• HABARI MPYA

    Friday, January 30, 2009

    WANARIADHA MAARUFU WAJA KILI MARATHON

    WANARIADHA maarufu duniani wanatarajia kushiriki kwenye mbio za Kilimanjaro Marathon zitakazofanyika mjini Moshi Machi 1 mwaka huu.
    John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo amesema kuwa wanariadha maarufu Watanzania kama Jumanne Tluway na Banuelia Brighton watachuana na washiriki wengine wa kimataifa kwenye mbio hizo.
    Jumanne Tluway alishinda mbio hizo za km 42 mwaka jana kwa kumaliza katika muda wa 02:15:37 akifuatiwa na Andrea Silvini (02:16:22). Banuelia Brighton alishinda mbio za km 42 kwa upande wa wanawake akimaliza katika muda wa 02:48:37.
    Addison aliongeza kuwa Tluway ameshiriki katika mashindano mengine mengi ya kimataifa kama vile Hamburg Marathon, Dresden Marathon, Mashindano ya Taifa ya Riadha 2008 ambapo alishinda mbio za km 21 kwa 1:04:00, na Great Standard Chartered Mumbai Marathon. Kati ya wanariadha wengine mashuhuri waliothibitisha kushiriki katika siku chache zilizopita ni pamoja na Martin Sulle (mshindi wa Kili Marathon km 21 mwaka 2006 kwa muda wa 01:04:03, mshindi wa tatu wa Villamora World Half Marathon Championship akiwa na rekodi nzuri ya 1:00:00), Peter Sulle (mshindi wa tatu wa Kili Marathon km 21 mwaka 2007 katika muda wa 1:04:56), na Samwel Shauri (mshindi wa nne Kili Marathon km 21 mwaka 2008).
    Washiriki walemavu waliothibitisha kushiriki mbio za km 21ni pamoja na Wilbert Constantino (Paralyimpic 2004) and John Joro (Jumuiya ya Madola 2006).
    Mkurugenzi Mkuu wa Executive Solutions Aggrey Marealle amesema "Kili Marathon inatambulika kimataifa ikiwa na washiriki kutoka nchi zaidi ya 30 ambapo ushiriki wa wageni hutoa changamoto na kuwapa uzoefu kwa wanariadha wa Tanzania".
    "Mbio hizi ni chimbuko la wanariadha wa kizazi kipya watakaoiletea Tanzania sifa siku zijazo, kupitia mbio hizi tunawapa mwanya ambao wa kujiendeleza. Jitihada thabiti za wadau mbalimbali ndio zinaendelea kufanikisha mbio hizi", aliongeza Marealle.
    Mbio za Kili Marathon zimedhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager (wadhamini wakuu); benki ya Standard Chartered (nusu marathon kwa walemavu), na Vodacom (mbio za kujifurahisha za 5Km). Wadhamini wengine ni Goodyear Tyres, CFAO DT Dobie, New Africa Hotel, Keys Hotels, Kili Water, Tanga Cement, KK Security, TanzaniteOne na Shoprite.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WANARIADHA MAARUFU WAJA KILI MARATHON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top