya kutaka mambo yaliyotuzidi kimo na mwisho kabisa tunapaswa tukubali kuwa vigezo na masharti ni lazima yazingatiwe. Tukutane Travertine Machi 22 na tukutane Escape One Machi 28.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BENDI KUSHIRIKIANA NI JAMBO JEMA LAKINI MASHARTI NA VIGEZO VIZINGATIWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top